Select Page

Masomo ya Misa Jumatano ya Pasaka

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 03/04/2024

2024 APRILI 3 : JUMATANO-JUMA LA KWANZA LA PASAKA

Mt. Agape
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

“Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilichonacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende.”

Somo 1. Mdo 3:1-10

Petro na Yohane walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. Mtu huyu akiwaona Petro na Yohane wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka. Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohane, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilichonacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu. Watu wote wakamwona akienda, akimsifu Mungu. Wakatambua, ya kuwa yeye ndiye aliyekuwa akiketi na kuomba sadaka penye mlango Mzuri wa hekalu; wakajaa ushangao wakastaajabia mambo yale yaliyompata.

Wimbo wa Katikati. Zab 105:1-4, 6-9

“1. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake,
Wajulisheni watu matendo yake,
Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote. (K)

K) Bwana anajaza nchi na fadhili zake.

2. Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake sikuzote. (K)

3. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake;
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
Duniani mwote mna hukumu zake. (K)

4. Analikumbuka agano lake milele;
Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.
Agano alilofanya na Ibrahimu,
Na uapo wake kwa Isaka. (K) “

Injili. Lk 24:14-35

Siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao. Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi? Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote;

tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo; tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona. Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je, haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe. Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele. Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao. Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao. Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko? Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao, wakisema, Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni. Nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate.

TAFAKARI

DAIMA UKARIMU UNA FAIDA: Kuna mwanasaikolojia anaitwa Delno Tromp alisema, “urafiki wa kweli ni kushirikishana hata tone la mwisho la maji wakati huna uhakika wa maji mengine.” Hawa wanafunzi wa Emau walimkirimu Yesu kwa kumkaribisha ili ale nao chakula cha jioni bila hata kujua ni Yesu. Walifanya vile kama binadamu tu, lakini matokeo yake Yesu akajifunua kwao na kuwaonesha kuwa ukarimu wao umewaneemesha. Hata Petro na Yohane nao katika somo la kwanza, walimkirimu yule kiwete kwa kumponya na wakamfanya afurahie maisha yake. Jamii yetu leo inakosa ukarimu, wenye nacho wanakosa majitoleo na huruma kwa wasio nacho. Sehemu nyingine imani potofu zimepelekea watu kutosaidiana katika shida kwani ukimsaidia mtu halafu mbeleni akapata taabu, uliyesaidia unaanza kutiliwa shaka, mara anataka amtoe kafara (sadaka-msukule) n.k. Tunasahau kuwa Mungu anatutaka tusaidiane.

SALA: Ee Kristo Mfufuka, utujalie moyo wa ukarimu wa kipasaka.

Masomo ya Misa Machi 20

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 20/03/2024

2024 MACHI 20 JUMATANO: JUMA LA 5 LA KWARESIMA
Mt. Kathbert, Askofu 
Urujuani
Zaburi: Juma 5

Somo 1. Dan 3: 14-20, 91-92,95

Nebukadreza, aliwaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakaye waokoa ninyi na mikono yangu? Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hatuna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha. Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto. Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto.
Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme. Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu. Nebakadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu ila Mungu wao wenyewe.

Wimbo wa Katikati. Dan 3:52-56

1. Umehimidiwa, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu;
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;
Lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. (K)

(K) Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

2. Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu;
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako;
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. (K)

3. Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya makerubi
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
Umehimidiwa katika anga la mbinguni
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)

Injili. Yn 8: 31-42

Yesu aliwaambia wale Wayahudi waliomwamini. Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu  kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo  kweli itawaweka huru.
Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru?
Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani siku zote; mwana hukaa siku zote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. Najua ya kuwa ninyi ni uzao wa Ibrahimu; lakini mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu halimo ndani yenu. Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo.
Wakajibu, wakamwambia, Baba yetu ndiye  Ibrahimu! Yesu akamwambia, Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu. Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo. Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu.
Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu. Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma.

TAFAKARI

USIKIVU UNAHITAJI KUJITAMBUA: Jinsi kutu inavyoharibu na kula chuma, ndivyo ilivyo kwa hasira kuharibu nafsi na fikra za mtu. Katika somo la kwanza tumeona mfalme Nebukadreza anajawa na ghadhabu na hasira na kutoa amri za kuangamizwa kwa moto kwa Shadraka, Meshaki na Abednego. Nebukadreza alikosa usikivu na kutokujitambua. Na katika Injili hawa Wayahudi wanalumbana na Yesu na kujiona kuwa wajuaji, hili nalo ni kukosa usikivu. Kitendo cha hawa waliotajwa katika somo la kwanza kutotetereka katika msimamo wao ni fundisho kwetu kuwa tunapaswa kusimama imara na kutetea imani yetu. Leo hii watu wanayumbayumba kiimani, mara leo yupo Katoliki kesho kwingine. Wanadanganyika. Tunaelezwa katika neno kuwa ‘watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.’ Mtu anaamini kwa kuambiwa kuwa akikanyaga mafuta ndio ataokoka, akinywa maji alioogea mtu eti ndo anapata wokovu, kumwagiwa soda ndio kupata wokovu. Kukosa huku msimamo katika imani kumepelekea wengi kuangamia. 

SALA: Ee Bwana utujalie uimara katika imani.

Masomo ya Misa Machi 19

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 19/03/2024

2024 MACHI 19 JUMANNE: JUMA LA 5 LA KWARESIMA
MT. YOSEFU, MUME WA BIKIRA MARIA
Urujuani
Zaburi: Juma 5

Somo 1. 2 Sam 7:4-5, 12-14, 16

Ikawa usiku huo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema, Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, Siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu, akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.

Wimbo wa Katikati. Zab 89:2-5, 27-29

1. Fadhili za Bwana nitaziimba milele;
Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. (K)

(K) Wazao wake watadumu milele.

2. Nimefanya agano na mteule wangu,
Nimemwapia Daudi, mtumishi wangu.
Wazao wako nitawafanya imara milele,
Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. (K)

3. Yeye ataniita, Wewe baba yangu,
Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
Hata milele nitamwekea fadhili zangu,
Na agano langu litafanyika amini kwake. (K)

Somo 2. Rum 4:13, 16-18, 22

Ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani. kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe, iwe njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila kwa wale wa imani ya Ibrahim; aliye baba yetu sisi sote; (kama ilivyoandikwa nimekuweka kuwa baba wa mataifa Mengi.) Mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako. Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.

Injili. Mt 1:16, 18-21, 24

Yakobo alimzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo.  Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe.

TAFAKARI

FAMILIA NI CHIMBUKO LA KANISA: Leo Mama Kanisa anatualika tumsherehekee Yosefu Mume wa Bikira Maria. Tunaelezwa kuwa katika maisha yake alikuwa mtu wa haki na hakupenda kumdhalilisha mtu yeyote. Alikuwa na mahusiano mazuri na Mungu na hofu ya kwake. Injili imetueleza “alitaka amwache kwa siri.” Katika hili tunajifunza kuwa na utu, kutunza heshima ya mtu hata kama inaonekana katenda kosa. Tuko ambao tunafurahia, kushangilia na kutangaza makosa ya wengine. Kitendo cha Mt. Yosefu kutopenda kuanika hadharani hali ya mwenzi wake (Bikira Maria) ni fundisho kwetu sote. Familia nyingi zimejikuta katika migogoro isiyoisha kutokana na kukosa ustahimilivu wa tabia kama ya Mt. Yosefu. Unakuta wanandoa wanatangazana kwenye mitandao ya kijamii na kuweka wazi madhaifu yao, wanasahau kiapo chao. Kuna mwanasaikolojia anaitwa William Ellery alisema, “uwazi, ukweli na uaminifu hujidhihirisha katika urafiki wa kweli.” Familia nyingi zinakosa hili na hii imepelekea hata Kanisa kuyumba kimaadili na hata maendeleo ya kiroho kwani kitalu halisi cha Kanisa ni familia. Kuyumba kwa familia ni kuyumba kwa Kanisa. 

SALA: Mt. Yosefu mlinzi wa Familia Takatifu, uziombee familia zetu ziishi kwa amani na uelewano.

Masomo ya Misa Machi 18

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 18/03/2024

2024 MACHI 18 JUMATATU: JUMA LA 5 LA KWARESIMA
Mt. Sirili wa Yerusalemu, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Urujuani
Zaburi: Juma 5

Somo 1. Dan 13:1-9, 15-17, 19-30, 33-62

Palikuwa na mtu, jina lake Yoakimu, akikaa Babeli, naye ameoa mke jina lake Susana binti Helkia, mwanamke mzuri sana na mcha Mungu. Wazee wake nao walikuwa wenye haki, pia wamemfundisha binti yao sawasawa na Torati ya Musa. Basi Yoakimu alikuwa mwungwana tajiri, na karibu na nyumba yake alikuwa na bustani nzuri; hivyo Wayahudi humwendea, maana alikuwa mwenye heshima kupita wengineo wote. Mwaka ule ule wakaamriwa wawili miongoni mwa wazee wa watu ili kuamua, watu wa namna ile ambao Bwana aliwanena, ya kama ufisadi ulitoka Babeli kwa wazee waamuzi waliohesabiwa kuwa wanatawala watu. Hao walikuwa wakienda mara nyingi kuzuru kwenye nyumba yake Yoakimu; na wote wenye mashtaka yo yote desturi yao wakawajia huko. Basi watu walipoondoka kwenda zao panapo saa sita, Susana huingia katika bustani ya mumewe ili kutembea. Nao wale wazee wawili humwona kila siku anakwenda kutembea; hata wakawaka tamaa kwa sababu yake. Ndipo walipozipotosha nia zao, wakayageuza upande macho yao wasiweze kutazama mbinguni wala kukumbuka hukumu za haki.  Ikawa, walipongoja wakati wa kufaa, yeye aliingia bustanini kama ilivyokuwa desturi yake pamoja na wajakazi wawili, naye alitaka kuoga kwa sababu kulikuwa na joto. Wala hapo hapakuwa na mtu ye yote isipokuwa wale wazee wawili, ambao wamejificha wakimvizia. Basi akawaambia wajakazi wake, Nileteeni mafuta na sabuni, mkaifunge milango ya bustani ili nioge.
 Mara, wale wajakazi walipokwisha kutoka, wale wazee wawili waliondoka wakamwendea mbio, wakasema, Tazama, milango ya bustani imefungwa asiweze kutuona mtu ye yote, nasi tunakupenda sana; haya! Basi, utukubali ulale nasi. La! Hutaki; tutakushuhudia ya kuwa hapa palikuwapo na kijana pamoja nawe, ndio sababu uliwaruhusu wajakazi wako. Basi Susana aliugua, akasema, Nimesongwa pande zote; maana nikilitenda hilo ni mauti yangu; nisipolitenda siwezi kuokoka mikononi mwenu. Ni  afadhali nianguke katika mikono yenu na kukataa, kuliko kutenda dhambi machoni pa Mungu. Mara Susana akapiga kelele kwa sauti kuu; nao wale wazee wawili wakampigia kelele pia. Kisha mmoja wao akakimbia, akaifungua milango ya bustani. Hivyo watumishi wa nyumbani waliposikia kelele bustanini, wao waliingia kwa kasi kwa mlango wa nyuma ili waone ni nini iliyompata. Lakini wale wazee waliisimulia hadithi yao, nao watumishi wakaona aibu kabisa; kwa maana Susana hakuchongelewa habari ya namna hiyo wakati  wo wote.  Ikawa, kesho yake watu walipokusanyika kwa Yoakimu mumewe, wale wazee wawili wakaja nao, wamejaa kusudi lao ovu juu ya Susana la kumfisha; wakasema mbele ya watu, mwiteni Susana binti Helkia, mkewe Yoakimu, aje hapa. Basi akaenda kuitwa; naye akaja pamoja na baba yake na mama yake, na watoto wake pamoja na jamaa zake zote. Kwa hiyo rafiki zake na wote waliomtazama wakasikitika. Ndipo wale wazee wawili waliposimama katikati ya watu wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. Naye akatoka machozi, akatazama juu mbinguni; kwa maana moyo wake alimtumaini Mungu. Wale wazee wakasema, sisi tulipoitembelea bustani peke yetu, huyu aliingia pamoja na wajakazi wawili, wakaifunga milango ya bustani, naye mara akawaruhusu wajakazi. Kisha, kukatokea kijana, ambaye amejificha humo, akamwendea akalala naye. Walakini sisi tungaliko pembeni mwa bustani, tuliuona ubaya huo, tukawaendea mbio. Hata tukiwa tumewaona pamoja, yule kijana hatukuweza kumkamata; maana alikuwa mwenye nguvu kuliko sisi, akaifungua milango akaepuka. Bali huyu tulimkamata, tukauliza yule kijana yu nani, asikubali kutuambia. Hayo, basi, tunashuhudu.
Basi, waliohudhuria wakawasadiki, wakiwa wazee wa watu na waamuzi; hivyo wakahukumu auawe. Mara Susana akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Mungu wa milele, Wewe wajua yaliyositirika, wajua mambo yote yasijekuwako, wewe wajua ya kwamba wananishuhudia uongo, na, tazama, imenipasa kufa; walakini sikufanya kamwe mambo kama hayo, ambayo watu hawa wameyabuni juu yangu kwa ukorofi. Naye Bwana akaisikia sauti yake. Kwa hiyo, alipochukuliwa huyo kwenda kuuawa, Mungu alimchochezea roho kijana mmoja, jina lake Danieli; naye akapaza sauti yake akasema, Mimi simo; mimi sina hatia kwa habari ya damu yake mwanamke huyu. Mara wote wakamgeukia, wakasema, maneno hayo uyasemayo maana yake nini? Akasimama katikati, akasema, Enyi bani Israeli, mmekuwa wapumbavu, hata kumhukumu binti Israeli bila kuhoji wala kupata hakika ya kweli? Rudini hukumuni; mradi hao wanamshuhudia uongo. Basi watu wote walirijea kwa haraka, nao wale wazee wakamwambia, njoo uketi kati yetu, utujulishe habari hiyo, endapo Mungu amekupa wewe heshima ya mzee. Hapo Danieli aliwaambia, watu hawa wawili watengwe, nami nitawahoji. Basi wakiisha kutengwa akamwita mmoja wao akamwambia, Ewe uliyepata kuwa mzee katika uovu, sasa dhambi zako zimekukalia, ulizozitenda zamani kwa kuhukumu isivyo haki, kumpatiliza asiye na hatia na kumwachilia mwovu; lakini Bwana asema, asiye na hatia mwenye haki, usimwue. Haya! Basi, wewe ulimwona kwa macho; useme; Chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, chini ya msandarusi. Danieli akasema, hakika umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana sasa hivi malaika wa Mungu amepokea hukumu ya Mungu, akukate vipande viwili. Akamtenga huyo tena, akaamuru kumleta yule mwingine, akamwambia, Ewe mzao wa Kanani, wala si wa Yuda, uzuri umekudanganya, na tamaa imeupotosha moyo wako. Hivyo ndivyo ulivyowafanyia binti za Israeli, na kwa hofu walitembea nawe; bali huyu binti Yuda hakuweza kustahimili uovu wako. Haya! Basi, nawe useme; chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, chini ya mkwaju. Danieli akamwambia, hakika wewe nawe umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana malaika wa Mungu yu tayari, anakungoja mwenye upanga, akukate vipande viwili; ili awaangamize wote wawili. Mara hiyo makusanyiko yote wakapaza sauti kwa nguvu, wakamhimidi Mungu awaokoaye wamtumainio. Wakawaondokea wale wazee wawili, kwa maana Danieli ameuhakikisha ushuhuda wao wa uongo hata vinywani mwao wenyewe. Wakawatenda kwa torati ya Musa kama vile walivyokusudia kwa ukorofi kumfanyia jirani yao; wakawaua; na mwenye damu isiyo na hatia aliokolewa siku ile.

Wimbo wa Katikati. Zab 23

1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
    Sitapungukiwa na kitu.
    Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
    Kando ya maji ya utulivu huniongoza. (K)


(K) Nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
       Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami. 
 

2. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza
    Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
    Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti
    Sitaogopa mabaya; kwa maana Wewe upo pamoja nami. (K)

3. Waandaa meza mbele yangu,
    Machoni pa watesi wangu.
    Umenipaka mafuta kichwani pangu,
    Na kikombe changu kinafurika. (K)

4.  Kakika wema na fadhili zitanifuata,
     Siku zote za maisha yangu,
     Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)

Injili. Yn 8: 1-11

Walikwenda kila mtu nyumbani kwake; naye Yesu akaenda mpaka mlima wa Mizeituni. Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha. Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati.Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.

TAFAKARI

MUNGU NI MWEMA KWA WAMCHAO: Upo msemo kwamba “mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.” Masomo yote ya leo yanasimulia wanawake wanaoonekana kutotendewa haki, kuonewa, kukandamizwa. Somo la kwanza wahusika wanawakwa na tamaa ya mapenzi na kumshitaki kwa uongo Suzana, baada ya vionjo vyao kutotimizwa. Sio wote walioko magerezani ni watenda maovu, wapo waliopelekwa huko kwa kusingiziwa uongo toka kwa wenye nazo (mali/madaraka). Ni dhana kama hii Yesu anairekebisha katika tuhuma dhidi ya huyu mwanamke wa Injili kuwa “asiye na dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe.” Yesu aliwataka wajichunguze dhamiri zao na ndio maana waliondoka wote baada ya kujitambua kuwa nao sio wakamilifu. Tuelewe hakuna aliyekamilika, sote tunakazana kuelekea ukamilifu. Tusiwe tu watu wa kuongozwa na vionjo na hisia za mwili na kuvuruga mpango mzima wa maisha.

SALA: Ee Mungu tupe ujasiri wa kutetea haki za watu bila woga.

Masomo ya Misa Machi 17

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 17/03/2024

2024 MACHI 17: DOMINIKA YA 5 YA KWARESIMA
Urujuani
Zaburi: Juma 1

Somo 1. Yer 31 :31-34

Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.  Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongo mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.

Wimbo wa Katikati. Zab 51: 3-4, 12-15

1. Ee Mungu unirehemu,
Sawasawa  na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema sako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu. (K)

(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi. 

2. Ee Mungu uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)

3. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho wa wepesi.
Nitawafundisha wakosaji njia zako,
Na wenye dhambi watarejea kwako. (K)

Somo 2. Ebr 5: 7-9

Yesu, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii..

Injili. Yn 12 :20-33

Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu. Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu. Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu.  Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu. Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataingamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu. Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemaje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii. Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena. Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika amesema naye. Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu,  bali kwa ajili yenu. Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.  Aliyanena hayo akionyesha ni mauti gani atakayokufa.

TAFAKARI

TUNAKUWA WAFU KATIKA UTU WA KALE NA KUWA HAI KATIKA KRISTO
Dominika ya tano ya Kwaresima inatuingiza katika tafakari ya mateso ya Kristo tukielekea katika kilele cha majira haya ya toba. Hii haimaanishi kwamba sasa kipindi cha toba kimekwisha bali kinatupatia maana ya toba yetu, yaani kutufikisha katika matunda ya fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tendo la toba linatualika kufanya mabadiliko ya maisha ambapo ni kuuvua utu wa kale, utu wa dhambi na kuuvaa utu mpya katika Kristo. Namna hiyo ya kuanza upya inafanyika ndani kabisa mwa nafsi ya kila mmoja wetu kwa kuuvua utu wake wa kale, utu wa dhambi na kuuvaa utu mpya.
Katika somo la kwanza mwanzo huu mpya unaonekana katika namna ambavyo Bwana atafanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. “Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika.” Upya huu unaonekana katika mahali itakapoandikwa sheria: si katika vipande vya mawe au juu ya vibao bali katika mioyo yao. Sheria inaandikwa si nje tena bali ndani ya moyo wa mwanadamu. Upya huu utawafanya wana wa Israeli kutoweza kuivunja Sheria ya Mungu kwani inakuwa ni sehemu ya maisha yao. Zaidi ya hapo hawatakuwa wanafundishwa na jirani kwani kila mmoja ataisikia ikiita ndani mwake. (Fumbo la umwilisho linauunganisha umungu na ubinadamu na kuwezeshwa kuijongea njia ya wokovu)
Tukiiangalia kidogo antholopolija ya kiyahudi tutaelewa zaidi mantiki ya andiko hili la Mungu kupitia kinywa cha nabii Yeremia. Wayahudi walitumia neno «leb» kuwakilisha moyo, neno ambalo lilimaanisha uwezo wa mwanadamu kiakili na kimaamuzi. Sheria inayoandikwa nje ya moyo haigusi moja kwa moja ufahamu na maamuzi ya mwanadamu na hivyo ni rahisi kusahaulika ama kuvunjwa. Hivyo sheria ilipoandikwa katika moyo ilihakikisha kuwa sasa mwanadamu atatambua nini anaelekezwa na pia atakuwa na uwezo wa kufanya uamuzi. Ni yeye mwenyewe anakuwa hakimu wa matendo yake kwani maelekezo yote yapo ndani mwake na utekelezaji wake pia unamtegemea yeye.
Hii ni ishara ya utu mpya tunaouvaa katika Kristo; tunaondolewa utu wa kale ambao ulitufanya kuwa wafu na kuvikwa utu mpya katika Kristo. Wayunani wanaotamani kumwona Kristo wanaelekezwa mara moja katika mwelekeo huo wa maisha. Pengine walishasikia habari zake wakiwa katika nchi yao au wakati walipokuwa wanafika Yerusalemu kuabudu na wakatamani kumwona. Hatuambiwi sababu za  tamanio lao lakini mafundisho anayounganisha Kristo mara yanatueleza mara moja ni nini ambacho tunapaswa kitendeke ndani mwetu kusudi tuweze kumwona; huku ni kufanywa upya katika yeye; ni kuipokea hiyo «leb» yake ili tuweze kumwelewa na kutenda kama yeye. Fumbo la umwilisho linauunganisha umungu na ubinadamu na kuwezeshwa kuijongea njia ya wokovu.
Kristo anatumia mfano wa kufa kwa mbegu ili kuweza kuzaliwa upya: “Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa hutoa mazao mengi.” Katika sayansi ya kilimo tunaelewa kuwa kuchipuka kwa mbegu kunatudai kuiweka ardhini ili kupitia hatua za kibailojia. Hii haijalishi mbegu hiyo ni nzuri au inavutia kiasi gani; uzuri wake unapata maana pale tu inapotoa mazao zaidi na hii ni kwa njia ya kuwekwa ardhini, kufa na kutoa mche ambao utazaa mbegu nyingine. Mkulima akiing’ang’ania na kuifurahia kwa kuiangalia tu ataishia kufa njaa tu kwani hatakuwa na chakula cha kutosha. Utayari wake wa kuiweka ardhini hufanya kuzaliwa kwa maisha mapya na kupata wingi wa mazao..
Huu ni mwaliko wa kuwa tayari kubadili mtindo wa kale wa maisha kusudi kumfikia na kumwona Yesu. Kamwe hatuwezi kumwona Yesu wakati tumeng’ang’aniwa na uzuri, umaridadi, umaarufu wa kidunia. Tunapaswa kuwa tayari kuvifukia ardhini ili tuchipuke tukiwa wapya katika Yeye. Suala la wokovu au kuwa karibu na Kristo si suala la muda mfupi na la kupita tu, bali ni lile linalobadilisha maisha yako yote. Si rahisi kuwa na Kristo wakati upo katika hali ya mchanganyo: upo kanisani lakini bado umefunga hirizi; unatakiana amani na wenzako wakati bado una kinyongo na jirani yako uliyemwacha nyumbani; unaomba utakaso wa dhambi wakati bado miundo mbinu yake umeihifadhi na upo tayari kuirudia baadaye na kadhalika.
Kristo anajiweka kwetu kama kielelezo na anataadharisha wale wanaopenda nafsi zao kiasi cha kushindwa kuzitoa ili kuzaliwa upya. “Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.” Ni kwa njia ya kumfuata Yeye tu na kuuacha utu wetu wa kale ndipo tutaweza kupata huo upya wa maisha: “Mtu akinitumikia na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo.” Tunapotaka kumwona Kristo tunapaswa kumfuata katika njia yake na hivyo tutakuwa naye mahali atakapokuwapo. Hata katika hali ya mateso, au mfadhahiko, au mahangaiko, yote tuyapitie tukichuchumilia kufikia pale Kristo alipo.
Ndivyo anavyotuasa Mtakatifu Paulo kupita katika njia ya mateso. Kristo analiona tendo hilo kama kutimilika kwa saa yake ya kumtukuza Mungu. Utilimilifu huu ni kilele cha utume wake hapa ulimwenguni ambapo atakamatwa na kuteswa na mwisho kuuawa juu msalabani; anaiona kuwa ndiyo saa muafaka kwake Yeye kama chembe ya ngano kufukiwa ardhini, kufa na hatimaye kuzaa matunda ya wokovu. Yeye anakuwa tayari kuipokea saa hiyo na anakiri ndiyo namna ya kumtukuza Mungu.
“Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii. Baba, ulitukuze jina lako.” Ni maneno ya Kristo ambayo yanatufundisha mambo mawili kwanza ni utayari wa kulitukuza jina na Mungu, yaani kuyafanya mapenzi yake kutimia hata katikati ya mateso mengi. Na pili ni nafasi ya Mungu katika kulitimiza hilo. Hapa tunauona uwezo wa Mungu unatenda katika uhuru wa mwanadamu. Ni namna ya juu kabisa ambayo mwanadamu anaudhihirisha uhuru wake kwa utii wa mapenzi ya Mungu. Mungu ndiye chanzo na asili ya yote mema tunayotenda; ameweka ndani mwetu uwezo wa kuyapokea mema yake na pia anatupatia uhuru wa kuyakubali mema hayo.
Kristo alikubali kumtukuza Mungu hadi kifo cha msalabani na kwa namna hiyo Mungu “alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina” (Flp 2:9). Ukristo wetu unatuita katika kumtukuza Mungu kwa namna hii; vinginevyo tunabaki tumedumaa na kutokukua katika utu wetu na utakatifu. Kwaresima yanatupatia fursa ya kuomba neema ya Mungu na kufanya mabadiliko ya kweli na kuzaliwa upya katika Kristo. Ni hakika tunakuwa na hamu ya kumwona Kristo, lakini hamu hiyo ijidhihirishe katika kumfuata mahali alipo kwa kuyasadaka maisha yetu ya kale na kuzaliwa upya katika Yeye na hivyo daima kumtukuza Mungu kwa maisha yetu.

SALA: Ee Bwana utujalie kufa katika Kristo ili tupate kuzaa matunda.

Masomo ya Misa Machi 16

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 16/03/2024

2024 MACHI 16 JUMAMOSI: JUMA 4 LA KWARESIMA
Mt. Heriberti, Askofu wa Koloni
Urujuani
Zaburi: Juma 4

Somo 1. Yer 11: 18-20

Bwana akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo uliponionyesha matendo yao. Lakini mimi nalikuwa kama mwana-kondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, ”Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena.” Lakini, Ee Bwana wa majeshi, uhukumuye haki ujaribuye viuno na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.

Wimbo wa Katikati. Zab 7:2-3, 9-12

1. Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe,
Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.
Asije akaipapura nafsi yangu kama simba,
Akiivunja vunja pasipokuwa na wa kuponya. (K)

(K) Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe.

2. Bwana, unihukumu mimi,
Kwa kadiri ya haki yangu,
Sawasawa na unyofu nilio nao.
Ubaya wao wasio haki na ukome,
Lakini mthibitishie mwenye haki. (K)

3. Ngao yangu ina Mungu,
Awaokoaye wanyofu wa moyo.
Mungu ni mwamuzi mwenye haki,
Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku. (K)

Injili. Yn 7: 40-53

Wengine katika mkutano walipoyasikia maneno ya Yesu, walisema, ”Hakika huyu ndiye nabii yule.” Wengine walisema, ”Huyu ndiye Kristo.” Wengine wakasema, ”Je, Kristo atoka Galilaya? Andiko halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa Daudi?” Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake. Baadhi yao wakataka kumkamata, lakini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika. Basi wale watumishi wakawaendea wakuu wa makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia, ”Mbona hamkumleta?” Wale watumishi wakajibu, ”Hajanena kamwe mtu yeyote kama huyu anavyonena.” Basi Mafarisayo wakawajibu, ”Je, ninyi nanyi mmedanganyika?” Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo?” Lakini makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa. Akawaambia ”Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea zamani, maana ni mmoja wao), Je, Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo? Wakajibu, wakamwambia, ”Je, Wewe nawe umetoka Galilaya! Tafuta, ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokea nabii.

TAFAKARI

DAIMA UKWELI HAUPINGIKI: Wakati wa utume wa Yesu, kila mara alikuwa akigusa maisha ya ile jamii na kuwaeleza ukweli. Wapo waliokubaliana na alichosema na wapo waliopinga. Wengine kwa kutambua hili na kutokukubali kubadilika, walikuwa wanatafuta ushawishi wa kuungwa mkono ili kujenga chuki dhidi ya Yesu. Kanisa nalo katika nyakati hizi linapitia katika misukosuko na kadhia kama hizi, kukataliwa. Hata Yohani Mbatizaji aliuawa kwa sababu ya kueleza ukweli kwa Herode. Wapo mapadre walishafitiniwa kwa uongozi wa juu wa Kanisa na hata kuhamishwa toka parokia hii kwenda ile kutokana na kusimamia ukweli. Tunaalikwa daima tuwe watu wa ukweli kama Nicodemo, tusiwe bendera fuata upepo, tuwe watu wenye uchunguzi wa kina na kuwa kabla ya kuchukua maamuzi. 

SALA: Ee Bwana tunakuomba utujalie kumpokea Kristo na kuyapokea mafundisho yake.