Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 28/04/2024
2024 APRILI 28 : DOMINIKA YA TANO YA PASAKA
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 1
Somo 1. Mdo 9: 26-31
Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina lake Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka. Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao wakajaribu kumwua. Lakini ndugu walipopata habari wakamchukua mpaka Kaisaria, wakampeleka aende Tarso. Basi Kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu.
K) Kwako, Bwana, zinatoka sifa zangu katika kusanyiko kubwa. |
Wimbo wa Katikati. Zab 22: 26- 28, 30-32
“1. Nitaziondoa nadhiri zangu
Mbele yao wamchao.
Wapole watakula na kushiba,
Wamtafutao Bwana watamsifu;
Mioyo yenu na iishi milele. (K)
2. Miisho yote ya dunia itakumbuka
Na watu watamrejea Bwana;
Jamaa zote za mataifa watamsujudia.
Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu,
Humwinamia wote washukao mavumbini. (K)
3. Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake,
Wazao wake watamtumikia.
Zitasimuliwa habari za Bwana,
Kwa kizazi kitakachokuja,
Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake,
Ya kwamba ndiye aliyefanya. (K)
“
Somo 2. 1 Yoh 3: 18-24
Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake, ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote. Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri. Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye, naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa.
Injili. Yn 15: 1-8
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamuwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.
TAFAKARI
“NI KATIKA KRISTO TUTAZAA MATUNDA
Moja ya changamoto inayoikabili jamii ya mwanadamu leo hii ni migawanyiko na ubinafsi kati ya wanadamu. Hali hii ni tishio kwa ustawi wa utu wa mtu na hupambwa na matendo mengi yenye kuungamiza ubinadamu wetu. Kila mmoja anajiamulia kadiri aonavyo inafaa na kujiwekea taratibu za kimaisha zinazoendana na vionjo au mawazo yake. Hivyo unyonyaji, ukiukwaji wa haki za wengine, mauaji, dhuluma na mengine mengi yanaupinga ubinadamu na bila binadamu huyu kujisikia katika dhamiri yake anatenda vibaya dhidi ya ndugu yake. Bila kuwa na chimbuko moja la uhai wetu kimaadili ni aghalabu kuujenga umoja na kuonja athari za migawanyiko hii. Dominika ya leo inatualika jamii nzima ya waamini kujitathimini na kuimarisha umoja wetu unaojijenga katika Kristo Mfufuka. Yeye anajitambulisha kwetu kuwa ni mzabibu ambao matawi yake ni sisi tunaomfuasa. Hivyo tunavyobaki katika mzabibu huo kama matawi na Yeye akiwa shina letu tunatajirishwa na kuuhishwa na yeye na pia kuwa katika hali ya umoja wa kindugu.
Kristo anaanza kwa kujitambulisha kama mzabibu wa kweli: “Mimi ndimi mzabibu wa kweli na Baba yangu ni mkulima.” Yatosha kurejea nyuma na kutafakari taswira ya mzabibu katika Agano la Kale. Taifa la Israeli lilipewa haiba hiyo lakini mara nyingi lilizaa zabibu mwitu (rej. Isa 5:1- 7). Hapa kuna tofauti kati ya mzabibu wa kweli na “mzabibu mwitu”. Mzabibu mwitu unazaa zabibu mwitu ambazo ni chukizo na hazifai kwa matumizi na kinyume chake mzabibu wa kweli huzaa matunda halisi. Umuhimu wa Kristo kama mzabibu unaonekana katika muunganiko wake na Mungu Baba. Yeye aliye shina la mzabibu anachota yote kutoka kwa Baba na hivyo kuweka mbele yetu kipimo kimoja na chanzo kimoja kwa utendaji wetu na uwepo wetu sisi. Kristo anajitambulisha katika taswira ya mzabibu na kutuunganisha sisi katika mzabibu huo kama matawi yake: “nanyi mu matawi yangu.” Matawi haya yataweza kuzaa pale tu yatakapobaki yameungana na tawi. Bila kukaa katika Yeye hatuwezi kuzaa matunda: “kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokuwa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu.”
Dominika iliyopita Kristo alijitanabaisha katika haiba ya Mchungaji Mwema akiwahakikishia Kondoo wake usalama pale wanapokuwa chini ya ulinzi wake (rej. Yn 10:28 -29). Dhana hiyo inaunganika na tafakari ya Dominika hii katika wazo la kuwa na umoja na Kristo. Hakika ya usalama wetu katika Kristo inajifunua au inajidadavua vizuri kwa kuuona na kuutambua umoja tunaoupata kwake kwa njia ya fumbo la umwilisho. Fumbo la umwilisho limetuunganisha na Kristo na matunda yake ni ukombozi wetu wanadamu. Fumbo hili linatuunganisha na Kristo na kwa njia yake tunaunganika sote kama ndugu katika Kristo. Migawanyiko na matendo maovu ya kibinadamu yanayoambatana nayo hupata mwarobaini katika tendo hili. Hivyo mahali popote katika jamii ya mwanadamu kunapoonekana cheche za migawanyiko na matunda yake maovu tunakumbushwa mara moja kumtambua na kumkumbatia Kristo kama mzabibu ambao sisi tulio matawi yake tunapobaki katika yeye na kuungana naye tunazaa matunda ya umoja na upendo katika jamii ya wanadamu. “Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda Baba yangu huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.” Muunganiko wetu na mzabibu kama matawi kunatudai kutoa matunda. Kwa maneno mengine ukombozi wetu unatutuma katika ushuhuda wa maisha. Imani tunda ambalo linaendelea kukua na kukomaa kila siku.
Somo la pili la Dominika hii linatuelekeza katika hilo na kutuonya katika kutekeleza nyajibu zetu mbalimbali kwa dhamiri iliyo safi, namna ambayo hutufanya kuzaa matunda ya kweli: “Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli.” Ipo hatari ya kuifurahia au kuifuatilia imani kwa bidii wakati wa faraja na kuikimbia wakati wa madhulumu. Ni changamoto katika kuilinda imani hata kama inahatarisha uhai wako kwa namna yoyote ile. Dhamiri safi ambayo hutusukuma kuzaa matunda mema inatubidisha hata katika hali ya kuwa tayari kutia mchanga kitumbua chako ili mradi umeusimamia ukweli. Maangamizi mengi ya utu wa mtu husababishwa na uzembe wangu au wake katika kutotimiza wajibu tuliopewa inavyotakikana. Nabaki katika ubinafsi wangu na kutojali kuangamia kwa mwenzangu. Najisahau kwamba nimeungana na shina la mzabibu na ninapaswa kuzaa matunda.
Muungano wetu na Kristo kama matawi katika Yeye aliye mzabibu hutupatia hamasa. Hizi ni neema na baraka kutoka mbinguni ambazo kwazo tunachota ujasiri na kukemea au kurekebisha au kusema ukweli kwa ajili ya manufaa ya mwanadamu kadiri ya mapenzi ya Mungu. Huku ndiko kuzaa matunda. Tunaposhindwa kuzaa matunda ukristo wetu unabaki kuwa butu na imani yetu inakosa ladha. Lakini tunapozaa matunda Baba hutusafisha na kuzaa zaidi. Neno la Mungu na mafundisho mbalimbali ya Kanisa hutupatia virutubisho kwa ajili ya kuzaa hayo matunda. Ni namna gani tunajitajirisha na nyenzo hizo ndiyo hakika ya kuzaa matunda mema na mengi. Huwezi kupata zabibu katika michongoma. Jiulize, nini ambacho kwako ni chakula kwa ajili ya roho yako na kuimarisha imani yako? Ni changamoto kubwa sana na hasa katika mazingira ya ulimwengu wa leo wenye teknolojia ya habari na mawasiliano isiyochujwa chini ya mitandao ya kijamii. Tuangalie tusije tukawa ndani ya mzabibu lakini tunakataa au kuzuia kushibishwa na utajiri unaotoka kwake huku tukitegemea kutoka nje ya mzabibu. Kwa hakika tutakakwa na kutupwa nje.
Sauli anakuwa kwetu mfano mzuri wa yeye ambaye ameungana na mzabibu na kuzaa matunda. Ingawa mwanzoni hakupokelewa kwa sababu ya historia yake ya kulidhulumu Kanisa, yeye hakukatishwa tamaa na pia alisaidiwa na utambulisho wa Barnaba. “Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani.” Umisionari wetu unatuelekeza katika mambo hayo mawili: kwanza kuhubiri kwa jina la Bwana. Yeye aliye shina letu ndiye chanzo cha yote tuhubiriyo na zaidi Yeye aliye ufunuo wa Baba anatufanya tuyatimize mapenzi ya Baba kwa kuungana naye. Pili ni kuhubiri kwa ushujaa, yaani bila kuogopa na kwa bidii yote. Juhudi ya Sauli inazaa matunda: “Kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likaendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu.”
Umoja wetu na Kristo Mfufuka ambaye ni shina la mzabibu udhihirike kwa matendo yetu mema ya kindugu kati yetu sisi kwa sisi. Dominika ya leo tunakumbushwa kurejea na kuwa na shina au chanzo kimoja ambacho kinatoa maana ya maisha yetu kiroho na kimaadili. Yeye ni Kristo Mzabibu wa kweli. Ni mwaliko wa kuinuia macho na kuona umuhimu wa Mwenyezi Mungu katika maisha yangu na hivyo kuimba kama Mzaburi anayesema: “Kwako Bwana, zinatoka sifa zangu katika kusanyiko kubwa.” Hapa tutaweza kweli kuwa wamoja katika Kristo na aliye Njia, Ukweli na Uzima wetu (rej. Yn 14:6). Muunganiko wetu na Kristo kama shina la mzabibu wa kweli unatupatia fursa ya kushibishwa kwa pamoja kwa njia yake na hivyo kuifunua mioyo yetu kwa ajili ya wenzetu.”
SALA: Ee Yesu utupe neema ya kuungana nawe zaidi. |