Select Page

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 16/03/2024

2024 MACHI 16 JUMAMOSI: JUMA 4 LA KWARESIMA
Mt. Heriberti, Askofu wa Koloni
Urujuani
Zaburi: Juma 4

Somo 1. Yer 11: 18-20

Bwana akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo uliponionyesha matendo yao. Lakini mimi nalikuwa kama mwana-kondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, ”Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena.” Lakini, Ee Bwana wa majeshi, uhukumuye haki ujaribuye viuno na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.

Wimbo wa Katikati. Zab 7:2-3, 9-12

1. Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe,
Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.
Asije akaipapura nafsi yangu kama simba,
Akiivunja vunja pasipokuwa na wa kuponya. (K)

(K) Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe.

2. Bwana, unihukumu mimi,
Kwa kadiri ya haki yangu,
Sawasawa na unyofu nilio nao.
Ubaya wao wasio haki na ukome,
Lakini mthibitishie mwenye haki. (K)

3. Ngao yangu ina Mungu,
Awaokoaye wanyofu wa moyo.
Mungu ni mwamuzi mwenye haki,
Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku. (K)

Injili. Yn 7: 40-53

Wengine katika mkutano walipoyasikia maneno ya Yesu, walisema, ”Hakika huyu ndiye nabii yule.” Wengine walisema, ”Huyu ndiye Kristo.” Wengine wakasema, ”Je, Kristo atoka Galilaya? Andiko halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa Daudi?” Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake. Baadhi yao wakataka kumkamata, lakini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika. Basi wale watumishi wakawaendea wakuu wa makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia, ”Mbona hamkumleta?” Wale watumishi wakajibu, ”Hajanena kamwe mtu yeyote kama huyu anavyonena.” Basi Mafarisayo wakawajibu, ”Je, ninyi nanyi mmedanganyika?” Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo?” Lakini makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa. Akawaambia ”Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea zamani, maana ni mmoja wao), Je, Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo? Wakajibu, wakamwambia, ”Je, Wewe nawe umetoka Galilaya! Tafuta, ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokea nabii.

TAFAKARI

DAIMA UKWELI HAUPINGIKI: Wakati wa utume wa Yesu, kila mara alikuwa akigusa maisha ya ile jamii na kuwaeleza ukweli. Wapo waliokubaliana na alichosema na wapo waliopinga. Wengine kwa kutambua hili na kutokukubali kubadilika, walikuwa wanatafuta ushawishi wa kuungwa mkono ili kujenga chuki dhidi ya Yesu. Kanisa nalo katika nyakati hizi linapitia katika misukosuko na kadhia kama hizi, kukataliwa. Hata Yohani Mbatizaji aliuawa kwa sababu ya kueleza ukweli kwa Herode. Wapo mapadre walishafitiniwa kwa uongozi wa juu wa Kanisa na hata kuhamishwa toka parokia hii kwenda ile kutokana na kusimamia ukweli. Tunaalikwa daima tuwe watu wa ukweli kama Nicodemo, tusiwe bendera fuata upepo, tuwe watu wenye uchunguzi wa kina na kuwa kabla ya kuchukua maamuzi. 

SALA: Ee Bwana tunakuomba utujalie kumpokea Kristo na kuyapokea mafundisho yake.