Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 20/03/2024

2024 MACHI 20 JUMATANO: JUMA LA 5 LA KWARESIMA
Mt. Kathbert, Askofu 
Urujuani
Zaburi: Juma 5

Somo 1. Dan 3: 14-20, 91-92,95

Nebukadreza, aliwaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakaye waokoa ninyi na mikono yangu? Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hatuna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha. Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto. Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto.
Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme. Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu. Nebakadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu ila Mungu wao wenyewe.

Wimbo wa Katikati. Dan 3:52-56

1. Umehimidiwa, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu;
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;
Lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. (K)

(K) Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

2. Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu;
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako;
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. (K)

3. Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya makerubi
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
Umehimidiwa katika anga la mbinguni
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)

Injili. Yn 8: 31-42

Yesu aliwaambia wale Wayahudi waliomwamini. Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu  kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo  kweli itawaweka huru.
Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru?
Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani siku zote; mwana hukaa siku zote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. Najua ya kuwa ninyi ni uzao wa Ibrahimu; lakini mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu halimo ndani yenu. Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo.
Wakajibu, wakamwambia, Baba yetu ndiye  Ibrahimu! Yesu akamwambia, Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu. Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo. Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu.
Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu. Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma.

TAFAKARI

USIKIVU UNAHITAJI KUJITAMBUA: Jinsi kutu inavyoharibu na kula chuma, ndivyo ilivyo kwa hasira kuharibu nafsi na fikra za mtu. Katika somo la kwanza tumeona mfalme Nebukadreza anajawa na ghadhabu na hasira na kutoa amri za kuangamizwa kwa moto kwa Shadraka, Meshaki na Abednego. Nebukadreza alikosa usikivu na kutokujitambua. Na katika Injili hawa Wayahudi wanalumbana na Yesu na kujiona kuwa wajuaji, hili nalo ni kukosa usikivu. Kitendo cha hawa waliotajwa katika somo la kwanza kutotetereka katika msimamo wao ni fundisho kwetu kuwa tunapaswa kusimama imara na kutetea imani yetu. Leo hii watu wanayumbayumba kiimani, mara leo yupo Katoliki kesho kwingine. Wanadanganyika. Tunaelezwa katika neno kuwa ‘watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.’ Mtu anaamini kwa kuambiwa kuwa akikanyaga mafuta ndio ataokoka, akinywa maji alioogea mtu eti ndo anapata wokovu, kumwagiwa soda ndio kupata wokovu. Kukosa huku msimamo katika imani kumepelekea wengi kuangamia. 

SALA: Ee Bwana utujalie uimara katika imani.