Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 30/04/2024

2024 APRILI 30 : JUMANE-JUMA LA TANO LA PASAKA

Mt. Pio V, Papa
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 1

Somo 1. Mdo 14:19-28

Wayahudi walifika toka Antiokia na Ikonio, wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji, wakidhani ya kuwa amekwisha kufa. Lakini wanafunzi walipokuwa wakimzunguka pande zote, akasimama, akaingia ndani ya mji; na siku ya pili yake akatoka, akaenda zake pamoja na Barnaba mpaka Derbe. Hata walipokwisha kuhubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi. Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini. Wakapita kati ya Pisidia wakaingia Pamfilia. Na baada ya kuhubiri lile neno katika Perge wakatelemka mpaka Atalia. Na kutoka huko wakaabiri kwenda Antiokia. Huko ndiko walipoombewa neema ya Mungu kwa ile kazi waliyokwisha kuitimiza. Hata walipofika wakalikutanisha kanisa, wakawaeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia mataifa mlango wa imani. Wakaketi huko wakati usiokuwa mchache, pamoja na wanafunzi.

(K). Watawajulisha watu matendo yake makuu, Na utukufu wa fahari wa zamani zote. 

Wimbo wa Katikati. Zab 145:10-13, 21

“1. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako,
Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
Na utukufu wa fahari ya ufalme wake. (K)

2. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)

3. Kinywa change kitazinena sifa za Bwana;
Wote wenye mwili na walihimidi jina lake takatifu
milele na milele. (K)”

Injili. Yn 14:27-31

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba; kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini. Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.

TAFAKARI

KRISTO NI AMANI YETU YA KWELI: Yesu anawaachia wafuasi wake kati ya zawadi kubwa za kipasaka: Amani. Kristo anajitofautisha na dunia hata katika kutoa amani. Yeye anatuachia amani ambayo dunia haiwezi kuitoa. Amani ya dunia hii ni ya muda, ndio maana mpaka leo dunia inashuhudia vurugu sehemu mbalimbali. Amani ya dunia hii ni ya mkataba; tumeshuhudia nchi kadhaa zikiwekeana saini za mikataba ya amani, na mara mikataba hii inapovunjika, na amani nayo huvunjika. Amani ya dunia hii mara kadhaa hupatikana baada ya mtutu wa bunduki. Na hii si amani ambayo Kristo anaichia dunia. Kristo dunia amani ambayo imepatikana kwa njia ya Damu yake iliyomwagika pale msalabani. Amani hiyo ni ya kudumu. Ni amani iletayo faraja ya roho na mwili. Ni amani ile ambayo ni tunda la Roho Mtakatifu; amani ambayo iliwafariji wafuasi wa kwanza wakati wa mateso katika kuhubiri Habari njema kama tusomavyo katika somo la kwanza kwamba “Imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi”(Mdo 14:22).

SALA: Ee Kristo Mfufuka uijalie dunia amani ya kweli.