Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 01/05/2024
2024 MEI 1 : JUMATANO-JUMA LA TANO LA PASAKA
Mt. Atanasi, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 1
MTAKATIFU ATANASI WA ALEKSANDRIA
Somo 1. Mdo 15:7-21
Wakati wa mtaguso wa Yerusalemu, baada ya hoja nyingi Petro alisimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu na kuliamini. Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia, akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi; wala hakufanya tofauti kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani. Basi sasa mbona mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua. Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao. Basi mkutano wote wakanyamaza, wakawasikiliza Barnaba na Paulo wakiwapasha habari za ishara na maajabu, ambayo Mungu aliyafanya kwa ujumbe wao katika Mataifa. Na hao walipokwisha kunyamaza Yakobo akajibu, akisema, Ndugu zangu, nisikilizeni. Simeoni ametueleza jinsi Mungu hapo kwanza alivyowaangalia Mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya jina lake. Na maneno ya manabii yapatana na hayo, kama ilivyoandikwa. Baada ya mambo haya nitarejea, nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena maanguko yake, nami nitaisimamisha; ili wanadamu waliosalia wamtafute Bwana, na mataifa yote ambao jina langu limetajwa kwao; asema Bwana, ajulishaye hayo tangu milele. Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika mataifa; bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu. Kwa maana tangu zamani za kale Musa anao watu wahubirio mambo yake; katika kila mji husomwa kila Sabato katika masinagogi.
(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake. |
Wimbo wa Katikati. Zab 96:1-3, 10
“1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake. (K)
2. Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake. (K)
3. Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki;
Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike,
Atawahukumu watu kwa adili. (K) “
Injili. Yn 15:9-11
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.
TAFAKARI
UPENDO NI UKAMILIFU WA FURAHA YOTE: Upendo ni fadhila ya Kimungu inayotuwezesha kumpenda Mungu kuliko vitu vingine vyote na kumpenda jirani kama Kristo alivyotupenda. Katika Injili ya leo Yesu anatufundisha kuwa furaha ya kweli ipo katika kushika amri zake hususani amri ya upendo. Utambulisho wa Mkristo unapaswa kuoneshwa kwa njia ya upendo wa kweli. Kipimo cha upendo wa kweli ni Yesu mwenyewe na siyo mwanadamu. Agano la Kale linatufundisha kumpenda jirani kama nafsi (rej. Wal 19:1). Yesu anakamilisha amri hii kwa kutuonesha kuwa kipimo cha upendo wa kweli ni yeye. Kama alivyompenda Baba, nasi hatuna budi kupendana, vivyo hivyo. Upendo wa kweli unaweza kutenda mambo makubwa. Tushirikishane upendo wa Kristo kwa kuwajali wahitaji na kuwapatia mahitaji yao. Wajane Yatima, Wagane, Wagonjwa, Wafungwa ni makundi yanayotegemea kupata upendo wa pekee kutoka kwetu.
SALA: Ee Yesu naomba uniwashie fadhila ya mapendo. |