Select Page

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 19/03/2024

2024 MACHI 19 JUMANNE: JUMA LA 5 LA KWARESIMA
MT. YOSEFU, MUME WA BIKIRA MARIA
Urujuani
Zaburi: Juma 5

Somo 1. 2 Sam 7:4-5, 12-14, 16

Ikawa usiku huo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema, Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, Siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu, akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.

Wimbo wa Katikati. Zab 89:2-5, 27-29

1. Fadhili za Bwana nitaziimba milele;
Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. (K)

(K) Wazao wake watadumu milele.

2. Nimefanya agano na mteule wangu,
Nimemwapia Daudi, mtumishi wangu.
Wazao wako nitawafanya imara milele,
Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. (K)

3. Yeye ataniita, Wewe baba yangu,
Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
Hata milele nitamwekea fadhili zangu,
Na agano langu litafanyika amini kwake. (K)

Somo 2. Rum 4:13, 16-18, 22

Ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani. kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe, iwe njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila kwa wale wa imani ya Ibrahim; aliye baba yetu sisi sote; (kama ilivyoandikwa nimekuweka kuwa baba wa mataifa Mengi.) Mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako. Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.

Injili. Mt 1:16, 18-21, 24

Yakobo alimzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo.  Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe.

TAFAKARI

FAMILIA NI CHIMBUKO LA KANISA: Leo Mama Kanisa anatualika tumsherehekee Yosefu Mume wa Bikira Maria. Tunaelezwa kuwa katika maisha yake alikuwa mtu wa haki na hakupenda kumdhalilisha mtu yeyote. Alikuwa na mahusiano mazuri na Mungu na hofu ya kwake. Injili imetueleza “alitaka amwache kwa siri.” Katika hili tunajifunza kuwa na utu, kutunza heshima ya mtu hata kama inaonekana katenda kosa. Tuko ambao tunafurahia, kushangilia na kutangaza makosa ya wengine. Kitendo cha Mt. Yosefu kutopenda kuanika hadharani hali ya mwenzi wake (Bikira Maria) ni fundisho kwetu sote. Familia nyingi zimejikuta katika migogoro isiyoisha kutokana na kukosa ustahimilivu wa tabia kama ya Mt. Yosefu. Unakuta wanandoa wanatangazana kwenye mitandao ya kijamii na kuweka wazi madhaifu yao, wanasahau kiapo chao. Kuna mwanasaikolojia anaitwa William Ellery alisema, “uwazi, ukweli na uaminifu hujidhihirisha katika urafiki wa kweli.” Familia nyingi zinakosa hili na hii imepelekea hata Kanisa kuyumba kimaadili na hata maendeleo ya kiroho kwani kitalu halisi cha Kanisa ni familia. Kuyumba kwa familia ni kuyumba kwa Kanisa. 

SALA: Mt. Yosefu mlinzi wa Familia Takatifu, uziombee familia zetu ziishi kwa amani na uelewano.