Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 01/05/2024

2024 MEI 1 : JUMATANO-JUMA LA TANO LA PASAKA

MT. YOSEFU MFANYAKAZI
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 1

SOMO I: Mwa. 1:26-2:3

Mungu alisema, Na tufanye mtu kwa mfano wetu; kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu akasema, tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, uliojuu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita. Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.

 Zab. 90:2- 4, 12-14, 16

1. Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia,
Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu.

2. Wamrudisha mtu mavumbini,
Usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
Maana mika elfu machoni pako
Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
Na kama kesha la usiku. (K)

3. Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.
Ee Bwana urudi, hata lini?
Uwahurumie watumishi wako. (K)

4. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
Utufurahishe kwa kadiri ya siku ulizotutesa,
Kama miaka ile tuliyoona mabaya.
Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako. (K)

(K) Kazi ya mikono yetu uithibitishe, Ee Bwana.

INJILI: Mt. 13:54-58
Yesu alipofika nchi yake, akawafundisha makutano katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, naYusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao.

TAFAKARI

TUACHE KUMTESA YESU: Katika somo la kwanza, tunaona ukuu wa neema ya Mungu. Neema hii ilifanya mambo ambayo nivigumu kuyaelewa kabisa. Kumvua aliyekuwa mtesi wa Kanisa kuwa mlinzi wa Kanisa. Saulo alikuwa akimtesa Kristo kwa kulitesa kanisa. Hii ni kwa sababu Kanisa ni mwili wa kichwa cha Kristo (1Kor 12:27). Mara ngapi na mimi ninalitesa Kanisa? Katika hili, labda kwa baadhi yetu ni zaidi ya Paulo. Ni mara ngapi nimelisema Kanisa vibaya, ni mara ngapi nimelichafua Kanisa kwa matendo yangu maovu kama ulevi, ushirikina na uasherati? Ni mara ngapi nimekataa kulipa zaka. Kweli baadhi yetu ni zaidi ya Paulo. Leo tunapomkumbuka Yosefu mfanyakazi, tuombe moyo wa kujitolea kwa ajili ya kazi ya Bwana. Yeye alisifika kwa kujitolea. Tumfariji Kristo kwa kujitolea zaidi kwa kazi ya Bwana. Tuache kumuumiza kristo. Tuanze upya na Kristo Mfufuka.

Sala: Ee Yesu ninakuomba unihurumie kwa kushiriki katika kukutesa wewe.