Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 29/04/2024

2024 APRILI 29 : JUMATATU-JUMA LA TANO LA PASAKA

Mt. Katarina wa Siena, Bikira, Mwalimu wa Kanisa
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 1

Somo 1. Mdo 14:5-18

Siku zile, palipotokea shambulio la watu wa Mataifa na Wayahudi pamoja na wakubwa wao juu yao, kuwatenda jeuri na kuwapiga kwa mawe, wao wakapata habari wakakimbilia Listra na Derbe, mji wa Likaonia, na nchi zilizo kando kando; wakakaa huko, wakiihubiri Injili. Na huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye hajaenda kabisa. Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa, akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda. Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu. Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji. Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng’ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano. Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele, wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi ni wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; ambaye zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao wenyewe. Lakini hakujiacha pasipo ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema, akiwapeni mvua kutoka mbinguni, na nyakati za mavuno, akiwashibisha mioyo yenu chakula na furaha. Na kwa maneno hayo wakawazuia makutano kwa shida, wasiwatolee dhabihu.

(k) Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi, Bali ulitukuze jina lako. 

Claret Catholic Center: Kwa mahitaji mbalimbali ya vifaa vya Makanisani na  Zawadi za waamini. Tupigie/whatsapp 255 688 404 040

Wimbo wa Katikati. Zab 115:1-4, 15-16

“1. Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi,
Bali ulitukuze jina lako.
Kwa ajili ya fadhili zako,
Kwa ajili ya uaminifu wako.
Kwa nini mataifa kusema,
Yuko wapi Mungu wao? (K)

2. Lakini Mungu wetu yuko mbinguni,
Alitakalo lote amelitenda
Sanamu zao ni fedha na dhahabu,
Kazi ya mikono ya wanadamu. (K)

3. Na mbarikiwe ninyi na Bwana,
Aliyezifanya mbingu nan chi.
Mbingu ni mbingu za Bwana,
Bali nchi amewapa wanadamu. (K)”

Injili. Yn 14:21-26

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. Yuda (siye Iskariote), akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu? Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka. Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.

SALA: Tuombe Mungu atupe moyo wa kujishusha na kuwa wanyenyekevu.

TAFAKARI

SIFA NA UTUKUFU NI KWA MUNGU: Yesu amesema katika Injili “yeye aliye na amri zangu atapendwa na Baba yangu.” Imani yetu lazima ijikite katika kumtukuza Mungu na sio katika kujitukuza sisi wenyewe. Ndio maana hata katika somo la kwanza, baada ya akina Barnaba na Paulo kumponya yule kiwete, alipotaka kuwarudishia shukrani na kuonesha kuwa ni wao waliomponya, tunaona mitume wanakataa na kuoneshsa kuwa ni Mungu. “Akina Bwana mbona mnafanya haya? Sisi nasi ni wanadamu kama nyie.” Hapa ni dhihirisho tosha kuwa Mungu ndiye mtendaji mkuu wa hiyo miujiza na si wao. Ni katika hili Yesu alionesha kuwa tujifungamanishe na yeye na Baba ili wafanye maskani/makao kwetu, tusijitukuze katika utume wetu. Wapo watu ambao wanasubiri kusifiwa na kutukuzwa kwa wanavyofanya utume, wanatamani wawe miungu mtu. Kwa hali hii wanachukua nafasi ya Mungu. Hawako tayari kurarua nguo zao na kujishusha kama walivyofanya mitume.