Select Page

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 18/03/2024

2024 MACHI 18 JUMATATU: JUMA LA 5 LA KWARESIMA
Mt. Sirili wa Yerusalemu, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Urujuani
Zaburi: Juma 5

Somo 1. Dan 13:1-9, 15-17, 19-30, 33-62

Palikuwa na mtu, jina lake Yoakimu, akikaa Babeli, naye ameoa mke jina lake Susana binti Helkia, mwanamke mzuri sana na mcha Mungu. Wazee wake nao walikuwa wenye haki, pia wamemfundisha binti yao sawasawa na Torati ya Musa. Basi Yoakimu alikuwa mwungwana tajiri, na karibu na nyumba yake alikuwa na bustani nzuri; hivyo Wayahudi humwendea, maana alikuwa mwenye heshima kupita wengineo wote. Mwaka ule ule wakaamriwa wawili miongoni mwa wazee wa watu ili kuamua, watu wa namna ile ambao Bwana aliwanena, ya kama ufisadi ulitoka Babeli kwa wazee waamuzi waliohesabiwa kuwa wanatawala watu. Hao walikuwa wakienda mara nyingi kuzuru kwenye nyumba yake Yoakimu; na wote wenye mashtaka yo yote desturi yao wakawajia huko. Basi watu walipoondoka kwenda zao panapo saa sita, Susana huingia katika bustani ya mumewe ili kutembea. Nao wale wazee wawili humwona kila siku anakwenda kutembea; hata wakawaka tamaa kwa sababu yake. Ndipo walipozipotosha nia zao, wakayageuza upande macho yao wasiweze kutazama mbinguni wala kukumbuka hukumu za haki.  Ikawa, walipongoja wakati wa kufaa, yeye aliingia bustanini kama ilivyokuwa desturi yake pamoja na wajakazi wawili, naye alitaka kuoga kwa sababu kulikuwa na joto. Wala hapo hapakuwa na mtu ye yote isipokuwa wale wazee wawili, ambao wamejificha wakimvizia. Basi akawaambia wajakazi wake, Nileteeni mafuta na sabuni, mkaifunge milango ya bustani ili nioge.
 Mara, wale wajakazi walipokwisha kutoka, wale wazee wawili waliondoka wakamwendea mbio, wakasema, Tazama, milango ya bustani imefungwa asiweze kutuona mtu ye yote, nasi tunakupenda sana; haya! Basi, utukubali ulale nasi. La! Hutaki; tutakushuhudia ya kuwa hapa palikuwapo na kijana pamoja nawe, ndio sababu uliwaruhusu wajakazi wako. Basi Susana aliugua, akasema, Nimesongwa pande zote; maana nikilitenda hilo ni mauti yangu; nisipolitenda siwezi kuokoka mikononi mwenu. Ni  afadhali nianguke katika mikono yenu na kukataa, kuliko kutenda dhambi machoni pa Mungu. Mara Susana akapiga kelele kwa sauti kuu; nao wale wazee wawili wakampigia kelele pia. Kisha mmoja wao akakimbia, akaifungua milango ya bustani. Hivyo watumishi wa nyumbani waliposikia kelele bustanini, wao waliingia kwa kasi kwa mlango wa nyuma ili waone ni nini iliyompata. Lakini wale wazee waliisimulia hadithi yao, nao watumishi wakaona aibu kabisa; kwa maana Susana hakuchongelewa habari ya namna hiyo wakati  wo wote.  Ikawa, kesho yake watu walipokusanyika kwa Yoakimu mumewe, wale wazee wawili wakaja nao, wamejaa kusudi lao ovu juu ya Susana la kumfisha; wakasema mbele ya watu, mwiteni Susana binti Helkia, mkewe Yoakimu, aje hapa. Basi akaenda kuitwa; naye akaja pamoja na baba yake na mama yake, na watoto wake pamoja na jamaa zake zote. Kwa hiyo rafiki zake na wote waliomtazama wakasikitika. Ndipo wale wazee wawili waliposimama katikati ya watu wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. Naye akatoka machozi, akatazama juu mbinguni; kwa maana moyo wake alimtumaini Mungu. Wale wazee wakasema, sisi tulipoitembelea bustani peke yetu, huyu aliingia pamoja na wajakazi wawili, wakaifunga milango ya bustani, naye mara akawaruhusu wajakazi. Kisha, kukatokea kijana, ambaye amejificha humo, akamwendea akalala naye. Walakini sisi tungaliko pembeni mwa bustani, tuliuona ubaya huo, tukawaendea mbio. Hata tukiwa tumewaona pamoja, yule kijana hatukuweza kumkamata; maana alikuwa mwenye nguvu kuliko sisi, akaifungua milango akaepuka. Bali huyu tulimkamata, tukauliza yule kijana yu nani, asikubali kutuambia. Hayo, basi, tunashuhudu.
Basi, waliohudhuria wakawasadiki, wakiwa wazee wa watu na waamuzi; hivyo wakahukumu auawe. Mara Susana akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Mungu wa milele, Wewe wajua yaliyositirika, wajua mambo yote yasijekuwako, wewe wajua ya kwamba wananishuhudia uongo, na, tazama, imenipasa kufa; walakini sikufanya kamwe mambo kama hayo, ambayo watu hawa wameyabuni juu yangu kwa ukorofi. Naye Bwana akaisikia sauti yake. Kwa hiyo, alipochukuliwa huyo kwenda kuuawa, Mungu alimchochezea roho kijana mmoja, jina lake Danieli; naye akapaza sauti yake akasema, Mimi simo; mimi sina hatia kwa habari ya damu yake mwanamke huyu. Mara wote wakamgeukia, wakasema, maneno hayo uyasemayo maana yake nini? Akasimama katikati, akasema, Enyi bani Israeli, mmekuwa wapumbavu, hata kumhukumu binti Israeli bila kuhoji wala kupata hakika ya kweli? Rudini hukumuni; mradi hao wanamshuhudia uongo. Basi watu wote walirijea kwa haraka, nao wale wazee wakamwambia, njoo uketi kati yetu, utujulishe habari hiyo, endapo Mungu amekupa wewe heshima ya mzee. Hapo Danieli aliwaambia, watu hawa wawili watengwe, nami nitawahoji. Basi wakiisha kutengwa akamwita mmoja wao akamwambia, Ewe uliyepata kuwa mzee katika uovu, sasa dhambi zako zimekukalia, ulizozitenda zamani kwa kuhukumu isivyo haki, kumpatiliza asiye na hatia na kumwachilia mwovu; lakini Bwana asema, asiye na hatia mwenye haki, usimwue. Haya! Basi, wewe ulimwona kwa macho; useme; Chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, chini ya msandarusi. Danieli akasema, hakika umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana sasa hivi malaika wa Mungu amepokea hukumu ya Mungu, akukate vipande viwili. Akamtenga huyo tena, akaamuru kumleta yule mwingine, akamwambia, Ewe mzao wa Kanani, wala si wa Yuda, uzuri umekudanganya, na tamaa imeupotosha moyo wako. Hivyo ndivyo ulivyowafanyia binti za Israeli, na kwa hofu walitembea nawe; bali huyu binti Yuda hakuweza kustahimili uovu wako. Haya! Basi, nawe useme; chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, chini ya mkwaju. Danieli akamwambia, hakika wewe nawe umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana malaika wa Mungu yu tayari, anakungoja mwenye upanga, akukate vipande viwili; ili awaangamize wote wawili. Mara hiyo makusanyiko yote wakapaza sauti kwa nguvu, wakamhimidi Mungu awaokoaye wamtumainio. Wakawaondokea wale wazee wawili, kwa maana Danieli ameuhakikisha ushuhuda wao wa uongo hata vinywani mwao wenyewe. Wakawatenda kwa torati ya Musa kama vile walivyokusudia kwa ukorofi kumfanyia jirani yao; wakawaua; na mwenye damu isiyo na hatia aliokolewa siku ile.

Wimbo wa Katikati. Zab 23

1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
    Sitapungukiwa na kitu.
    Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
    Kando ya maji ya utulivu huniongoza. (K)


(K) Nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
       Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami. 
 

2. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza
    Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
    Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti
    Sitaogopa mabaya; kwa maana Wewe upo pamoja nami. (K)

3. Waandaa meza mbele yangu,
    Machoni pa watesi wangu.
    Umenipaka mafuta kichwani pangu,
    Na kikombe changu kinafurika. (K)

4.  Kakika wema na fadhili zitanifuata,
     Siku zote za maisha yangu,
     Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)

Injili. Yn 8: 1-11

Walikwenda kila mtu nyumbani kwake; naye Yesu akaenda mpaka mlima wa Mizeituni. Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha. Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati.Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.

TAFAKARI

MUNGU NI MWEMA KWA WAMCHAO: Upo msemo kwamba “mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.” Masomo yote ya leo yanasimulia wanawake wanaoonekana kutotendewa haki, kuonewa, kukandamizwa. Somo la kwanza wahusika wanawakwa na tamaa ya mapenzi na kumshitaki kwa uongo Suzana, baada ya vionjo vyao kutotimizwa. Sio wote walioko magerezani ni watenda maovu, wapo waliopelekwa huko kwa kusingiziwa uongo toka kwa wenye nazo (mali/madaraka). Ni dhana kama hii Yesu anairekebisha katika tuhuma dhidi ya huyu mwanamke wa Injili kuwa “asiye na dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe.” Yesu aliwataka wajichunguze dhamiri zao na ndio maana waliondoka wote baada ya kujitambua kuwa nao sio wakamilifu. Tuelewe hakuna aliyekamilika, sote tunakazana kuelekea ukamilifu. Tusiwe tu watu wa kuongozwa na vionjo na hisia za mwili na kuvuruga mpango mzima wa maisha.

SALA: Ee Mungu tupe ujasiri wa kutetea haki za watu bila woga.