Select Page

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 17/03/2024

2024 MACHI 17: DOMINIKA YA 5 YA KWARESIMA
Urujuani
Zaburi: Juma 1

Somo 1. Yer 31 :31-34

Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.  Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongo mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.

Wimbo wa Katikati. Zab 51: 3-4, 12-15

1. Ee Mungu unirehemu,
Sawasawa  na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema sako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu. (K)

(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi. 

2. Ee Mungu uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)

3. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho wa wepesi.
Nitawafundisha wakosaji njia zako,
Na wenye dhambi watarejea kwako. (K)

Somo 2. Ebr 5: 7-9

Yesu, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii..

Injili. Yn 12 :20-33

Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu. Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu. Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu.  Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu. Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataingamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu. Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemaje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii. Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena. Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika amesema naye. Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu,  bali kwa ajili yenu. Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.  Aliyanena hayo akionyesha ni mauti gani atakayokufa.

TAFAKARI

TUNAKUWA WAFU KATIKA UTU WA KALE NA KUWA HAI KATIKA KRISTO
Dominika ya tano ya Kwaresima inatuingiza katika tafakari ya mateso ya Kristo tukielekea katika kilele cha majira haya ya toba. Hii haimaanishi kwamba sasa kipindi cha toba kimekwisha bali kinatupatia maana ya toba yetu, yaani kutufikisha katika matunda ya fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tendo la toba linatualika kufanya mabadiliko ya maisha ambapo ni kuuvua utu wa kale, utu wa dhambi na kuuvaa utu mpya katika Kristo. Namna hiyo ya kuanza upya inafanyika ndani kabisa mwa nafsi ya kila mmoja wetu kwa kuuvua utu wake wa kale, utu wa dhambi na kuuvaa utu mpya.
Katika somo la kwanza mwanzo huu mpya unaonekana katika namna ambavyo Bwana atafanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. “Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika.” Upya huu unaonekana katika mahali itakapoandikwa sheria: si katika vipande vya mawe au juu ya vibao bali katika mioyo yao. Sheria inaandikwa si nje tena bali ndani ya moyo wa mwanadamu. Upya huu utawafanya wana wa Israeli kutoweza kuivunja Sheria ya Mungu kwani inakuwa ni sehemu ya maisha yao. Zaidi ya hapo hawatakuwa wanafundishwa na jirani kwani kila mmoja ataisikia ikiita ndani mwake. (Fumbo la umwilisho linauunganisha umungu na ubinadamu na kuwezeshwa kuijongea njia ya wokovu)
Tukiiangalia kidogo antholopolija ya kiyahudi tutaelewa zaidi mantiki ya andiko hili la Mungu kupitia kinywa cha nabii Yeremia. Wayahudi walitumia neno «leb» kuwakilisha moyo, neno ambalo lilimaanisha uwezo wa mwanadamu kiakili na kimaamuzi. Sheria inayoandikwa nje ya moyo haigusi moja kwa moja ufahamu na maamuzi ya mwanadamu na hivyo ni rahisi kusahaulika ama kuvunjwa. Hivyo sheria ilipoandikwa katika moyo ilihakikisha kuwa sasa mwanadamu atatambua nini anaelekezwa na pia atakuwa na uwezo wa kufanya uamuzi. Ni yeye mwenyewe anakuwa hakimu wa matendo yake kwani maelekezo yote yapo ndani mwake na utekelezaji wake pia unamtegemea yeye.
Hii ni ishara ya utu mpya tunaouvaa katika Kristo; tunaondolewa utu wa kale ambao ulitufanya kuwa wafu na kuvikwa utu mpya katika Kristo. Wayunani wanaotamani kumwona Kristo wanaelekezwa mara moja katika mwelekeo huo wa maisha. Pengine walishasikia habari zake wakiwa katika nchi yao au wakati walipokuwa wanafika Yerusalemu kuabudu na wakatamani kumwona. Hatuambiwi sababu za  tamanio lao lakini mafundisho anayounganisha Kristo mara yanatueleza mara moja ni nini ambacho tunapaswa kitendeke ndani mwetu kusudi tuweze kumwona; huku ni kufanywa upya katika yeye; ni kuipokea hiyo «leb» yake ili tuweze kumwelewa na kutenda kama yeye. Fumbo la umwilisho linauunganisha umungu na ubinadamu na kuwezeshwa kuijongea njia ya wokovu.
Kristo anatumia mfano wa kufa kwa mbegu ili kuweza kuzaliwa upya: “Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa hutoa mazao mengi.” Katika sayansi ya kilimo tunaelewa kuwa kuchipuka kwa mbegu kunatudai kuiweka ardhini ili kupitia hatua za kibailojia. Hii haijalishi mbegu hiyo ni nzuri au inavutia kiasi gani; uzuri wake unapata maana pale tu inapotoa mazao zaidi na hii ni kwa njia ya kuwekwa ardhini, kufa na kutoa mche ambao utazaa mbegu nyingine. Mkulima akiing’ang’ania na kuifurahia kwa kuiangalia tu ataishia kufa njaa tu kwani hatakuwa na chakula cha kutosha. Utayari wake wa kuiweka ardhini hufanya kuzaliwa kwa maisha mapya na kupata wingi wa mazao..
Huu ni mwaliko wa kuwa tayari kubadili mtindo wa kale wa maisha kusudi kumfikia na kumwona Yesu. Kamwe hatuwezi kumwona Yesu wakati tumeng’ang’aniwa na uzuri, umaridadi, umaarufu wa kidunia. Tunapaswa kuwa tayari kuvifukia ardhini ili tuchipuke tukiwa wapya katika Yeye. Suala la wokovu au kuwa karibu na Kristo si suala la muda mfupi na la kupita tu, bali ni lile linalobadilisha maisha yako yote. Si rahisi kuwa na Kristo wakati upo katika hali ya mchanganyo: upo kanisani lakini bado umefunga hirizi; unatakiana amani na wenzako wakati bado una kinyongo na jirani yako uliyemwacha nyumbani; unaomba utakaso wa dhambi wakati bado miundo mbinu yake umeihifadhi na upo tayari kuirudia baadaye na kadhalika.
Kristo anajiweka kwetu kama kielelezo na anataadharisha wale wanaopenda nafsi zao kiasi cha kushindwa kuzitoa ili kuzaliwa upya. “Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.” Ni kwa njia ya kumfuata Yeye tu na kuuacha utu wetu wa kale ndipo tutaweza kupata huo upya wa maisha: “Mtu akinitumikia na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo.” Tunapotaka kumwona Kristo tunapaswa kumfuata katika njia yake na hivyo tutakuwa naye mahali atakapokuwapo. Hata katika hali ya mateso, au mfadhahiko, au mahangaiko, yote tuyapitie tukichuchumilia kufikia pale Kristo alipo.
Ndivyo anavyotuasa Mtakatifu Paulo kupita katika njia ya mateso. Kristo analiona tendo hilo kama kutimilika kwa saa yake ya kumtukuza Mungu. Utilimilifu huu ni kilele cha utume wake hapa ulimwenguni ambapo atakamatwa na kuteswa na mwisho kuuawa juu msalabani; anaiona kuwa ndiyo saa muafaka kwake Yeye kama chembe ya ngano kufukiwa ardhini, kufa na hatimaye kuzaa matunda ya wokovu. Yeye anakuwa tayari kuipokea saa hiyo na anakiri ndiyo namna ya kumtukuza Mungu.
“Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii. Baba, ulitukuze jina lako.” Ni maneno ya Kristo ambayo yanatufundisha mambo mawili kwanza ni utayari wa kulitukuza jina na Mungu, yaani kuyafanya mapenzi yake kutimia hata katikati ya mateso mengi. Na pili ni nafasi ya Mungu katika kulitimiza hilo. Hapa tunauona uwezo wa Mungu unatenda katika uhuru wa mwanadamu. Ni namna ya juu kabisa ambayo mwanadamu anaudhihirisha uhuru wake kwa utii wa mapenzi ya Mungu. Mungu ndiye chanzo na asili ya yote mema tunayotenda; ameweka ndani mwetu uwezo wa kuyapokea mema yake na pia anatupatia uhuru wa kuyakubali mema hayo.
Kristo alikubali kumtukuza Mungu hadi kifo cha msalabani na kwa namna hiyo Mungu “alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina” (Flp 2:9). Ukristo wetu unatuita katika kumtukuza Mungu kwa namna hii; vinginevyo tunabaki tumedumaa na kutokukua katika utu wetu na utakatifu. Kwaresima yanatupatia fursa ya kuomba neema ya Mungu na kufanya mabadiliko ya kweli na kuzaliwa upya katika Kristo. Ni hakika tunakuwa na hamu ya kumwona Kristo, lakini hamu hiyo ijidhihirishe katika kumfuata mahali alipo kwa kuyasadaka maisha yetu ya kale na kuzaliwa upya katika Yeye na hivyo daima kumtukuza Mungu kwa maisha yetu.

SALA: Ee Bwana utujalie kufa katika Kristo ili tupate kuzaa matunda.