Masomo ya Misa Oktoba 12

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 12/10/2024

2024 OKTOBA 12: JUMAMOSI-JUMA LA 27 LA MWAKA

Mt. Wilfridi wa York, Askofu
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma III

SOMO 1. Gal 3:22-29

Andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo. Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 105: 2-7

1. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.

(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.

2. Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake sikuzote.
Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya,
Miujiza yake na hukumu za kinywa chake. (K)

3. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake,
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
Duniani mwote mna hukumu zake. (K)

INJILI. Lk 11:27-28

Ikawa, Yesu alipokuwa akisema, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, “Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya.” Lakini yeye alisema, “Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika.”

TAFAKARI

KUIVUNJA SHERIA: Sababu moja inayofanya tushindwe katika jaribio la kuhubiri Habari Njema kwa wengine ni kule kusita au kuogopa kupandikiza na kuifanya sheria ikue katika maisha ya wale tunaowahubiria. Tunachofikiri ni kwamba dhamiri zao zinatosha kuwafanya wakiri dhambi zao na kumuhitaji Mungu kama suluhisho lao. Kifupi tunaacha waongozwe na dhamira zao. Kwa hiyo tunaishia kujenga malumbano au hoja na watu ambao matumaini yao ni kwamba wao sio waovu kama walivyo watu wengine. Tunajenga hoja na watu wanaosema kwamba uelewa wao juu ya Mungu unawafanya wafaulu katika maadili. Lakini ikiwa tutawaongoza katika Amri Kumi za Mungu, moja baada ya nyingine, na kuwaambia wayapime maisha yao kulingana na viwango alivyoweka Mungu, tutawafanya waone mwanga mpya katika Injili. Mara nyingi hatutaki uhuru unaopatikana katika Kristo, hadi pale tunapopata uelewa wa kina kuhusu utumwa wetu wa dhambi na hukumu ya Mungu.

SALA: Bwana Yesu utujalie tutambue kwamba sheria yako ni kamilifu.

Masomo ya Misa Oktoba 11

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 11/10/2024

2024 OKTOBA 11: IJUMAA-JUMA LA 27 LA MWAKA

Mt. Yohane wa XXIII, Papa
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma III

SOMO 1. Gal 3:7-14

Fahamuni basi, yakuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa. Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani.  Kwa maana wale walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye. Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 111:1-6

1. Aleluya.
Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
Matendo ya Bwana ni makuu,
Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo.

(K) Alikumbuka agano lake milele.

2. Kazi yake ni heshima na adhama,
Na haki yake yakaa milele.
Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu,
Bwana ni mwenye fadhili na rehema. (K)

3. Amewapa wamchao chakula,
Atalikumbuka agano lake milele.
Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake,
Kwa kuwapa urithi wa mataifa. (K)   

INJILI. Lk 11:15-26

Wengine wa makutano walisema, “Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo.” Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia, “Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli. Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je, huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake. Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutawanya. “Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, ‘Nitarudia nyumba yangu niliyotoka.’ Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.”

TAFAKARI

KUVUKA MSTARI: Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. Katika filamu ‘Hook’ kijana Peter Pan alichora mstari mchangani, kisha akawaambia kila mtu anayeamini na avuke huo mstari. Peter alisahau kwamba wako wanaoweza kuamua asivuke mstari badala yake akasimama katikati ya mstari (hayuko upande wowote). Ikiwa tunamwamini Yesu kuwa Bwana na Mwokozi, tunapaswa kuyapima mambo, kutafuta uwezekano, kufanya maamuzi, kuvuka mstari, na kumtumainia Mungu. Inawezekana tumekuwa na changamoto nyingi katika maisha, inawezekana tumekuwa na maswali ambayo hayajajibiwa bado, hilo lisitukatishe tamaa, sio kwamba hatuna maana au thamani mbele za Mungu, maswali yetu yana maana na ni ya muhimu. Tafuteni nanyi mtaona; Mashaka tuliyonayo kuhusu imani yatamalizika. Bisheni nanyi mtafunguliwa. Mahitaji uliyonayo ni ya muhimu. Ombeni nanyi mtapewa; tudumu katika sala.

SALA: Bwana utujalie kuyapima mambo ya ulimwengu huu ili tujipatie busara.

Masomo ya Misa Oktoba 10

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 10/10/2024

2024 OKTOBA 10: ALHAMISI-JUMA LA 27 LA MWAKA

Mt. Daniel Komboni, Askofu Mmisionari
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Juma III

SOMO 1. Gal 3:1-5

Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa? Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili? Mmepatikana na mateso makubwa namna hii bure? Ikiwa ni bure kweli. Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?

WIMBO WA KATIKATI. Lk 1: 69- 75

1. Ametusimamishia pembe ya wokovu
Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake.
Kama alivyosema tangu mwanzo
Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu;

(K) “Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,
kwa kuwa amewajia watu wake. “

2. Tuokolewe na adui zetu
Na mikononi mwao wote wanaotuchukia;
Ili kuwatendea rehema baba zetu,
Na kulikumbuka agano lake takatifu. (K)

3. Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu
Ya kwamba atatujalia sisi,
Tuokoke mikononi mwa adui zetu,
Na kumwabudu pasipo hofu,
Kwa utakatifu na kwa haki
Mbele zake siku zote. (K)

INJILI. Lk 11:5-13

Yesu aliwaambia wafuasi wake: “Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, ‘Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu, kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake;’ na yule wa ndani amjibu akisema, ‘Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe?’ Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake. Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”

TAFAKARI

TUSALI KWA IMANI: Yesu anatutia moyo kudumu katika sala. Sala inasaidia kuwatofautisha wale wasiosali na wale wanaosali. Kumeibuka wimbi la watu wanaotuma ujumbe katika mtindo wa sala na kuwataka watu wengine watume kwa watu kadhaa au katika makundi kadhaa kisha wataona muujiza. Mara nyingi ujumbe huo huendana na vitisho kwa yoyote atakayepuuzia. Kumbe sala haiwafanyi waamini wawe walegevu katika kufanya kazi waseme tu amina na muujiza utatendeka, sala haipaswi kuwafanya wawe wazubavu, haipaswi kuwafanya kushindwa kuwa na ndoto au malengo, sala haiwafanyi waamini wasiwe na upendo. Badala yake sala inawafanya waamini kuwa na tamaa ya kuwa na maisha, kuwa na siku nzuri, kuwa tayari kukabiliana na changamoto na kuwa na ujasiri wa kuendeleza ndoto zao na kuwashirikisha wengine upendo wa Mungu. Mungu hatuambii tusali kusudi tumlaumu pale tunaposhindwa katika maisha, bali tumtukuze na tumsifu pale maisha yanapofunguka na tunaposhinda.

SALA: Mungu Mwenyezi utujalie tudumu katika sala na kutimiza wajibu wetu katika kazi kusudi neema zako zifuatane nasi katika kila tutendalo.

Masomo ya Misa Oktoba 9

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 09/10/2024

2024 OKTOBA 9: JUMATANO-JUMA LA 27 LA MWAKA

Mt. Dionisi, Askofu na Wenzake, Mashahidi/ Mt. Yohane Leonardi, Padre
Rangi:Kijani

Zaburi: Juma III

SOMO 1. Gal 2:1-2, 7-14

Baada ya miaka kumi na minne, nalipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito pamoja nami. Nami nalikwenda kwa kuwa nalifunuliwa, nikawaeleza injili ile niihubiriyo katika Mataifa, lakini kwa faragha kwa hao walio wenye sifa, isiwe labda napiga mbio bure, au nalipiga mbio bure. Bali, kinyume cha nayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa. Maana yeye aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi kwenda kwa mataifa. Tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohane, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara; ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya. Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu. Kwa maana kabla hawajaja watu kadha wa kadha waliotoka kwa Yakobo, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa; lakini walipokuja wao, akarudi nyuma akajitenga, huku akiwaogopa waliotahiriwa. Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao. Walakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawasawa na ile kweli ya Injili, nalimwambia Kefa mbele ya wote, “Ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha mataifa kufuata desturi za Wayahudi?

WIMBO WA KATIKATI. Zab 117

1. Aleluya.
Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
Enyi watu wote, mhimidini.

(K) “Enendeni ulimwenguni wote,
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. “

2. Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
Na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)

INJILI. Lk 11:1-4

Yesu alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, “Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake.” Akawaambia, “Msalipo, semeni: Baba, Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, Utupe siku kwa siku riziki yetu. Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni.”

TAFAKARI.

JIFUNZE KUSALI NA KUSAMEHE: Inaonekana maisha ya sala ni rahisi sana. Unatafuta mahali pa ukimya, kisha unazungumza na Mungu. Lakini hata wafuasi wa Yesu waliomba kufundishwa kusali, hili likionesha kwamba, hawakuwa na ufahamu wa kutosha katika sala na kwa sababu hiyo walihitaji elimu hiyo. Mara ya mwisho ni lini ulijifunza kusali? Makundi mbali mbali wanalisaidia Kanisa na kuwaongoza watu kujua nini maana ya sala. Nawe fanya hivyo; elekeza, wasiliana na watu na anzisha vikundi vidogo vidogo vya sala ukianzia katika familia. Kuhusu msamaha; kuwasamehe wale waliotukosea ni jambo gumu sana. Frank amenisaliti, John ameniibia, na Richard amenidanganya. Kuwasamehe watu hawa ni ngumu sana. Lakini hata hivyo Kristo anatualika kuwasamehe. Hivi ndivyo unavyoweza kuanza kuwa mtu wa msamaha: Fikiria jinsi ulivyozishika amri za Mungu kwa kiwango cha chini kabisa. Kusudi Mungu aweze kukusamehe, unahitajika upendo mkubwa sana. Kumbuka watu wanaoweka kisasi jinsi walivyo. Sala zetu zituongeze katika kusameheana. 

SALA: Bwana utujalie moyo wa sala na majuto pale tunapokosea nasi tukumbuke kuwasamehe waliotukosea.

Masomo ya Misa Oktoba 8

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 08/10/2024

2024 OKTOBA 8: JUMANNE-JUMA LA 27 LA MWAKA

Mt. Reparata
Rangi:Kijani

Zaburi: Juma III

SOMO 1. Gal 1:13-24

Mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu; wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski. Kisha, baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano. Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana. Na hayo ninayowaandikia, angalieni, mbele za Mungu, sisemi uongo. Baadaye nalikwenda pande za Shamu na Kilikia. Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 139:1-3, 13-15

1. Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.

(K) Uniongoze, Ee Bwana, katika njia ya milele.

2. Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.
Matendo yako ni ya ajabu. (K)

3. Na nafsi yangu yajua sana,
Mifupa yangu haikusitirika kwako,
Nilipoumbwa kwa siri,
Nilipoungwa kwa ustadi pande za nchi. (K)

INJILI. Lk 10:38-42

Yesu aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, “Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie.” Bwana akajibu akamwambia, “Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.”

TAFAKARI. 

WAFANYAKAZI TUWE MAKINI: Wale tunaofanya kazi kwa bidii tunapaswa kuwa makini. Yapo matatizo makubwa matatu yanaweza kututokea: Mosi; unapoomba msaada (msaada halali) usilenge katika kuonesha mafanikio yako mwenyewe au kujigamba (Unakwenda kuomba msaada huku unajisifia). “Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Pili; Unapomwita Yesu “Bwana” huku unahoji maamuzi na mamlaka yake au kumuonesha kwamba haongozi timu yake sawa sawa, unamuonesha Yesu kwamba wewe ni bora zaidi kuliko Yeye. Tatu; Unapokubali uhusiano wako na mtu mwingine, kama Martha alivyofanya kwa dada yake, kisha unampinga kwa kushindwa kufuata maongozi yako, unayafanya matakwa yako kuwa sahihi na bora zaidi kuliko yake hii ni kwa sababu pengine zina matokeo mazuri. Lakini njia iliyo bora ni hii; Usijitafutie au kujitangazia ukuu wako mwenyewe. Wasaidie wengine katika wajibu wao muhimu. Muombe Yesu kwanza kisha nenda kafanye kazi yako halali.

SALA: Bwana utusaidie tuwe wanyenyekevu tusijitafutie ukuu wala kuwadharau wengine ikiwa sisi tunafanya vyema zaidi.