Select Page

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 03/03/2024


2024 MACHI 3 JUMAPILI: DOMINIKA YA 3 YA KWARESIMA
Urujuani
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Kut 20 :1-17

Mungu alinena maneno haya yote akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa Usiwe na miungu ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure jina la Bwana, Mungu wako, maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure. Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana Mungu, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba, kwa hiyo Bwana akaibariki siku ya Sabato akaitakasa. Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako. Usiue. Usizini. Usiibe. Usimshuhudie jirani yako uongo. Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng’ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako. 

Wimbo wa Katikati. Zab 19: 8-11

1. Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima. (K)

(K) Wewe, Bwana, ndiwe mtakatifu wa Mungu. 
   
2. Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia macho nuru.  (K)

3. Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli
Zina haki kabisa (K)

4. Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
Kuliko wingi wa dhahabu safi.
Nazo ni tamu kuliko asali,
Kuliko sega la asali. (K)

Somo 2. 1 Kor 1 :22-25

Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu. Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu.

Injili. Yn 2 :13-25

Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara. Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila. Basi Wayahudi wakajibu wakamwambia, Ni ishara gani utuoneshayo, kwamba unafanya haya?  Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake. Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema  hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu.  Hata alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizofanya. Lakini Yesu hakujiaminisha kwao; kwa kuwa yeye aliwajua wote; na kwa sababu hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu; kwa maana yeye mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwandamu.

TAFAKARI

LIVUNJENI HEKALU HILI NAMI NITALIJENGA KWA SIKU TATU
Amri, maagizo, miongozo na kanuni hupatikana katika jamii ya mwanadamu kwa ajili ya kuleta uwiano wa kimaisha. Wanapoishi watu wawili au zaidi kuna umuhimu wa kuweka miongozo ambayo itawezesha amani, haki na uelewano kati ya watu. Katika jamii yoyote ya kidini, kisiasa au kiuchumi mwanadamu huandaa kanuni mbalimbali kwa makusudi tajwa hapo juu kusudi kuepuka migongano kati ya wahusika wa jamii fulani. Mwenyezi Mungu ambaye ni muumba wetu ametuwekea pia amri zake ili tuweze kuishi kwa kadiri ya maongozi yake na kuyatimiza mapenzi yake. Kitabu cha kutoka kimetuorodheshea amri hizi za Mungu ambazo kwa haki zinaratibu uhusiano wetu na Mungu na uhusiano wetu na binadamu wenzetu. Mwanadamu anapokiuka amri za Mungu anatenda dhambi na hivyo anaalikwa kufanya toba na kumrudia Mungu.
Majira ya Kwaresima yanatualika katika toba. Ni wazi mwaliko huu unatutaka kurejea katika Amri za Mungu. Lakini lipo jambo la msingi ambalo kwalo amri, sheria, kanuni au mwongozo wowote ule unapaswa kulenga. Jambo hilo ni kukua na kukomaa. Hivyo safari hii ya toba isitumike tu kama fursa ya kuorodhesha makosa yako na kuomba msamaha bali ni majira ya kukua na kuimarika kiroho. Amri za Mungu zinapaswa kutukuza na kutuimarisha kiroho. Huku ndiko kukua kwa upendo wetu kwa Mungu na kwa jirani zetu (rej. Mt 22:37 – 40). Tendo hili la kukua katika upendo linaonekana katika utayari wa kujifunua na kutimiza mapenzi ya Mungu na kwa upande mwingine kuiona nafsi ya jirani yako na kuifanya kuwa kama yako. Hivyo amri za Mungu zinapaswa kutuelekeza katika kuimarika kwa fadhila za upendo, imani na matumaini.
Ni changamoto ambayo inawekwa mbele yetu wakati wa majira haya ya Kwaresima. Tunapaswa kujiuliza namna ambavyo tumefanikiwa kuistawisha taswira ya Mungu na ya jirani yangu ndani ya nafsi yangu. Ipo hatari ya kuzitimiza amri za Mungu kwa kutaka kuonekana na hivyo kubaki kudumaa kiroho. Hii ni ile hali ya mmoja anapojitahidi kutimiza amri ili kuepa adhabu. Namna hii kamwe haimsaidii mtu. Namna hii inatupelekea hata mara nyingine kushindwa kuufunua upendo wa Mungu ambao ni lengo msingi la amri za Mungu na kusisitizwa zitekelezwe tu hata bila kutumia hekima. Mazingira haya ya kutekeleza amri au kanuni kwa ajili ya kuonekana yamekemewa tangu mwanzoni mwa Kwaresima. Mmoja yupo radhi mithili ya Kuhani na Mlawi katika simulizi la Msamaria Mwema (rej. Lk 10:31 – 32) kumwacha jirani yake anaangamia kwa kigezo cha kwenda kutimiza amri ya Mungu.
Nabii Isaya alituonya juu ya mfungo wa kufuatilia tu maelekezo ya kisheria bila kukua kwa upendo kati yako na jirani zako: “Je, saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii … siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta masikini waliotupwa nje nyumbani kwako, umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo? (Isa 58:7). Ni tendo ambalo linapaswa kumfanya Kristo aendelee kukua ndani mwetu nasi kupungua. Tunapomfanya Yeye kukua ndani mwetu tunampatia nafasi ya kuadhimishwa ndani mwetu na hivyo yote anayoyatimiza kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu, yaani yale yanayofupishwa katika Injili ya Luka 4:18 – 19 yanaadhimishwa katika maisha yako. Amri na Torati yote kama tulivyotafakari Dominika iliyopita inajumuishwa katika nafsi ya Kristo, hivyo tunapomwadhimisha Kristo kwa uaminifu na kuueneza upendo wake tunapewa fursa ya kuzitimiza Amri za Mungu.
Kristo katika Injili anawaumbua Wayahudi ambao walijikinai kuzishika amri za Mungu lakini si katika namna inayofaa. Viongozi wa dini na watu wengine wenye uwezo walitumia nafasi zao katika hekalu na kuligeuza kuwa si mahali pa kuufunua upendo wa Mungu bali kuendelea kuwanyonya na kuwakandamiza wengine. Aliwaambia: “msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara”. Ni wazi biashara hizo zilifanywa si kwa kuwasaidia waliotoka mbali kupata urahisi wa kutoa dhabihu zao bali waliwaibia kwa kuwazidishia gharama; wale waliobadilisha fedha waliweka faida ya juu ili kupata zaidi na hawa wote walilindwa na viongozi wa hekalu ambao pengine walifaidika kwa namna fulani. Tendo hili la kutoa sadaka ambalo lilikubalika kisheria liligeuka kuwa ni fursa ya unyonyaji na kupora upendo wa ndugu kwa ndugu.
Kristo anawaambia: “Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha.” Ni tangazo la mapinduzi yaliyoletwa na Kristo. Hekalu lipaswalo kubomolewa ni mioyo ya wanadamu iliyojaa dhuluma na unyonyaji wa hadhi wa mwanadamu mwenzeke. Yeye ambaye anatumia nafasi yake na hata wakati mwingine kujikinai kwa njia za kihalali kuwepo katika nafasi hiyo lakini si katika kuonesha upendo bali kumwangamiza mwanadamu. Huyo kisheria ataonekana ametimiza wajibu wake lakini sheria hiyo haijamkuza katika upendo kwa Mungu na kwa jirani yake. Mapinduzi yaletwayo na Kristo ni mwaliko wa kubadili mwenendo wetu. Ni wito wa kuitafakari jamii yetu ambayo inaendelea kumgandamiza na kumgaragaza mwanadamu kwa jina la sheria na taratibu ambazo kwa ujumla wake zinakinzana na ukweli wa amri za Mungu. Hakutapaswi kubaki katika ishara au ushahidi wa kidunia kama wayahudi au hekima za kidunia kama wayunani bali ni kumtanguliza “Kristo nguvu ya Mungu.”
Kukua na kuimarika kiroho kunawezeshwa pia na tafakari ya dhati ya mazingira ambayo hupelekea mmoja kuanguka dhambini. Hizi ni nafasi za vishawishi. Tunapaswa kujikumbusha kuwa sisi tu mithili ya mshumaa ambao ukipita au kupitishwa karibu na moto lazima utayeyuka. Hivyo tunaalikwa kujitafakari na kujiuliza: Ni nini ambacho huyeyusha uwepo wa Mungu ndani mwangu? Ni nini ambacho roho yangu hushindwa kuhimili joto lake na hivyo kuvunja amri na maagizo ya Mungu? Kila mmoja anao uwezo wa kutambua mazingira yanayomwangusha dhambini. Kama ni udhaifu wako katika kutawala kilevi basi unapaswa kukimbia mazingira hayo; kama ni udhaifu wako wa kushindwa kutawala tamaa za mwili kwa kuona ama filamu au picha za utupu au kuwaona watu wa jinsia tofauti na wewe katika mzingira fulani unapaswa kuyakimbia mazingira hayo; kama ni udhaifu wako katika kushindwa kuwa mwaminifu katika mali zako binafsi na za jumuiya tafuta mbinu muafaka n.k. Tembea vema ili kuzishika vema amri za Mungu na hatimaye mwisho wa majira haya uwe umekuwa kiroho na kimwili.

SALA: Ee Mungu utujalie neema ya kushika amri zako kiaminifu. Amina.