Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 27/03/2024

2024 MACHI 27 JUMATANO: JUMA KUU
Mt. Ruperto, Askofu
Rangi: Urujuani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Isa 50:4-9

Bwana Mungu amenipa ulinzi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemea kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya. Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi. Tazama, Bwana Mungu atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa?

Wimbo wa Katikati. Zab 69:8-10, 21-22, 31, 33-34

1. Kwa ajili yako nimestahimili laumu
Fedheha imenifunika uso wangu.
Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
Maana wivu wa nyumba yako umenila,
Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata. (K)

(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, ee Bwana.

2. Laumu imenivunja moyo,
Nami ninaugua sana.
Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna;
Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu..
Wakanipa uchungu kuwa chakula changu;
Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki. (K)

3. Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
Nami nitamtukuza kwa shukrani.
Walioonewa watakapoona watafurahi;
Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
Wala hawadharau wafunga wale. (K)”

“Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. ”  

Mt. 26:24

Injili. Mt 26:14-25

Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti. Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka? Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.

TAFAKARI

RUSHWA HUFIFISHA UTU: Tupo katika Juma Kuu ambapo tunaelekea kwenye mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kristo katika utume wake yapo mengi aliyowaeleza wale mitume wake kwa lengo la kuwaachia utume huo kuendelezwa. Kwa Kristo kukamatwa, kuteswa, kifo na ufufuko kulichangiwa na mtu wake wa karibu, vijana wa leo watasema, ‘Yuda alimzunguka Yesu’ kuna usemi usemao, “kikulacho ki nguni mwako.” Kuna mwanamuziki aitwae Mr Nice aliimba wimbo hivi, “Kikulacho kumbe ki nguoni mwako, rafiki ndiye adui yako, ninakula nae ninacheka nae kumbe mwenzangu anaona gere.” Yuda alikuwa rafiki wa karibu sana na Yesu, alikubali kupokea rushwa ili amsaliti Yesu kwa Makuhani. Hapa tunajifunza kusipende kudanganyika kwa vitu au mali ya aina yoyote kwa gharama ya maisha yetu au ya wenzetu. Tamaa ya mali imeangamiza wengi.

SALA: Ee Bwana utuepushe na taama ya mali.