Select Page

Masomo ya Misa Feb 20

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 20/02/2024

2024 FEBRUARI 20 JUMANNE: JUMA LA 1 LA KWARESIMA
Mwenyeheri Yasinta
Urujuani
Zaburi: Juma 1

Somo 1. Isa 55: 10-11

Bwana asema: Kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.

Wimbo wa Katikati. Zab 34:4-6, 16-19

1. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote. (K)

(K) Wenye haki, Bwana anawaponya
        na taabu zao zote.


2. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote. (K)

3. Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,
Na masikio yake hukielekea kilio chao.
Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoa kumbukumbu lao duniani. (K)

4. Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote.
Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa. (K)

Injili. Mt 6: 7-15

Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnavyohitaji kabla ninyi hamjamwomba. Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

TAFAKARI

TUTULIE KATIKA SALA NA BWANA ATATUTIMIZIA HAJA ZETU: Katika maisha yetu, tuna mahitaji mbalimbali ambayo tunahitaji kutoka kwa Mungu. Ni kwa njia ya sala iliyo bora na yenye utulivu, Mungu anatutimizia mahitaji yetu. Injili Takatifu inatupa mfano wa utulivu katika kusali kwa njia ya maonyo kwa wafuasi wa Yesu, kwamba wasiwe kama watu wa mataifa. Wanaambiwa wasipayuke payuke, yaani namna hii inawataka wawe na utulivu. Pia Yesu aliwapa mfano wa namna ya kusali, ndio sala ya Baba yetu. Utulivu huu katika sala hupelekea kujibiwa shida zetu kwani maombi yetu humfikia Mungu na wala hayarudi. Namna hii inashuhudiwa na nabii Isaya ya kuwa Neno la Mungu litatimia wala halitarudi na litatimiliza haja zetu. Wapendwa, katika sala tuliyoishuhudia ina namna mbalimbali za kuzungumza na Mungu kwa utulivu, inamsifu na kumtukuza Mungu, inatoa shukrani kwa Mungu, inaeleza maombi ya mahitaji, na kudhihirisha namna ya kusameheana. Nasi tujifunze katika hayo ili pindi tusalipo tusali kwa utulivu hali tukiweka wazi malengo yetu ya sala.

SALA: Ee Bwana Yesu, tunakuomba utufundishe kusali jinsi vile itupasavyo. Amina. 

Masomo ya Mia Feb 19

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa 19/02/2024

2024 FEBRUARI 19 JUMATATU YA YA KWARESIMA
Mt. Konradi
Urujuani
Zaburi: Juma 1

Somo 1. Law 19:1-2, 11-18

Bwana akanena na Musa, akamwambia, ”Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu. Msiibe, wala msidanganye, wala msiambiane uongo. Msiape uongo kwa jina langu, hata ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi Bwana. Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang’anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi. Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi Bwana. Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. Usiende huko na huko katikati ya watu wako, kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha damu ya jirani yako; Mimi ndimi Bwana. Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi Bwana.    

Wimbo wa Katikati. Zab 19:8-10, 15

1. Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima. (K)

(K) Bwana unayo maneno ya uzima wa milele.

2. Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia macho nuru. (K)

3. Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa. (K)

4. Maneno ya kinywa change,
Na mawazo ya moyo wangu,
Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana,
Mwamba wangu, na mwokozi wangu. (K)

Injili. Mt 25:31-46

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme, mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika; nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi. Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama. Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie? Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.

TAFAKARI

MIENENDO YETU NDIYO HAKIMU WETU WA HAKI: Wapendwa, kipindi hiki cha Kwaresma ni kipindi cha kufanya toba ya kweli ili tumrudie Mungu na kustahilishwa kuurithi Ufalme wa Mungu. Kwa njia ya hukumu tunapata mastahili hayo. Katika kitabu cha Walawi, mastahili yetu ya hukumu ya haki ni kadiri ya kufuata na kuishi Amri ya Mapendo yaani kumpenda Mungu na kuwapenda jirani zetu kama nafsi zetu. Kumpenda Mungu ni kufuata na kuziishi Amri zake na kumpenda jirani ni kutomtendea mambo yaliyo kinyume na utu ambayo hata sisi wenyewe hatupendi kutendewa. Mienendo yetu juu ya kuziishi Amri hizo au kutoziishi ndiko kunaleta wazo la hukumu ya haki linalowasilishwa na Injili, ambapo tunaelezwa kuwa Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wake na kuhukumu ulimwengu. Atahukumu kadiri ya matendo ya kila mmoja, aliyetenda vema atastahilishwa kuupata uzima wa milele na aliyetenda dhambi atakwenda katika adhabu ya milele. 

SALA: Ee Mwenyezi Mungu, utujalie kutenda mema bila ya ubaguzi wowote.

Masomo ya Misa Feb 18

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa takatifu 18/02/2024

2024 FEBRUARI 18. DOMINIKA YA 1 YA KWARESIMA 
Urujuani
Zaburi: Juma 1

Somo 1. Mwa 9:8-15

Mungu akamwambia Nuhu, na wanawe pamoja naye, akisema, Mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi, tena na uzao wenu baada yenu; tena na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi; ndege, na mnyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi. Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo, kuiharibu nchi. Mungu  akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele; Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi. Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni, nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili.

Wimbo wa Katikati.  Zab 25:4-9

1. Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha
Maana wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu.  (K)

(K) Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli,
       Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.  

 
2. Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako,
Maana zimekuwako tokea zamani.
Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako,
Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako. (K)

3. Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake.  (K)

Somo 2. 1 Pet 3:18-22

Kristo aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri; watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji. Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo. Naye yupo mkono wa kuume wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake.

Injili. Mk 1:12-15

Roho alimtoa Yesu aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia.  Hata baada ya Yohane kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.

TAFAKARI
Ni Dominika ya kwanza ya Kwaresima. Maneno mawili makuu yanasikika: Dhambi na Toba. Somo la kwanza (Mwa 9:8-15) linasimulia kisa cha Nuhu na familia yake. Kiini cha simulizi hii ni kuenea kwa uovu ulimwenguni. Tukisoma kitabu cha Mwanzo kuanzia sura ya 6 hadi sura ya 11 tunaelezwa jinsi mwanadamu alivyozidi kutenda uovu na kumwasi Mungu na kukataa ufunuo wake (Mwa 6:5-6; taz. Rum 1:20-25). Mwanadamu alizama katika dhambi na hasa ile ya uasherati. Kutokana na uovu huo Mungu akaamua kuiangamiza dunia na kila kiumbe ambacho kilikuwa juu ya uso wa nchi ili kuitengeneza dunia mpya.
Hata hivyo kulikuwa na familia moja tu iliyomcha Mungu, familia ya Nuhu. Nuhu na familia yake walibaki kuwa waaminifu kwa Mungu. Aliishi na Mungu bila kuachana naye (Mwa 6:8-11). Mungu alitumia gharika (Mwa 6:5-7,17) kuiangamiza dunia na watu wake wote isipokuwa Nuhu na familia yake, ambapo Mungu alimwamuru atengeneze safina (mfano wa meli kubwa) ya kumuhifadhi yeye na familia yake pamoja na wanyama wawili wawili wa kila aina. Kwa siku 40 usiku na mchana ikanyesha mvua kubwa iliyoambatana na aina fulani ya matetemeko ya nchi (Mwa. 7:11-12). Tukio hili lilikuwa ni zaidi ya tsunami. Hata baada ya mvua kuacha, ilichukua muda mrefu hadi maji kupungua. Na miezi minne baada ya hayo safina ikatulia juu ya mlima Ararati (Mwa 8:3-4). Lakini ni miezi saba baadaye Nuhu, watu wake na wanyama waliweza kutokana safinani na kuanza maisha mapya duniani (Mwa. 8:14-19). Na baada ya hayo, ndipo Mungu anaweka agano na Nuhu. Mungu anaahidi kwamba hataiharibu tena nchi. Na kama ishara ya agano hilo akauweka upinde winguni. (Mwa. 9:8-15).
Wakati Mungu anaahidi kutoiangamiza dunia, swali linakuja, Je, uovu umetoweka duniani? Je, mwanadamu ameacha uasi dhidi ya Mungu? Je, hukuna tena dhambi duniani? Majibu ya maswali haya tunayapata katika Injili ya leo Mk.1:12-15). Yesu anashinda majaribu ya Shetani. Anaenda Galilaya. Na anaanza kuhubiri. Na ujumbe wake mkuu ni: “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni na kuiamini Injili”(Mk. 1:15). Kwanini tunaalikwa kutubu? Ni kwa sababu tu wadhambi.
Dhambi ni uasi dhidi ya Mungu. Uasi huu humtenga mtu na Mungu. Na njia ya ya kuunganika tena na Mungu ni kutubu; kufanya toba. Toba ni hali ya kubadilika ndani ya moyo. Ni ile metanoia. Kutubu ni kuitikia mwaliko wa kuacha dhambi na kumrudia Mungu. Ni kuomba rehema na huruma ya Mungu. Hali hiyo ya mabadiliko ya ndani huchagizwa na matendo ya nje: Sala pamoja na kufunga kunakoendana na kurarua mavazi, kuvaa magunia (1Fal 20:31; 2Fal 6:30; Isa. 22:12); na kujipaka majivu (Isa 58:5). Mababa wa Mtaguso wa II wa Vatikano wanafundisha kwamba “Toba ya wakati wa Kwaresima isiwe ni tendo la ndani na la binafsi tu, bali pia lionekanalo kwa nje na katika maisha ya jamii”(Hati za Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, Liturujia, 110).
Mwenyezi Mungu anatupatia sisi pia nafasi ya kumrudia. Anatupatia safina, Kanisa kama chombo chetu cha kutupatia wokovu. Ili kutupa wokovu, Mama Kanisa ametupatia Sakramenti ili “Kututakatifuza wanadamu…kutupatia neema…pia kuwezesha kumheshimu Mungu jinsi ipasavyo na kufanya matendo ya huruma”(Hati za Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, Liturujia, 59). Lakini kwa namna ya pekee Mama Kanisa ametuwekea Sakramenti ya Kitubio ambayo “Wanayoijongea hupokea humo kutoka huruma ya Mungu ondoleo la makosa yaliyotendwa dhidi yake, na papo hapo hupatanishwa na Kanisa, ambalo dhambi yao imelijeruhi…”(Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, Fumbo la Kanisa, 11). Sakramenti ya Kitubio ni njia ya kujipatanisha na Mungu. Kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio wakosefu hupatanishwa si na Mungu tu, bali pia na Kanisa.
Mimi na wewe tunaalikwa kufanya toba. Na wakati ndio huu. Tumepewa siku 40 za kujitakasa na kuacha njia zetu mbaya. Tuongozane na Yesu ambaye “aliteswa Mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili ya wasio na haki”(1Pet 3:18); kwenda naye jangwani ili kwa njia ya sala na mfungo tuweze nasi kupata nguvu ya kumshinda Shetani/Ibilisi na hila zake zote. Kwaresima iwe kwetu kipindi cha kukua kiroho; kipindi cha mazoezi ya nidhamu ya kiroho. Tukiwa mwanzoni Kabisa mwa Kwaresima, tumwombe Mungu tukisema “Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako, uniongoze katika kweli yako. Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu”(Zab 25:4-5).

SALA: Ee Bwana utujalie moyo wa toba ya kweli ili tuiishi vyema Kwaresima.

Masomo ya Misa Feb 17

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa takatifu 17/02/2024

2024 FEBRUARI 17 JUMAMOSI BAADA YA MAJIVU
Wat. Waanzilishi saba wa shirika la Watumishi wa Bikira Maria
Urujuani
Zaburi: Juma 4

Somo 1. Isa 58: 9b-14

Bwana asema hivi: kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui. Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia. Kama ukigeuza mguu wako usiihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe; wala kuyatafuta ya kupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe; ndipo utakapojifurahisha katika Bwana; nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha Bwana kimenena hayo.

Wimbo wa Katikati. Zab 86:1-2, 3-4,5-6

1. Ee Bwana, utege sikio lako unijibu,
Maana mimi ni maskini na mhitaji,
Unihifadhi nafsi yangu,
Maana mimi ni mcha Mungu.
Wewe uliye Mungu wangu,
Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini. (K)

(K) Ee Bwana, unifundishe njia yako;
       Nitakwenda katika kweli yako. 


2. Wewe, Bwana unifadhili,
Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako,
Maana nafsi yangu yakuinulia Wewe Bwana. (K)

3. Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema,
Umekuwa tayari kusamehe,
Na mwingi wa fadhili,
Kwa watu wote wakuitao.
Ee Bwana, uyasikie maombi yangu;
Uisikilize sauti ya dua zangu. (K)

Injili. Lk 5: 27-32

Siku ile: Yesu aliona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaacha vyote, akaondoka, akamfuata. Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake; palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao. Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung’unikia wanafunzi wake, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?” Yesu akajibu akawaambia, “Wenye afya hawana haja ya tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”

TAFAKARI

BWANA NAACHA YOTE YA ULIMWENGU HUU NAKUFUATA WEWE: Kuacha mambo ya ulimwengu si kwa kutotumia mali na mambo ya ulimwengu, bali kuyatumia kadiri ya mpango wa Mungu. Katika kipindi hiki tunaalikwa kujikatalia, kuachilia yale yasiyofaa na kumwendea Bwana. Tumeshuhudiwa na ujumbe wa Bwana kupitia Nabii Isaya kwa taifa la Yuda, kwamba wakiacha maelekeo yao maovu, wakijali wahitaji, wakiishika siku ya Bwana, ndipo wataongozwa na Bwana, nuru yao itapambazuka gizani. Tena watarithishwa urithi wa Yakobo baba yao. Katika Injili, Mtoza ushuru Lawi, baada ya kuitwa na Yesu, aliacha yote na kumfuata, jambo lililowafanya Mafarisayo na waandishi wanung’unike na kuuliza swali. Jibu la Yesu linadhihirisha shauku ya Yesu kwa wanadamu juu ya kutubu dhambi. Wapendwa, maishani ili kutimiza wajibu wetu mbele za Mungu na wenzetu, ni lazima tujitoe sadaka, tuachilie mambo ya ulimwengu huu, ambako ni pamoja na kuacha maelekeo mabaya hasa kwa kutubu. 

SALA: Bwana, tunakuomba utujalie ujasiri wa kutojishikamanisha na mali kiasi cha kutosikia mwaliko wa kukufuata Wewe.

Masomo ya Misa Feb 16

Itukuzwe Damu ya Yesu… Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 16/02/2024

2024 FEBRUARI 16 IJUMAA: IJUMAA BAADA YA MAJIVU
Mt. Romano, Abati/ Mt. Lupisini Mtawa
Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1:  Isa. 58: 1-9

Bwana Mungu asema hivi: piga kelele, usiache, paza sauti yako kama tarumbeta; uwahubiri watu wangu kosa lao, na nyumba ya Yakobo dhambi zao. Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu. Husema, “mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii?” Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, nakupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je! kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Si siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana. Je! saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Sio kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, “Mimi hapa.”

Wimbo wa Katikati. Zab 51:3-6a, 18-19

1. Maana nimejua mimi makosa yangu,
Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako,
Na kufanya maovu mbele za macho yako. (K)

(K) Moyo uliovunjika na kupondeka,
      Ee Mungu, hutadharau.    


2. Tazama mimi naliumbwa katika hali ya uovu;
Mama yangu alinichukua mimba hatiani.
Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni
Nawe wanijulisha hekima kwa siri. (K)

3. Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako,
Uzijenge kuta za Yerusalemu .
Ndipo utakapopendezwa na dhabihu ya haki;
Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. (K) 

Injili. Mt 9: 14-15

Siku ile: Yesu alipofika ng’ambo, katika nchi ya Wagerasi, wanafunzi wake Yohane wakamwendea, wakasema, “Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi?” Yesu akawaambia, “Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga.”

TAFAKARI

NIFUNGE NAMNA GANI? Katika kipindi hiki tunachoalikwa na Mama Kanisa kutafakari juu ya matendo yetu na kufanya toba, tunaalikwa pia kufunga kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Tujiulize, tunapaswa kufaunga vipi? Nabii Isaya anatukumbusha juu ya namna ya kufunga kupitia ujumbe wa Bwana ambao unamtaka awakumbushe watu wake na nyumba ya Yakobo juu ya dhambi zao. Wao wanafunga ili kujionesha, kutafuta anasa, kufunga kwao ni katika maovu. Wanaelezwa namna bora ya kufunga impendezayo Bwana, yaani kufunga vifungo vya uovu, kujali watu na kutenda haki. Kuwasaidia wenye mahitaji kama vile, chakula, nguo n.k. Walielezwa kuwa namna hii ndiyo itakayowastahilisha mbele ya Bwana. Kwa Wayahudi kufunga kulifanywa siku ya upatanisho ambapo watu walipaswa wajitese kwa kuachilia vionjo vya kimwili kama vile kula, kunywa, n.k. Mafungo yanalenga kupata furaha ya ukombozi na utimilifu wake upo kwa Yesu. Tujifunze kuacha dhambi, kujikatalia, kuwasaidia wasiojiweza na kusali zaidi. 

SALA: Ee Bwana tunaomba utujalie moyo wa majitoleo na kujali wahitaji kwani katika wao tunakuona wewe, amina. 

Masomo ya Misa Feb 15

Itukuzwe Damu ya Yesu… Karibu Katika Masomo ya Misa 15/02/2024

2024 FEBRUARI 15 ALHAMISI: ALHAMISI BAADA YA MAJIVU
Mt. Leandri, Askofu
Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1:  Kum. 30: 15-20

Musa aliwaambia watu akisema: “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki. Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia; nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia, hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yordani, uingie kuimiliki. Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.”

Wimbo wa Katikati. Zab 1:1-4,6

1. Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Basi sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. (K)

(K) Heri mtu aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.

2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)

3. Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)

Injili. Lk 9: 22-25

Siku ile: Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka. Akawaambia wote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?”

TAFAKARI

NIKUFUATAJE BWANA? Katika maisha yetu kama wakristo, lazima lengo letu liwe kufika Mbinguni. Katika safari ya kulitimiza lengo hili tumepewa uhuru wa kuchagua, kwani tuna akili na utashi. Uchaguzi tuufanyao ndio utakaopelekea kikomo cha maisha yetu. Je, tunachagua kumfuata Bwana au la? Je, tunajiuliza ni kwa namna gani tunamfuata Bwana? Musa aliwaeleza watu juu kuchagua njia ipi ya kufuata mbele ya Bwana, je ni uzima na mema au mauti na mabaya? Aliwaeleza kinagaubaga juu ya matokeo ya uchaguzi kwamba mtu akichagua mema atabarikiwa katika nchi ya kuimiliki na mtu akichagua upotovu ataangamia. Yesu aliwaambia wafuasi wake, mtu yeyote anayetaka kumfuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, amfuate. Namna ya kumfuata Bwana ni kwa kuchagua mambo yaliyo mema na kukataa maovu, ni kwa kuwa tayari kupata mateso kwa ajili ya imani, ni kwa kuvumilia mateso. Ni kwa kuzisahau nafsi zetu kwa ajili ya wenzetu, huku ndiko kujitoa sadaka.

SALA: Ubinadamu wetu haufai kitu mbele yako Ee Bwana, utujalie mwamko wa kujitakasa maovu yetu ili tuweze kuwa wafuasi wako bora, amina.