Select Page

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa takatifu 17/02/2024

2024 FEBRUARI 17 JUMAMOSI BAADA YA MAJIVU
Wat. Waanzilishi saba wa shirika la Watumishi wa Bikira Maria
Urujuani
Zaburi: Juma 4

Somo 1. Isa 58: 9b-14

Bwana asema hivi: kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui. Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia. Kama ukigeuza mguu wako usiihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe; wala kuyatafuta ya kupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe; ndipo utakapojifurahisha katika Bwana; nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha Bwana kimenena hayo.

Wimbo wa Katikati. Zab 86:1-2, 3-4,5-6

1. Ee Bwana, utege sikio lako unijibu,
Maana mimi ni maskini na mhitaji,
Unihifadhi nafsi yangu,
Maana mimi ni mcha Mungu.
Wewe uliye Mungu wangu,
Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini. (K)

(K) Ee Bwana, unifundishe njia yako;
       Nitakwenda katika kweli yako. 


2. Wewe, Bwana unifadhili,
Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako,
Maana nafsi yangu yakuinulia Wewe Bwana. (K)

3. Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema,
Umekuwa tayari kusamehe,
Na mwingi wa fadhili,
Kwa watu wote wakuitao.
Ee Bwana, uyasikie maombi yangu;
Uisikilize sauti ya dua zangu. (K)

Injili. Lk 5: 27-32

Siku ile: Yesu aliona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaacha vyote, akaondoka, akamfuata. Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake; palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao. Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung’unikia wanafunzi wake, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?” Yesu akajibu akawaambia, “Wenye afya hawana haja ya tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”

TAFAKARI

BWANA NAACHA YOTE YA ULIMWENGU HUU NAKUFUATA WEWE: Kuacha mambo ya ulimwengu si kwa kutotumia mali na mambo ya ulimwengu, bali kuyatumia kadiri ya mpango wa Mungu. Katika kipindi hiki tunaalikwa kujikatalia, kuachilia yale yasiyofaa na kumwendea Bwana. Tumeshuhudiwa na ujumbe wa Bwana kupitia Nabii Isaya kwa taifa la Yuda, kwamba wakiacha maelekeo yao maovu, wakijali wahitaji, wakiishika siku ya Bwana, ndipo wataongozwa na Bwana, nuru yao itapambazuka gizani. Tena watarithishwa urithi wa Yakobo baba yao. Katika Injili, Mtoza ushuru Lawi, baada ya kuitwa na Yesu, aliacha yote na kumfuata, jambo lililowafanya Mafarisayo na waandishi wanung’unike na kuuliza swali. Jibu la Yesu linadhihirisha shauku ya Yesu kwa wanadamu juu ya kutubu dhambi. Wapendwa, maishani ili kutimiza wajibu wetu mbele za Mungu na wenzetu, ni lazima tujitoe sadaka, tuachilie mambo ya ulimwengu huu, ambako ni pamoja na kuacha maelekeo mabaya hasa kwa kutubu. 

SALA: Bwana, tunakuomba utujalie ujasiri wa kutojishikamanisha na mali kiasi cha kutosikia mwaliko wa kukufuata Wewe.