Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 03/05/2024

2024 MEI 3 : IJUMAA-JUMA LA TANO LA PASAKA

WAT. FILIPO NA YAKOBO, MITUME
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Juma 1

Somo 1. 1 Kor 15:1-8

Ndugu zangu, nawaarifu ile Injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri; isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake.

Wimbo wa Katikati. Zab 19:2-5

“1. Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa. (K)

K) Sauti yao imeenea duniani mwote.

2. Hakuna lugha wala maneno,
Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
Katika hizo ameliwekea jua hema. (K)”

Injili. Yn 14:6-14

Yesu alimwambia Tomaso: Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba, tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuoneshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuoneshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe. Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.

SALA: Ee Yesu naomba unifungue macho yangu ya imani nimwone Baba kupitia wewe.

TAFAKARI

YESU NI NJIA YETU: Leo tunaadhimisha sikukuu ya watakatifu Filipo na Yakobo mitume. Hawa walitambua umuhimu wa maisha ya sadaka ili waweze kufika kwa Baba. Katika Injili tunaona kuwa Yesu ni Sakramenti ya Baba, yaani tunamwona Baba kupitia Yesu. Yesu anaposema yeye ni njia ya kwenda kwa Baba, hamaanishi kuwa yeye ni barabara tu bali anayetaka kwenda kwa Baba ni lazima aishi na kutenda kama Yesu. Yeye ni njia kwa kuwa yeye ndiye mlango wa kuingia na kutoka (Yn 10:9). Yeye ndiye ukweli kwani kwa kumtazama yeye tunamwona Baba. Yeye ni uzima kwani kwa kuishi kama yeye tunaungana na Baba anayetupa uzima. Swali la Philipo la kutamani kumwona Baba liwe tamanio letu sote ila tusimtafute Baba nje ya Yesu. Tumwone Baba katika Neno lake, katika Sakramenti zake, katika mamlaka funzi ya kanisa na katika nafsi ya kuhani mwadhimishaji wa mafumbo matakatifu ya imani yetu. Pia tumwone Baba katika mapokeo matakatifu yanayofunuliwa kwetu na Yesu Kristo.