Masomo ya Misa Feb 16

Itukuzwe Damu ya Yesu… Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 16/02/2024

2024 FEBRUARI 16 IJUMAA: IJUMAA BAADA YA MAJIVU
Mt. Romano, Abati/ Mt. Lupisini Mtawa
Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1:  Isa. 58: 1-9

Bwana Mungu asema hivi: piga kelele, usiache, paza sauti yako kama tarumbeta; uwahubiri watu wangu kosa lao, na nyumba ya Yakobo dhambi zao. Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu. Husema, “mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii?” Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, nakupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je! kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Si siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana. Je! saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Sio kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, “Mimi hapa.”

Wimbo wa Katikati. Zab 51:3-6a, 18-19

1. Maana nimejua mimi makosa yangu,
Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako,
Na kufanya maovu mbele za macho yako. (K)

(K) Moyo uliovunjika na kupondeka,
      Ee Mungu, hutadharau.    


2. Tazama mimi naliumbwa katika hali ya uovu;
Mama yangu alinichukua mimba hatiani.
Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni
Nawe wanijulisha hekima kwa siri. (K)

3. Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako,
Uzijenge kuta za Yerusalemu .
Ndipo utakapopendezwa na dhabihu ya haki;
Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. (K) 

Injili. Mt 9: 14-15

Siku ile: Yesu alipofika ng’ambo, katika nchi ya Wagerasi, wanafunzi wake Yohane wakamwendea, wakasema, “Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi?” Yesu akawaambia, “Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga.”

TAFAKARI

NIFUNGE NAMNA GANI? Katika kipindi hiki tunachoalikwa na Mama Kanisa kutafakari juu ya matendo yetu na kufanya toba, tunaalikwa pia kufunga kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Tujiulize, tunapaswa kufaunga vipi? Nabii Isaya anatukumbusha juu ya namna ya kufunga kupitia ujumbe wa Bwana ambao unamtaka awakumbushe watu wake na nyumba ya Yakobo juu ya dhambi zao. Wao wanafunga ili kujionesha, kutafuta anasa, kufunga kwao ni katika maovu. Wanaelezwa namna bora ya kufunga impendezayo Bwana, yaani kufunga vifungo vya uovu, kujali watu na kutenda haki. Kuwasaidia wenye mahitaji kama vile, chakula, nguo n.k. Walielezwa kuwa namna hii ndiyo itakayowastahilisha mbele ya Bwana. Kwa Wayahudi kufunga kulifanywa siku ya upatanisho ambapo watu walipaswa wajitese kwa kuachilia vionjo vya kimwili kama vile kula, kunywa, n.k. Mafungo yanalenga kupata furaha ya ukombozi na utimilifu wake upo kwa Yesu. Tujifunze kuacha dhambi, kujikatalia, kuwasaidia wasiojiweza na kusali zaidi. 

SALA: Ee Bwana tunaomba utujalie moyo wa majitoleo na kujali wahitaji kwani katika wao tunakuona wewe, amina. 

About the Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You may also like these