Select Page

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa takatifu 18/02/2024

2024 FEBRUARI 18. DOMINIKA YA 1 YA KWARESIMA 
Urujuani
Zaburi: Juma 1

Somo 1. Mwa 9:8-15

Mungu akamwambia Nuhu, na wanawe pamoja naye, akisema, Mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi, tena na uzao wenu baada yenu; tena na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi; ndege, na mnyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi. Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo, kuiharibu nchi. Mungu  akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele; Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi. Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni, nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili.

Wimbo wa Katikati.  Zab 25:4-9

1. Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha
Maana wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu.  (K)

(K) Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli,
       Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.  

 
2. Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako,
Maana zimekuwako tokea zamani.
Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako,
Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako. (K)

3. Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake.  (K)

Somo 2. 1 Pet 3:18-22

Kristo aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri; watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji. Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo. Naye yupo mkono wa kuume wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake.

Injili. Mk 1:12-15

Roho alimtoa Yesu aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia.  Hata baada ya Yohane kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.

TAFAKARI
Ni Dominika ya kwanza ya Kwaresima. Maneno mawili makuu yanasikika: Dhambi na Toba. Somo la kwanza (Mwa 9:8-15) linasimulia kisa cha Nuhu na familia yake. Kiini cha simulizi hii ni kuenea kwa uovu ulimwenguni. Tukisoma kitabu cha Mwanzo kuanzia sura ya 6 hadi sura ya 11 tunaelezwa jinsi mwanadamu alivyozidi kutenda uovu na kumwasi Mungu na kukataa ufunuo wake (Mwa 6:5-6; taz. Rum 1:20-25). Mwanadamu alizama katika dhambi na hasa ile ya uasherati. Kutokana na uovu huo Mungu akaamua kuiangamiza dunia na kila kiumbe ambacho kilikuwa juu ya uso wa nchi ili kuitengeneza dunia mpya.
Hata hivyo kulikuwa na familia moja tu iliyomcha Mungu, familia ya Nuhu. Nuhu na familia yake walibaki kuwa waaminifu kwa Mungu. Aliishi na Mungu bila kuachana naye (Mwa 6:8-11). Mungu alitumia gharika (Mwa 6:5-7,17) kuiangamiza dunia na watu wake wote isipokuwa Nuhu na familia yake, ambapo Mungu alimwamuru atengeneze safina (mfano wa meli kubwa) ya kumuhifadhi yeye na familia yake pamoja na wanyama wawili wawili wa kila aina. Kwa siku 40 usiku na mchana ikanyesha mvua kubwa iliyoambatana na aina fulani ya matetemeko ya nchi (Mwa. 7:11-12). Tukio hili lilikuwa ni zaidi ya tsunami. Hata baada ya mvua kuacha, ilichukua muda mrefu hadi maji kupungua. Na miezi minne baada ya hayo safina ikatulia juu ya mlima Ararati (Mwa 8:3-4). Lakini ni miezi saba baadaye Nuhu, watu wake na wanyama waliweza kutokana safinani na kuanza maisha mapya duniani (Mwa. 8:14-19). Na baada ya hayo, ndipo Mungu anaweka agano na Nuhu. Mungu anaahidi kwamba hataiharibu tena nchi. Na kama ishara ya agano hilo akauweka upinde winguni. (Mwa. 9:8-15).
Wakati Mungu anaahidi kutoiangamiza dunia, swali linakuja, Je, uovu umetoweka duniani? Je, mwanadamu ameacha uasi dhidi ya Mungu? Je, hukuna tena dhambi duniani? Majibu ya maswali haya tunayapata katika Injili ya leo Mk.1:12-15). Yesu anashinda majaribu ya Shetani. Anaenda Galilaya. Na anaanza kuhubiri. Na ujumbe wake mkuu ni: “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni na kuiamini Injili”(Mk. 1:15). Kwanini tunaalikwa kutubu? Ni kwa sababu tu wadhambi.
Dhambi ni uasi dhidi ya Mungu. Uasi huu humtenga mtu na Mungu. Na njia ya ya kuunganika tena na Mungu ni kutubu; kufanya toba. Toba ni hali ya kubadilika ndani ya moyo. Ni ile metanoia. Kutubu ni kuitikia mwaliko wa kuacha dhambi na kumrudia Mungu. Ni kuomba rehema na huruma ya Mungu. Hali hiyo ya mabadiliko ya ndani huchagizwa na matendo ya nje: Sala pamoja na kufunga kunakoendana na kurarua mavazi, kuvaa magunia (1Fal 20:31; 2Fal 6:30; Isa. 22:12); na kujipaka majivu (Isa 58:5). Mababa wa Mtaguso wa II wa Vatikano wanafundisha kwamba “Toba ya wakati wa Kwaresima isiwe ni tendo la ndani na la binafsi tu, bali pia lionekanalo kwa nje na katika maisha ya jamii”(Hati za Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, Liturujia, 110).
Mwenyezi Mungu anatupatia sisi pia nafasi ya kumrudia. Anatupatia safina, Kanisa kama chombo chetu cha kutupatia wokovu. Ili kutupa wokovu, Mama Kanisa ametupatia Sakramenti ili “Kututakatifuza wanadamu…kutupatia neema…pia kuwezesha kumheshimu Mungu jinsi ipasavyo na kufanya matendo ya huruma”(Hati za Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, Liturujia, 59). Lakini kwa namna ya pekee Mama Kanisa ametuwekea Sakramenti ya Kitubio ambayo “Wanayoijongea hupokea humo kutoka huruma ya Mungu ondoleo la makosa yaliyotendwa dhidi yake, na papo hapo hupatanishwa na Kanisa, ambalo dhambi yao imelijeruhi…”(Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, Fumbo la Kanisa, 11). Sakramenti ya Kitubio ni njia ya kujipatanisha na Mungu. Kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio wakosefu hupatanishwa si na Mungu tu, bali pia na Kanisa.
Mimi na wewe tunaalikwa kufanya toba. Na wakati ndio huu. Tumepewa siku 40 za kujitakasa na kuacha njia zetu mbaya. Tuongozane na Yesu ambaye “aliteswa Mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili ya wasio na haki”(1Pet 3:18); kwenda naye jangwani ili kwa njia ya sala na mfungo tuweze nasi kupata nguvu ya kumshinda Shetani/Ibilisi na hila zake zote. Kwaresima iwe kwetu kipindi cha kukua kiroho; kipindi cha mazoezi ya nidhamu ya kiroho. Tukiwa mwanzoni Kabisa mwa Kwaresima, tumwombe Mungu tukisema “Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako, uniongoze katika kweli yako. Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu”(Zab 25:4-5).

SALA: Ee Bwana utujalie moyo wa toba ya kweli ili tuiishi vyema Kwaresima.