Itukuzwe Damu ya Yesu… Karibu Katika Masomo ya Misa 15/02/2024

2024 FEBRUARI 15 ALHAMISI: ALHAMISI BAADA YA MAJIVU
Mt. Leandri, Askofu
Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1:  Kum. 30: 15-20

Musa aliwaambia watu akisema: “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki. Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia; nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia, hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yordani, uingie kuimiliki. Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.”

Wimbo wa Katikati. Zab 1:1-4,6

1. Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Basi sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. (K)

(K) Heri mtu aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.

2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)

3. Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)

Injili. Lk 9: 22-25

Siku ile: Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka. Akawaambia wote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?”

TAFAKARI

NIKUFUATAJE BWANA? Katika maisha yetu kama wakristo, lazima lengo letu liwe kufika Mbinguni. Katika safari ya kulitimiza lengo hili tumepewa uhuru wa kuchagua, kwani tuna akili na utashi. Uchaguzi tuufanyao ndio utakaopelekea kikomo cha maisha yetu. Je, tunachagua kumfuata Bwana au la? Je, tunajiuliza ni kwa namna gani tunamfuata Bwana? Musa aliwaeleza watu juu kuchagua njia ipi ya kufuata mbele ya Bwana, je ni uzima na mema au mauti na mabaya? Aliwaeleza kinagaubaga juu ya matokeo ya uchaguzi kwamba mtu akichagua mema atabarikiwa katika nchi ya kuimiliki na mtu akichagua upotovu ataangamia. Yesu aliwaambia wafuasi wake, mtu yeyote anayetaka kumfuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, amfuate. Namna ya kumfuata Bwana ni kwa kuchagua mambo yaliyo mema na kukataa maovu, ni kwa kuwa tayari kupata mateso kwa ajili ya imani, ni kwa kuvumilia mateso. Ni kwa kuzisahau nafsi zetu kwa ajili ya wenzetu, huku ndiko kujitoa sadaka.

SALA: Ubinadamu wetu haufai kitu mbele yako Ee Bwana, utujalie mwamko wa kujitakasa maovu yetu ili tuweze kuwa wafuasi wako bora, amina.