Select Page

Masomo ya Misa Machi 3

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 03/03/2024


2024 MACHI 3 JUMAPILI: DOMINIKA YA 3 YA KWARESIMA
Urujuani
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Kut 20 :1-17

Mungu alinena maneno haya yote akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa Usiwe na miungu ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure jina la Bwana, Mungu wako, maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure. Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana Mungu, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba, kwa hiyo Bwana akaibariki siku ya Sabato akaitakasa. Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako. Usiue. Usizini. Usiibe. Usimshuhudie jirani yako uongo. Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng’ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako. 

Wimbo wa Katikati. Zab 19: 8-11

1. Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima. (K)

(K) Wewe, Bwana, ndiwe mtakatifu wa Mungu. 
   
2. Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia macho nuru.  (K)

3. Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli
Zina haki kabisa (K)

4. Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
Kuliko wingi wa dhahabu safi.
Nazo ni tamu kuliko asali,
Kuliko sega la asali. (K)

Somo 2. 1 Kor 1 :22-25

Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu. Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu.

Injili. Yn 2 :13-25

Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara. Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila. Basi Wayahudi wakajibu wakamwambia, Ni ishara gani utuoneshayo, kwamba unafanya haya?  Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake. Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema  hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu.  Hata alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizofanya. Lakini Yesu hakujiaminisha kwao; kwa kuwa yeye aliwajua wote; na kwa sababu hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu; kwa maana yeye mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwandamu.

TAFAKARI

LIVUNJENI HEKALU HILI NAMI NITALIJENGA KWA SIKU TATU
Amri, maagizo, miongozo na kanuni hupatikana katika jamii ya mwanadamu kwa ajili ya kuleta uwiano wa kimaisha. Wanapoishi watu wawili au zaidi kuna umuhimu wa kuweka miongozo ambayo itawezesha amani, haki na uelewano kati ya watu. Katika jamii yoyote ya kidini, kisiasa au kiuchumi mwanadamu huandaa kanuni mbalimbali kwa makusudi tajwa hapo juu kusudi kuepuka migongano kati ya wahusika wa jamii fulani. Mwenyezi Mungu ambaye ni muumba wetu ametuwekea pia amri zake ili tuweze kuishi kwa kadiri ya maongozi yake na kuyatimiza mapenzi yake. Kitabu cha kutoka kimetuorodheshea amri hizi za Mungu ambazo kwa haki zinaratibu uhusiano wetu na Mungu na uhusiano wetu na binadamu wenzetu. Mwanadamu anapokiuka amri za Mungu anatenda dhambi na hivyo anaalikwa kufanya toba na kumrudia Mungu.
Majira ya Kwaresima yanatualika katika toba. Ni wazi mwaliko huu unatutaka kurejea katika Amri za Mungu. Lakini lipo jambo la msingi ambalo kwalo amri, sheria, kanuni au mwongozo wowote ule unapaswa kulenga. Jambo hilo ni kukua na kukomaa. Hivyo safari hii ya toba isitumike tu kama fursa ya kuorodhesha makosa yako na kuomba msamaha bali ni majira ya kukua na kuimarika kiroho. Amri za Mungu zinapaswa kutukuza na kutuimarisha kiroho. Huku ndiko kukua kwa upendo wetu kwa Mungu na kwa jirani zetu (rej. Mt 22:37 – 40). Tendo hili la kukua katika upendo linaonekana katika utayari wa kujifunua na kutimiza mapenzi ya Mungu na kwa upande mwingine kuiona nafsi ya jirani yako na kuifanya kuwa kama yako. Hivyo amri za Mungu zinapaswa kutuelekeza katika kuimarika kwa fadhila za upendo, imani na matumaini.
Ni changamoto ambayo inawekwa mbele yetu wakati wa majira haya ya Kwaresima. Tunapaswa kujiuliza namna ambavyo tumefanikiwa kuistawisha taswira ya Mungu na ya jirani yangu ndani ya nafsi yangu. Ipo hatari ya kuzitimiza amri za Mungu kwa kutaka kuonekana na hivyo kubaki kudumaa kiroho. Hii ni ile hali ya mmoja anapojitahidi kutimiza amri ili kuepa adhabu. Namna hii kamwe haimsaidii mtu. Namna hii inatupelekea hata mara nyingine kushindwa kuufunua upendo wa Mungu ambao ni lengo msingi la amri za Mungu na kusisitizwa zitekelezwe tu hata bila kutumia hekima. Mazingira haya ya kutekeleza amri au kanuni kwa ajili ya kuonekana yamekemewa tangu mwanzoni mwa Kwaresima. Mmoja yupo radhi mithili ya Kuhani na Mlawi katika simulizi la Msamaria Mwema (rej. Lk 10:31 – 32) kumwacha jirani yake anaangamia kwa kigezo cha kwenda kutimiza amri ya Mungu.
Nabii Isaya alituonya juu ya mfungo wa kufuatilia tu maelekezo ya kisheria bila kukua kwa upendo kati yako na jirani zako: “Je, saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii … siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta masikini waliotupwa nje nyumbani kwako, umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo? (Isa 58:7). Ni tendo ambalo linapaswa kumfanya Kristo aendelee kukua ndani mwetu nasi kupungua. Tunapomfanya Yeye kukua ndani mwetu tunampatia nafasi ya kuadhimishwa ndani mwetu na hivyo yote anayoyatimiza kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu, yaani yale yanayofupishwa katika Injili ya Luka 4:18 – 19 yanaadhimishwa katika maisha yako. Amri na Torati yote kama tulivyotafakari Dominika iliyopita inajumuishwa katika nafsi ya Kristo, hivyo tunapomwadhimisha Kristo kwa uaminifu na kuueneza upendo wake tunapewa fursa ya kuzitimiza Amri za Mungu.
Kristo katika Injili anawaumbua Wayahudi ambao walijikinai kuzishika amri za Mungu lakini si katika namna inayofaa. Viongozi wa dini na watu wengine wenye uwezo walitumia nafasi zao katika hekalu na kuligeuza kuwa si mahali pa kuufunua upendo wa Mungu bali kuendelea kuwanyonya na kuwakandamiza wengine. Aliwaambia: “msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara”. Ni wazi biashara hizo zilifanywa si kwa kuwasaidia waliotoka mbali kupata urahisi wa kutoa dhabihu zao bali waliwaibia kwa kuwazidishia gharama; wale waliobadilisha fedha waliweka faida ya juu ili kupata zaidi na hawa wote walilindwa na viongozi wa hekalu ambao pengine walifaidika kwa namna fulani. Tendo hili la kutoa sadaka ambalo lilikubalika kisheria liligeuka kuwa ni fursa ya unyonyaji na kupora upendo wa ndugu kwa ndugu.
Kristo anawaambia: “Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha.” Ni tangazo la mapinduzi yaliyoletwa na Kristo. Hekalu lipaswalo kubomolewa ni mioyo ya wanadamu iliyojaa dhuluma na unyonyaji wa hadhi wa mwanadamu mwenzeke. Yeye ambaye anatumia nafasi yake na hata wakati mwingine kujikinai kwa njia za kihalali kuwepo katika nafasi hiyo lakini si katika kuonesha upendo bali kumwangamiza mwanadamu. Huyo kisheria ataonekana ametimiza wajibu wake lakini sheria hiyo haijamkuza katika upendo kwa Mungu na kwa jirani yake. Mapinduzi yaletwayo na Kristo ni mwaliko wa kubadili mwenendo wetu. Ni wito wa kuitafakari jamii yetu ambayo inaendelea kumgandamiza na kumgaragaza mwanadamu kwa jina la sheria na taratibu ambazo kwa ujumla wake zinakinzana na ukweli wa amri za Mungu. Hakutapaswi kubaki katika ishara au ushahidi wa kidunia kama wayahudi au hekima za kidunia kama wayunani bali ni kumtanguliza “Kristo nguvu ya Mungu.”
Kukua na kuimarika kiroho kunawezeshwa pia na tafakari ya dhati ya mazingira ambayo hupelekea mmoja kuanguka dhambini. Hizi ni nafasi za vishawishi. Tunapaswa kujikumbusha kuwa sisi tu mithili ya mshumaa ambao ukipita au kupitishwa karibu na moto lazima utayeyuka. Hivyo tunaalikwa kujitafakari na kujiuliza: Ni nini ambacho huyeyusha uwepo wa Mungu ndani mwangu? Ni nini ambacho roho yangu hushindwa kuhimili joto lake na hivyo kuvunja amri na maagizo ya Mungu? Kila mmoja anao uwezo wa kutambua mazingira yanayomwangusha dhambini. Kama ni udhaifu wako katika kutawala kilevi basi unapaswa kukimbia mazingira hayo; kama ni udhaifu wako wa kushindwa kutawala tamaa za mwili kwa kuona ama filamu au picha za utupu au kuwaona watu wa jinsia tofauti na wewe katika mzingira fulani unapaswa kuyakimbia mazingira hayo; kama ni udhaifu wako katika kushindwa kuwa mwaminifu katika mali zako binafsi na za jumuiya tafuta mbinu muafaka n.k. Tembea vema ili kuzishika vema amri za Mungu na hatimaye mwisho wa majira haya uwe umekuwa kiroho na kimwili.

SALA: Ee Mungu utujalie neema ya kushika amri zako kiaminifu. Amina.

Masomo ya Misa Machi 2

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 02/03/2024


2024 MACHI 2 JUMAMOSI: JUMA 2 LA KWARESIMA
Mt Agnes wa Praha au Bohemia 
Urujuani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Mik 7: 14-15, 18-20

Walishe watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, wakaao peke yao, mwituni katikati ya Karmeli; na walishe katika Bashani na Gileadi, kama siku za kale. Kama katika siku zile za kutoka kwako katika nchi ya Misri nitamwonyesha mambo ya ajabu. Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema. Atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu yetu; nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya bahari. Wewe utamtimilizia Yakobo kweli yako, na Ibrahimu rehema zako, ulizowaapia baba zetu tangu siku za kale.

Wimbo wa Katikati. Zab 103:1-4, 9-12

1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote. (K)

(K) Bwana amejaa huruma na neema.
  
2. Akusamehe maovu yako yote,  
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema. (K)

3. Yeye hatatea siku zote,
Wala hatashika hasira yake milele.
Hakututenda sawa na hatia zetu,
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.

4. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. (K)

Injili. Lk 15: 1-3, 11-32

Watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia Yesu wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung’unika, wakisema, ”Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.” Akawaambia mfano huu, akisema, ”Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, ”Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, ”Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteeni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.” Wakaanza kushangilia. Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumshi mmoja, akamwuliza, ‘Mambo haya, maana yake nini?’ Akamwambia, ‘Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima.’ Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema. ‘Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. Akamwambia, ‘Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”’

Tafakari

MZAZI NI MUNGU WA HAPA DUNIANI: Kuna usemi wa wahenga usemao “Damu ni nzito kuliko maji.” Maana halisi ya usemi huu ni kuwa, ndugu wa damu ana umuhimu wa kipekee, hata akifanya kosa laweza angaliwa kwa namna tofauti na inavyotarajiwa. Huyu baba tuliyemsikia katika Injili, kitendo alichokifanya cha kumpokea mwanae huyu aliyekwisha tapanya mali yake kwa ulevi na maisha ya kihuni, na sasa anarudi tena nyumbani. Kwa ulimwengu wa leo hii ni vigumu sana, sio ajabu kwa wengine wetu tungemfukuza au kumfungulia mashtaka ya wizi au ubadhirifu wa mali na hata tukasahau kuwa ni ndugu. Baba huyu anasimama katika nafasi ya Mungu, kuwa Mungu anatuhurumia na kutusamehe bila hata kujali uzito wa kosa ili mradi mhusika/mdhambi amechukua hatua na kurudi kwa unyenyekevu na kukiri kosa/dhambi husika wazi wazi. Leo hii tujiulize tunaungamaje dhambi zetu? Je tunazitaja wazi wazi na kukusudia kuziacha? Au tunaungama kwa kuficha nyingine kwa kusema, ‘naungama na zile nilizozisahau’ angali unazikumbuka vyema, au tunaona aibu kuungama!

SALA: Baba wa Huruma, tunaomba neema ya kutambua makosa yetu na kuyakiri bila kificho kwako.

Masomo ya Misa Mar 1

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 01/03/2024


2024 MACHI 1 IJUMAA: JUMA 2 LA KWARESIMA
Mt. Switberti, Askofu
Urujuani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Mwa 37:3-4, 12-13, 17-28

Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, ”Je, Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo nikutume kwao.” Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, ”Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja! Haya, twende tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, ”Mnyama mkali amemla;” kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake! Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, ”Tusimwue.” Reubeni akawaambia, ”Msimwage damu; mtupeni katika birika hii iliyopo nyikani, wala msimguse;” ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula chakula.  Wakainua macho yao, wakaona msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, ”Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? Haya na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yenu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu.” Ndugu zake wakakubali. Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.  

Wimbo wa Katikati. Zab 105:16-21

1. Akaiita njaa iijilie nchi,
Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
Alimpeleka mtu mbele yao,
Yusufu aliuzwa utumwani. (K)

(K) Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.   
  
2. Walimwumiza miguu yake kwa pingu,
Akatiwa katika minyororo ya chuma.
Hata wakati wa kuwadia neno lake,
Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)

3. Mfalme alituma watu akamfungua
Mkuu wa watu akamwachia.
Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,
Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)

Injili. Mt 21: 33-43; 45-46

Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa watu, ”Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza, wakawatenda vilevile. Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu.’ Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, ‘Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake.’ Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, ‘Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake.” Yesu akawaambia, ”Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake. Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata waliwaogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.

TAFAKARI

WIVU HAUJENGI: Daima maisha hukosa ladha hasa pale tunaposhindwa kufikiri kwa pamoja na kuamua yanayofanana. Tusipokubaliana kuwa na msemaji mmoja, mwisho tunajikuta tumegawanyika na kuishia hata kuwa na wivu. Somo la kwanza tumeona jinsi kaka zake na Yusufu walivyokuwa na wivu juu ya ndugu yao kwa sababu ya kupendwa zaidi na baba yao. Na katika Injili wale wakulima wanamwonea wivu mtoto wa bwana wao kisa ni mrithi. Jamii yetu ya leo imegubikwa na wivu unaozidi kuchanua kila uchwao. Watu wanasemana visivyo sehemu zao za kazi ili kuchafuliana na hii inapelekea hadi mtu kufukuzwa kazi, tunasahau kuwa kila mmoja ana bahati yake, hata vidole vya mikono havilingani. Wivu ni matokeo ya kutoridhika na haki yako au bahati yako, kupenda kuwa sawa na mwingine au kuwa zaidi.

Masomo ya Misa Feb 29

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 29/02/2024


2024 FEBRUARI 29 ALHAMIS: JUMA 2 LA KWARESIMA
Mt. Aswoldi, Askofu 
Urujuani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Yer 17: 5-10

Bwana asema hivi: ”Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, hataona yatakapotokea mema; bali atakaa jangwani palipo ukame, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, uenezao mizizi yake karibu na mto; hautaona hofu wakati wa hari ujapo, bali jani lake litakuwa bichi; wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, wala hautaacha kuzaa matunda. Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.

Wimbo wa Katikati Zab 1:1-4, 6

1. Heri mtu Yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sharia ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku . (K)

(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.  

2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)

3. Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)

Injili. Lk 16: 19-31

Yesu aliwaambia Mafarisayo: ”Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamlamba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, ”Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Ibrahimu akasema, ‘Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu’. Akasema, ‘Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso’. Ibrahimu akasema, ‘Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao.’ Akasema, ‘La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu.’ Akamwambia, ‘Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishiwa hata mtu akifufuka katika wafu.”’

TAFAKARI

MAMBO YA DUNIANI NI YA MUDA MFUPI, YADUMUYO NI YA MBINGUNI: Licha yetu sisi wanadamu kuwa na akili na utashi, bado tunaangukia katika wimbi la kutopambanua na kuchagua vema. Wengi tunachagua mambo yatuleteayo vionjo vya kidunia na si wokovu wetu. Wengi tunajiamini na kuwaamini wanadamu wenzetu na si Mungu. Tumeshuhudiwa na ujumbe wa Bwana uelezao juu ya kulaaniwa mtu amtegemeaye mwanadamu na kubarikiwa mtu amtegemeaye Bwana. Namna hii ya uovu tunaiona kwa tajiri ambaye amekuwa akilimbikiza mali na kutomjali Lazaro aliyekuwa maskini. Baada ya vifo vyao Lazaro anafurahia na malaika mbinguni, lakini tajiri anateseka kuzimu. Tajiri alijikita katika kujilimbikizia mali za ulimwengu huu zipitazo lakini Lazaro alijitafutia mbingu angali hapa duniani. Katika maisha yetu tuwe watu wa kujali wenzetu, watu wa majitoleo tuwasaidie wenzetu tungali bado hapa dunia hasa kuwaelekeza kumfahamu na kumtegemea Mungu. Wakati wetu ni sasa tusisubiri baadaye. Yote tuyatende kwa sifa na utukufu wa Mungu na si kwa kujionesha mbele ya wanadamu.

SALA: Tunakuomba Mwenyezi Mungu utukuwa chachu ya kuwajali wenzetu na tuyafanye yote kwa sifa na utukufu wako. Amina.

Masomo ya Misa Feb 28

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 28/02/2024


2024 FEBRUARI 27 JUMANNE: JUMA 2 LA KWARESIMA
Mt. Romano na Mt. Lupisini 
Urujuani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Yer 18: 18-20

Waliposema, ”Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote. Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili niseme mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.

Wimbo wa Katikati. Zab 31:4-5, 13-15

1. Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,
Maana Wewe ndiwe ngome yangu.
Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. (K)

(K) Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako, Ee Bwana. 

2. Maana nimesikia masingizio ya wengi;
Hofu ziko pande zote.
Waliposhauriana juu yangu,
Walifanya hila wauondoe uhai wangu. (K)

3. Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)

Injili. Mt 20: 17-28

Yesu alipokua akipanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia, ”Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi; nao watamhukumu afe; kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeredi, na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka”. Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, ”Wataka nini?” Akamwambia, ”Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako”. Yesu akajibu akasema, ”Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, ”Twaweza”. Akawaambia, ”Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.” Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; Kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumikia, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”

TAFAKARI.

TUSHUHUDIE IMANI KWA KUTUMIKIA: Ufuasi kwa Kristo uhusisha kulitangaza Neno lake. Katika kutangaza Neno la Kristo hatuwezi kukwepa wapinzani wa Kristo, jambo la msingi ni kusali, kuomba neema na ujasiri wa kuendelea, kumwomba Kristo mwenyewe atusimamie. Nabii Yeremia anasali, anamwomba Bwana amuangalie pale watesi wake wanapoibuka pindi amshuhudiapo Bwana. Yeremia anaomba kuimarishwa. Kristo mwenyewe anapowaeleza wana wa Zebedayo na mama yao juu ya ombi lao, anawataka waimarike katika kutumikia si katika nafasi. Kikombe alichokieleza Yesu ni safari nzima ya maisha ya kumfuasa yeye ambayo inajumuisha magumu pia. Yesu anawatia nguvu kwa kuwasihi wawe wanyenyekevu. Anawaimarisha wawe tayari kutumikia na siyo kutumikiwa. Katika maisha yetu tuwe tayari kutumikia pasi kuwa na shaka kwa sababu Yesu yu pamoja nasi. Wana wa Zebedayo walikuwa tayari kukinywea kikombe. Katika kuimarishwa nasi inatupasa tujitahidi kuiishi imani yetu kwa sababu ufalme wa Mungu ni kwa wale walioishi vizuri.

SALA: Ee Bwana utuimarishe katika safari yetu ya kuelekea mbinguni, utujalie nguvu tuweze kuishuhudia vema imani yetu, amina.

Masomo ya Misa Feb 27

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 27/02/2024


2024 FEBRUARI 27 JUMANNE: JUMA 2 LA KWARESIMA
Mt. Gelasio 
Urujuani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Isa 1: 10, 16-20

Lisikieni neno la Bwana, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. ”Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.”

Wimbo wa Katikati. Zab 50:8-9, 16-17, 21-23

1. Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
Na kafara zako ziko mbele yangu daima.
Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako,
Wala beberu katika mazizi yako. (K)

(K) Autengenezaye mwenendo wake,
       Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.


2. Una nini wewe luitangaza sheria yangu,
Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
Maana wewe umechukia maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. (K)

3. Ndivyo ulivyofanya, name nikanyamaza,
Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe,
Atoaye dhabihu za kushukuru, ndiye anayenitukuza.
Naye autegemeza mwenyendo wake,
Nitamwonyesha wokovu na Mungu. (K)

Injili. Mt 23: 1-12

Yesu aliwaambia makutano na wanafunzi wake, akasema, ”Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yo yote watakayowaambia, myashike, na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende, maana wao hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao, wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao; hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, ‘Rabi’. Bali ninyi msiitwe ‘Rabi’, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu ‘baba’ duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe ‘viongozi’; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.

TAFAKARI

TUJISTAHILISHE MBELE YA MUNGU KWA KUISHI VEMA: Wahenga wanasema, “Mkataa pema, pabaya panamwita.” Tunapotenda mema tunajiweka karibu na Mungu, tunapotenda dhambi tunajitengea na Mungu na tunajikabidhi kwa shetani. Waamuzi wa Sodoma na watu wa Gomora, wanaalikwa kutenda mema, wanaalikwa kuichukia na kuacha dhambi, pia wanaalikwa kumrudia Mungu haijalishi dhambi zao zina uzito wa namna gani, Bwana atawasamehe. Kwa kufanya hivyo watakuwa wamestahilishwa mbele ya Mungu. Yesu anawataka wanafunzi wake kuishi imani yao kwa kutoiga mifano mibaya ya Mafarisayo ambao wao hupenda kusema bila kuishi kile wakisemacho, anawataka wawe wanyenyekevu. Katika maisha yetu ya kumuelekea Mungu, hatuwezi kukwepa suala la kujistahilisha mbele yake. Tunajistahilisha kwa kuitafuta na kuitunza amani, kwa kutimiza wajibu wetu, kwa kupendana, kwa kutubu dhambi zetu. Daima maisha yetu yanapaswa kuwa kwa matendo zaidi kuliko maneno. Wengi wetu ni washauri wazuri lakini hatuishi ushauri huo, tunataka nani aishi? 

SALA: Ee Mungu uliye nguvu na kimbilio letu, tusaidie daima tuwe watu wa kutenda zaidi kuliko kuongea. Amina.