Select Page

Masomo ya Misa Machi 9

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 09/03/2024

2024 MACHI 9 JUMAMOSI: JUMA 3 LA KWARESIMA
Mt. Fransiska wa Roma 
Urujuani
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Hos 6:1-6

Bwana asema: ”Katika taabu yao watanitafuta kwa bidii: Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu.” Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake. Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi. Ee Efrahimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema. Kwa sababu hiyo, nimewakata-kata kwa vinywa vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa changu; na hukumu yangu itatokea kama mwanga. Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.

Wimbo wa Katikati. Zab 51:3-4, 18-21

1. Ee Mungu, unirehemu,
Sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu. (K)

(K) Ninavyotaka ni fadhili, si sadaka.

2. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
Moyo uliovunjika na kupondeka,
Ee Mungu, hutaudharau. (K)

3. Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako,
Uzijenge kuta za Yerusalemu.
Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki,
Na sadaka za kuteketezwa, na kafara (K)

Injili. Lk 18:9-14

Yesu aliwaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. ”Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; ”Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang`anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato  yangu yote.” Lakini yule mtoza ushuru alisisima mbali, wala hakudhubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, ”Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.” Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhilie atakwezwa. 

TAFAKARI

DHARAU MWISHO WAKE MAJUTO: Kama kuna sala inayofika kwa Mungu kwa haraka ni ‘sikitiko la mnyonge sababu ya kuonewa, kudhalilishwa na kukosa haki.’ Mwanadamu akifanikiwa wakati mwingine hujisahau na kuanza kudharau na kudhalilisha wengine. Huo tunaweza kuuita ni Ufarisayo. Huyu Mfarisayo alijiona kuwa bora kuliko yule mtoza ushuru na kuanza kujisifia kwa litania ya majigambo, oh mimi niko 1,2,3, mimi nina 1,2,3 na mbaya zaidi kusema, ‘mimi sio kama akina fulani wala kama huyu mtoza ushuru’. Mara nyingi wasio nacho hugandamizwa na walio nacho kiuchumi/kimadaraka. Kuna baadhi wakijaliwa hawaambiliki, wanajikweza na kujiona mungu mtu, wanajisahau na kudhani ni kwa nguvu zao, au wanastahili kuliko wengine, Mungu anakosa nafasi katika maisha yao, wanakosa unyenyekevu, wanajiona kuwa wao ni binadamu zaidi ya wengine. Tumwangalie huyu Mfarisayo na tujifunze kitu. Je, kwa kujua la mwenzako ndio unalitangaza? Tuko ambao tunaposali tunawaangalia wengine kwanza wanafanyaje. Huo ni ulemavu wa kiroho.

SALA: Ee Baba wa huruma, utuhurumie sisi wakosefu.

Masomo ya Misa Machi 8

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 08/03/2024

2024 MACHI 8 IJUMAA: JUMA 3 LA KWARESIMA
Mt. Yohane wa Mungu, Mtawa
Urujuani
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Hos 14:2-10

Bwana asema: ”Ee Israeli, mrudie Bwana, Mungu wako; maana umeanguka kwa sababu ya uovu wako. Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Bwana; mkamwambie, ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo tutakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng’ombe. Ashuru hatatuokoa; hatutapanda farasi; wala hatutaiambia tena kazi ya mikono yetu, Ninyi ndinyi miungu yetu; maana kwako wewe wasio na baba hupata rehema. Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao; nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo; kwa maana hasira yangu imemwacha. Nitakuwa kama umande kwa Israeli; naye atachanua maua kama nyinyoro, na kueneza mizizi yake kama Lebanoni. Matawi yake yatatandaa, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake kama Lebanoni. Na wao wakaao chini ya uvuli wake watarejea; watafufuka kama ngano, na kuchanua maua kama mzabibu; harufu yake itakuwa kama harufu ya divai ya Lebanoni.” Efrahimu atasema, ”Mimi nina nini tena na sanamu? Mimi mimeitika, nami nitamwangalia. Mimi ni kama mberoshi wenye majani mabichi. Kwangu mimi yamepatikana matunda yako. Ni nani aliye na hekima, naye atayafahamu mambo haya? Ni nani aliye na busara, naye atayajua? Kwa maana njia za Bwana zimenyoka, nao wenye haki watakwenda katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake.

Wimbo wa Katikati. Zab 81:6-9, 10-11,14-17

1. Maneno yake nisiyemjua naliyasikia.
Nimelitenga bega lake na mzigo,
Mikono yake ikaachana na kikapu.
Katika shida uliniita nikakuokoa. (K)

(K) Mimi ndimi Bwana Mungu wako, Sikiliza sauti yangu.  

2. Nalikuitikia katika sitara ya radi;
Nalikujaribu penye maji ya Meriba.
Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya,
Enyi Israeli, kama ukitaka kunisikiliza. (K)

3. Usiwe na mungu mgeni ndani yako;
Wala usimsujudie mungu mwingine.
Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,
Niliyekupandisha toka inchi ya Misri. (K)

Injili. Mk 12:28-34

Mmojawapo wa waandishi alifika, akawasikia wakisemezana naye, akatambua ya kuwa amewajibu vema, akamwuliza, ”Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?” Yesu akamjibu, ”Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja. Nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Yule mwandishi akamwambia, ”Hakika, Mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye; na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhabihu zote pia.” Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, ”Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu.” Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo.

TAFAKARI

UPENDO NI KILELE CHA UTAKATIFU: Somo la Injili limetawaliwa na dhamira ya upendo, mwandishi aliyemuuliza Yesu swali alichokoza na hivi akaibua mjadala mzima uliogusia suala la upendo. Katika maisha yetu twaweza peana zawadi nyingi, lakini zawadi pekee yenye maana unayoweza kumpa mtu ni upendo. Paulo katika barua yake kwa Waefeso 4:2-3 anatuasa tuishi maisha ya unyenyekevu, upole na uvumilivu tukichukuliana katika upendo ndani ya Roho Mtakatifu. Anaelezea zaidi kwenye aya ya 15-16 kuwa, upendo huu utatusaidia kumfikia Kristo aliye kichwa chetu. Ni katika jibu alilotoa Kristo katika swali aliloulizwa kuwa, upendo ndio ukamilifu wa yote. Ulimwengu umechafuka kutokana na kukosa upendo wa dhati, watu wanaishi upendo geresha, upendo danganya toto, watu wanatamkiana tu neno upendo lakini kiuhalisia hakuna upendo wowote.

SALA: Bwana Yesu tujalie mioyo yetu iweze kuwa chemchemi ya upendo kwa wote.

Masomo ya Misa Machi 7

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 07/03/2024

2024 MACHI 7 ALHAMISI: JUMA 3 LA KWARESIMA
Wat. Perpetua na Felisita, Mashahidi 
Urujuani
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Yer 7:23-28

Naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru, mpate kufanikiwa. Lakini hawakusikiliza, wala kutega sikio lao, bali walikwenda kwa mashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele. Tokea siku ile baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu ninyi, nikiamka mapema kila siku, na kuwatuma. Lakini hawakunisikiliza, wala kutega sikio lao; bali walifanya shingo yao kuwa ngumu; walitenda mabaya kuliko baba zao. Nawe utawaambia maneno hayo yote; lakini hawatakusikiliza; nawe utawaita; lakini hawatakuitikia. Nawe utawaambia, Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali na vinywa vyao. 

Wimbo wa Katikati. Zab 95:1-2, 6-9

1. Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)

(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu. 


2. Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)

3. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba,
Kama siku ya Masa jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)

Injili. Lk 11: 14-23

Yesu alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu. Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli. Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake. Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.

TAFAKARI

UKAIDI HUSABABISHA KUKOSA MENGI: Katika somo la kwanza, Nabii anajitahidi kuwaasa wanajamii husika lakini wanakuwa wakaidi. Yesu naye katika Injili anawaasa makutano lakini hawakubali na badala yake wanamsingizia uongo kuwa anatumia nguvu za giza. Yote haya yanasababishwa na ukaidi, kutokujikubali. Kuna watu ukiwashauri jambo tena la manufaa kwao, hawapokei ushauri, badala yake wanaanza kukuchambua wewe unayemshauri. Nilishashuhudia padre alimshauri mwanandoa ili aishi vyema kiapo chake cha ndoa kwa vile ilikuwa inavunjika, lakini matokeo yake yule mwanandoa alimjibu padre kuwa huwezi kunishauri kwani wewe (padre) hujaoa na hujui changamoto za ndoa. Hii inatokana na ukweli kuwa, alitaka kusimamia msimamo wake ambao haukuwa sahihi. Ndivyo ilivyokuwa hata kwa hawa wahusika wa Injili, walitaka kubaki katika msimamo wao na sio kupokea hii Huruma ya Mungu.

SALA: Tunakuomba Ee Yesu mwema, utupe moyo wa unyenyekevu na kujikubali.

Masomo ya Misa Machi 6

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa 06/03/2024

2024 MACHI 5 JUMANNE: JUMA 3 LA KWARESIMA
Mt. Koleta wa Corbie Bikira na Mtawa 
Urujuani
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Kum 4: 1, 5-9

Musa aliwaambia makutano: ”Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo. Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako.   

Wimbo wa Katikati. Zab 147:12-13, 15-16, 19-20

1. Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapigo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako. (K)

(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.

2. Huipeleka amri yake juu ya nchi,
Neno lake lapiga mbio sana.
Ndiye atoaye theluji kama sufu,
Huimwaga barafu yake kama majivu. (K)

3. Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua. (K)

Injili. Mt 5: 17-19

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: ”Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.

TAFAKARI

SHERIA NA TARATIBU HUSAIDIA KURATIBISHA MAMBO: Katika jamii yoyote ile, zipo sheria, taratibu na miongozo ambayo husaidia jamii husika katika kuratibisha mambo. Hata katika imani yetu zipo, Amri za kutuelekeza. Masomo yote ya leo yanasisitiza umuhimu wa sheria. Musa katika somo la kwanza, aliwaasa wana wa Israel kuzingatia Amri za Mungu ili wasivurugwe na zile za jamii iliyokuwa inawazunguka na Yesu katika Injili anakazia kufundisha Amri katika usahihi wake. Katika jamii yetu ya leo tunaona jinsi baadhi ya watawala wanavyotunga sheria za kukandamiza wanyonge na kujinufaisha wao, mahali pengine ukweli unapindishwa kisa mwenye kosa ni tajiri au kiongozi. Kwenye kusimamia sheria inahitajika Hekima ya hali ya juu. Mwanasaikolojia Anne Bradstreet alisema “uongozi bila hekima ni sawa na shoka zito lisilo na mpini.” Hapa alimaanisha kuwa, uongozi unahitaji hekima ili uweze kusimamia mambo kwa haki bila upendeleo.

SALA: Mungu Baba tunaomba Hekima yako katika kusimamia sheria tunazojiwekea.

Masomo ya Misa Machi 5

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu Machi 5


2024 MACHI 5 JUMANNE: JUMA 3 LA KWARESIMA
Mt. Yohane Yoseph wa Napoli 
Urujuani
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Kum 4: 1, 5-9

Musa aliwaambia makutano: ”Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo. Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako.   

Wimbo wa Katikati. Zab 147:12-13, 15-16, 19-20

1. Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapigo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako. (K)

(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.

2. Huipeleka amri yake juu ya nchi,
Neno lake lapiga mbio sana.
Ndiye atoaye theluji kama sufu,
Huimwaga barafu yake kama majivu. (K)

3. Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua. (K)

Injili. Mt 5: 17-19

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: ”Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.

TAFAKARI

SHERIA NA TARATIBU HUSAIDIA KURATIBISHA MAMBO: Katika jamii yoyote ile, zipo sheria, taratibu na miongozo ambayo husaidia jamii husika katika kuratibisha mambo. Hata katika imani yetu zipo, Amri za kutuelekeza. Masomo yote ya leo yanasisitiza umuhimu wa sheria. Musa katika somo la kwanza, aliwaasa wana wa Israel kuzingatia Amri za Mungu ili wasivurugwe na zile za jamii iliyokuwa inawazunguka na Yesu katika Injili anakazia kufundisha Amri katika usahihi wake. Katika jamii yetu ya leo tunaona jinsi baadhi ya watawala wanavyotunga sheria za kukandamiza wanyonge na kujinufaisha wao, mahali pengine ukweli unapindishwa kisa mwenye kosa ni tajiri au kiongozi. Kwenye kusimamia sheria inahitajika Hekima ya hali ya juu. Mwanasaikolojia Anne Bradstreet alisema “uongozi bila hekima ni sawa na shoka zito lisilo na mpini.” Hapa alimaanisha kuwa, uongozi unahitaji hekima ili uweze kusimamia mambo kwa haki bila upendeleo.

SALA: Mungu Baba tunaomba Hekima yako katika kusimamia sheria tunazojiwekea.

Masomo ya Misa Machi 4

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 04/03/2024

2024 MACHI 4 JUMATATU: JUMA 3 LA KWARESIMA
Mt. Kasmiri
Urujuani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. 2 Fal 5: 1-15

Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana  mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, ”Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.” Mtu mmoja akaingia, akamwambia bwana wake, akasema, ”Yule kijana mwanamke aliyetoka nchi ya Israeli asema hivi na hivi.” Mfalme wa Shamu akasema, ”Haya! basi, mimi nitampelekea mfalme wa Israeli waraka.” Basi, akaenda zake, akachukua mikononi mwake talanta kumi za fedha, na vipande vya dhahabu elfu sita, na mavazi kumi. Akampelekea mfalme wa Israeli waraka ule, kusema, ”Waraka huu utakapokuwasilia, tazama, nimemtuma mtumishi wangu Naamani kwako, ili upate kumponya ukoma wake.” Ikawa, mfalme wa Israeli alipousoma waraka, alirarua mavazi yake, akasema, ”Je, mimi ni Mungu, niue na kuhuisha, hata mtu huyu akanipelekea mtu nimponye ukoma wake? Fahamuni, basi, nakusihini, mwone ya kuwa mtu huyu anataka kugombana nami. Ikawa, Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, ”Mbona umeyararua mavazi yako?” Na aje sasa kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli. Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha. Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, ”Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia nawe utakuwa safi. Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, ”Tazama, nalidhania, ‘Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la Bwana, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma.’ Je, Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira. Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi?’ Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi, ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi. Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema,” Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli, basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako.”

Wimbo wa Katikati.Zab 42:2-3, 43:3-4

1. Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji.
Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu. (K)

(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai,
      Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu. 


2. Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai,
Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu? (K)

3. Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze,
Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu
Na hata maskani yako. (K)

4. Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu,
Kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu. (K)

Injili. Lk 4: 24-30

Yesu alifika Nazareti akawaambia makutano hekaluni: ”Amin, nawaambia ya kuwa, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe. Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu.”Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake.

TAFAKARI

DHARAU HUONDOA UTII: Tunashuhudia mara nyingi katika maisha, mtu anavyojaliwa kuwa na mali, akili au cheo/madaraka huota tabia ya dharau, kujiona, kujisikia na hivi kukosa utii. Naaman wa somo la kwanza alikuwa mtu mashuhuri lakini mgonjwa wa ukoma na alipoambiwa na Nabii akajichovye katika maji ili aweze kupona, alidharau na kuondoka kwa hasira, alitaka aponywe kwa jinsi alivyofikiri yeye. Kama sio wale watumishi wake waliomshauri angeishia kutopona. Dharau hizi hizi ndo tunaziona katika Injili, hawa makutano walijaa ghadhabu na kutaka kumdhuru Yesu baada ya kuwaeleza ukweli kuhusu mwenendo wao. Ulimwengu wa leo, watu wanyonge hawasikilizwi, hata wakitoa wazo la kujenga linapuuzwa. Tujifunze kujishusha na kukubali kuelekezwa, kukubali ushauri, tusijione au kujifanya wajuaji, tuelewe kuwa majigambo hutukosesha mengi.

SALA: Ee Yesu tujalie tukubali kushauriwa na kuacha madharau na kujikweza. Amina.