Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 01/03/2024
2024 MACHI 1 IJUMAA: JUMA 2 LA KWARESIMA
Mt. Switberti, Askofu
Urujuani
Zaburi: Juma 2
Somo 1. Mwa 37:3-4, 12-13, 17-28
Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, ”Je, Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo nikutume kwao.” Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, ”Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja! Haya, twende tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, ”Mnyama mkali amemla;” kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake! Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, ”Tusimwue.” Reubeni akawaambia, ”Msimwage damu; mtupeni katika birika hii iliyopo nyikani, wala msimguse;” ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula chakula. Wakainua macho yao, wakaona msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, ”Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? Haya na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yenu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu.” Ndugu zake wakakubali. Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.
Wimbo wa Katikati. Zab 105:16-21
1. Akaiita njaa iijilie nchi,
Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
Alimpeleka mtu mbele yao,
Yusufu aliuzwa utumwani. (K)
(K) Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.
2. Walimwumiza miguu yake kwa pingu,
Akatiwa katika minyororo ya chuma.
Hata wakati wa kuwadia neno lake,
Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)
3. Mfalme alituma watu akamfungua
Mkuu wa watu akamwachia.
Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,
Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)
Injili. Mt 21: 33-43; 45-46
Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa watu, ”Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza, wakawatenda vilevile. Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu.’ Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, ‘Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake.’ Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, ‘Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake.” Yesu akawaambia, ”Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake. Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata waliwaogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.
TAFAKARI
WIVU HAUJENGI: Daima maisha hukosa ladha hasa pale tunaposhindwa kufikiri kwa pamoja na kuamua yanayofanana. Tusipokubaliana kuwa na msemaji mmoja, mwisho tunajikuta tumegawanyika na kuishia hata kuwa na wivu. Somo la kwanza tumeona jinsi kaka zake na Yusufu walivyokuwa na wivu juu ya ndugu yao kwa sababu ya kupendwa zaidi na baba yao. Na katika Injili wale wakulima wanamwonea wivu mtoto wa bwana wao kisa ni mrithi. Jamii yetu ya leo imegubikwa na wivu unaozidi kuchanua kila uchwao. Watu wanasemana visivyo sehemu zao za kazi ili kuchafuliana na hii inapelekea hadi mtu kufukuzwa kazi, tunasahau kuwa kila mmoja ana bahati yake, hata vidole vya mikono havilingani. Wivu ni matokeo ya kutoridhika na haki yako au bahati yako, kupenda kuwa sawa na mwingine au kuwa zaidi.