Select Page

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 08/03/2024

2024 MACHI 8 IJUMAA: JUMA 3 LA KWARESIMA
Mt. Yohane wa Mungu, Mtawa
Urujuani
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Hos 14:2-10

Bwana asema: ”Ee Israeli, mrudie Bwana, Mungu wako; maana umeanguka kwa sababu ya uovu wako. Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Bwana; mkamwambie, ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo tutakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng’ombe. Ashuru hatatuokoa; hatutapanda farasi; wala hatutaiambia tena kazi ya mikono yetu, Ninyi ndinyi miungu yetu; maana kwako wewe wasio na baba hupata rehema. Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao; nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo; kwa maana hasira yangu imemwacha. Nitakuwa kama umande kwa Israeli; naye atachanua maua kama nyinyoro, na kueneza mizizi yake kama Lebanoni. Matawi yake yatatandaa, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake kama Lebanoni. Na wao wakaao chini ya uvuli wake watarejea; watafufuka kama ngano, na kuchanua maua kama mzabibu; harufu yake itakuwa kama harufu ya divai ya Lebanoni.” Efrahimu atasema, ”Mimi nina nini tena na sanamu? Mimi mimeitika, nami nitamwangalia. Mimi ni kama mberoshi wenye majani mabichi. Kwangu mimi yamepatikana matunda yako. Ni nani aliye na hekima, naye atayafahamu mambo haya? Ni nani aliye na busara, naye atayajua? Kwa maana njia za Bwana zimenyoka, nao wenye haki watakwenda katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake.

Wimbo wa Katikati. Zab 81:6-9, 10-11,14-17

1. Maneno yake nisiyemjua naliyasikia.
Nimelitenga bega lake na mzigo,
Mikono yake ikaachana na kikapu.
Katika shida uliniita nikakuokoa. (K)

(K) Mimi ndimi Bwana Mungu wako, Sikiliza sauti yangu.  

2. Nalikuitikia katika sitara ya radi;
Nalikujaribu penye maji ya Meriba.
Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya,
Enyi Israeli, kama ukitaka kunisikiliza. (K)

3. Usiwe na mungu mgeni ndani yako;
Wala usimsujudie mungu mwingine.
Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,
Niliyekupandisha toka inchi ya Misri. (K)

Injili. Mk 12:28-34

Mmojawapo wa waandishi alifika, akawasikia wakisemezana naye, akatambua ya kuwa amewajibu vema, akamwuliza, ”Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?” Yesu akamjibu, ”Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja. Nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Yule mwandishi akamwambia, ”Hakika, Mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye; na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhabihu zote pia.” Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, ”Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu.” Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo.

TAFAKARI

UPENDO NI KILELE CHA UTAKATIFU: Somo la Injili limetawaliwa na dhamira ya upendo, mwandishi aliyemuuliza Yesu swali alichokoza na hivi akaibua mjadala mzima uliogusia suala la upendo. Katika maisha yetu twaweza peana zawadi nyingi, lakini zawadi pekee yenye maana unayoweza kumpa mtu ni upendo. Paulo katika barua yake kwa Waefeso 4:2-3 anatuasa tuishi maisha ya unyenyekevu, upole na uvumilivu tukichukuliana katika upendo ndani ya Roho Mtakatifu. Anaelezea zaidi kwenye aya ya 15-16 kuwa, upendo huu utatusaidia kumfikia Kristo aliye kichwa chetu. Ni katika jibu alilotoa Kristo katika swali aliloulizwa kuwa, upendo ndio ukamilifu wa yote. Ulimwengu umechafuka kutokana na kukosa upendo wa dhati, watu wanaishi upendo geresha, upendo danganya toto, watu wanatamkiana tu neno upendo lakini kiuhalisia hakuna upendo wowote.

SALA: Bwana Yesu tujalie mioyo yetu iweze kuwa chemchemi ya upendo kwa wote.