Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa 06/03/2024

2024 MACHI 5 JUMANNE: JUMA 3 LA KWARESIMA
Mt. Koleta wa Corbie Bikira na Mtawa 
Urujuani
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Kum 4: 1, 5-9

Musa aliwaambia makutano: ”Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo. Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako.   

Wimbo wa Katikati. Zab 147:12-13, 15-16, 19-20

1. Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapigo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako. (K)

(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.

2. Huipeleka amri yake juu ya nchi,
Neno lake lapiga mbio sana.
Ndiye atoaye theluji kama sufu,
Huimwaga barafu yake kama majivu. (K)

3. Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua. (K)

Injili. Mt 5: 17-19

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: ”Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.

TAFAKARI

SHERIA NA TARATIBU HUSAIDIA KURATIBISHA MAMBO: Katika jamii yoyote ile, zipo sheria, taratibu na miongozo ambayo husaidia jamii husika katika kuratibisha mambo. Hata katika imani yetu zipo, Amri za kutuelekeza. Masomo yote ya leo yanasisitiza umuhimu wa sheria. Musa katika somo la kwanza, aliwaasa wana wa Israel kuzingatia Amri za Mungu ili wasivurugwe na zile za jamii iliyokuwa inawazunguka na Yesu katika Injili anakazia kufundisha Amri katika usahihi wake. Katika jamii yetu ya leo tunaona jinsi baadhi ya watawala wanavyotunga sheria za kukandamiza wanyonge na kujinufaisha wao, mahali pengine ukweli unapindishwa kisa mwenye kosa ni tajiri au kiongozi. Kwenye kusimamia sheria inahitajika Hekima ya hali ya juu. Mwanasaikolojia Anne Bradstreet alisema “uongozi bila hekima ni sawa na shoka zito lisilo na mpini.” Hapa alimaanisha kuwa, uongozi unahitaji hekima ili uweze kusimamia mambo kwa haki bila upendeleo.

SALA: Mungu Baba tunaomba Hekima yako katika kusimamia sheria tunazojiwekea.