Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 07/03/2024
2024 MACHI 7 ALHAMISI: JUMA 3 LA KWARESIMA
Wat. Perpetua na Felisita, Mashahidi
Urujuani
Zaburi: Juma 3
Somo 1. Yer 7:23-28
Naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru, mpate kufanikiwa. Lakini hawakusikiliza, wala kutega sikio lao, bali walikwenda kwa mashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele. Tokea siku ile baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu ninyi, nikiamka mapema kila siku, na kuwatuma. Lakini hawakunisikiliza, wala kutega sikio lao; bali walifanya shingo yao kuwa ngumu; walitenda mabaya kuliko baba zao. Nawe utawaambia maneno hayo yote; lakini hawatakusikiliza; nawe utawaita; lakini hawatakuitikia. Nawe utawaambia, Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali na vinywa vyao.
Wimbo wa Katikati. Zab 95:1-2, 6-9
1. Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu.
2. Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)
3. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba,
Kama siku ya Masa jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)
Injili. Lk 11: 14-23
Yesu alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu. Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli. Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake. Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.
TAFAKARI
UKAIDI HUSABABISHA KUKOSA MENGI: Katika somo la kwanza, Nabii anajitahidi kuwaasa wanajamii husika lakini wanakuwa wakaidi. Yesu naye katika Injili anawaasa makutano lakini hawakubali na badala yake wanamsingizia uongo kuwa anatumia nguvu za giza. Yote haya yanasababishwa na ukaidi, kutokujikubali. Kuna watu ukiwashauri jambo tena la manufaa kwao, hawapokei ushauri, badala yake wanaanza kukuchambua wewe unayemshauri. Nilishashuhudia padre alimshauri mwanandoa ili aishi vyema kiapo chake cha ndoa kwa vile ilikuwa inavunjika, lakini matokeo yake yule mwanandoa alimjibu padre kuwa huwezi kunishauri kwani wewe (padre) hujaoa na hujui changamoto za ndoa. Hii inatokana na ukweli kuwa, alitaka kusimamia msimamo wake ambao haukuwa sahihi. Ndivyo ilivyokuwa hata kwa hawa wahusika wa Injili, walitaka kubaki katika msimamo wao na sio kupokea hii Huruma ya Mungu.
SALA: Tunakuomba Ee Yesu mwema, utupe moyo wa unyenyekevu na kujikubali.