Masomo ya Misa Oktoba 7

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 07/10/2024

2024 OKTOBA 7: JUMATATU-JUMA LA 27 LA MWAKA

Bikira Maria Mt. Mama wa Rozari
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Juma III

SOMO 1. Gal 1:6-12

Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe. Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo. Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 111:1-2, 7-10

1. Aleluya.
Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
Matendo ya Bwana ni makuu,
Ukawafunulia watoto wachanga.

(K) Alikumbuka agano lake milele.

2. Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu,
Maagizo yake yote ni amini.
Yamethibitika milele na milele,
Yamefanywa katika kweli na adili. (K)

3. Amewapelekea watu wake ukombozi,
Ameamuru agano lake liwe la milele.
Jina lake ni takatifu la kuogopwa.
Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima,
Wote wafanyao hayo wana akili njema,
Sifa zake zakaa milele. (K)      

INJILI. Lk 10:25-37

Mwana-sheria mmoja alisimama akamjaribu Yesu, akisema, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Akamwambia, “Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?” Akajibu akasema, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.” Akamwambia, “Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi.” Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, “Na jirani yangu ni nani?” Yesu akajibu akasema, “Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipitia kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapitia kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, ‘Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.’ Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake, yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi?” Akasema, “Ni huyo aliyemwonea huruma.” Yesu akamwambia, “Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.”

TAFAKARI

UPENDO USIO NA UBAGUZI: Katika masimulizi, Msamaria mwema alikuwa mkarimu sana, na Yesu anaonesha kile alichokifanya katika kutoa msaada kwa yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi. Ukarimu unaotokana na Mungu na ni zaidi ya kumpikia mtu chakula. Ni wema ambao unawasha mishumaa kusudi wengine waweze kuona. Ni wema ambao unawaombea wengine neema, unaoomba baraka za Mwenyezi Mungu kwa kila mtu yaani kwa wale walio wema na wasio wema pia. Wale wanaotupenda na wasio tupenda. Ukarimu unaotokana na Mungu sio tu unawapatia wengine chakula, bali pia unawavuta wengine katika mazungumzo ya furaha na amani. Jiongeze. Ikiwa unaona kwamba kuna kazi inapaswa kufanyika, nenda kafanye. Fanya kazi ili kuonesha wengine jinsi Mungu anavyokutendea wewe. Fanya kwa furaha ambayo Mungu ameiweka moyoni mwako na wala sio kwa manung’uniko. Yesu akamwambia, na anatuambia mimi na wewe “Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.”

SALA: Ee Mungu utujalie tuwe watu wema na wakarimu kwa kila tunayekutana naye.

Masomo ya Misa Dominika ya 27

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 06/10/2024

2024 OKTOBA 6: DOMINIKA YA 27 YA MWAKA

Rangi: Kijani
Zaburi: Juma III

SOMO 1. Mwa 2:18 – 24

Bwana Mungu alisema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanya msaidizi wa kufanana naye. Bwana Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamleta Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake. Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 128

1. Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika njia yake.
Taabu ya mikono yako hakika utaila,
Utakuwa mwenye heri na baraka tele.

(K) Bwana atubariki siku zote za maisha yetu.

2. Mke atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni,
Wakizunguka meza yako. (K)

3. Hakika, atabarikiwa hivyo,
Yule amchaye Bwana.
Bwana akubariki toka Sayuni,
Uone uheri ya Yerusalemu siku zote za maisha yako;
Naam, ukawaone wana wa wanao.
Amani ikae na Israeli. (K)

SOMO 2. Ebr 2: 9-11

Ndugu, twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wakovu wao kwa njia ya mateso. Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake.

INJILI. Mk 10: 2-16

Mafarisayo walimwendea Yesu, wakamwuliza, Je, ni halali mtu kumwacha mkewe? huku wakimjaribu. Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini? Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha. Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja, hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu mwanadamu asikitenganishe. Hata nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo. Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine azini.  Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.

TAFAKARI

TUNAUNGANIKA KWA MPANGO WA MUNGU WALA SI BINADAMU
Mwanadamu katika asili yake ni mjamii. Yeye ameumbwa kuwa na mahusiano na watu wengine kwa kusaidiana na kushirikisha mema mbalimbali kadiri ya majaaliwa ya mwenyezi Mungu. Tunu hii ya mahusiano inamdai mmoja kujifungua na kutambua uwepo wa mwenzake aliyeko pembeni yake na hivyo kushikamana naye. Namna hii ndiyo inamtambulisha mwanadamu. Mmoja akionekana katika jamii ngeni wenyeji lazima wataanza kuulizia na kuchunguza asili yake; anatokea wapi, jamaa yake ni ya namna gani na mengineyo mengi. Mwishoni jamii hiyo itafanya bidii kuunganishwa na jamii husika ili kushiriki pamoja na wanajamii wengine. Katika mahusiano haya ya kibinadamu watu hutengeneza jumuiya au vikundi vidogo vidogo kuanzia na urafiki, uchumba, familia, ukoo na hata kabila. Namna hizi zote za kuhusiana zinapata asili yake katika haiba hiyo ya kutoka nje na kuunganika na mtu mwingine.
Masomo ya Dominika hii yanaelezea zaidi tunu ya ndoa ambayo ni zao la mahusiano ya kibinadamu. Tunu hii hutengeneza familia ambayo mama Kanisa anaiita kama kitalu cha mahusiano yote ya kibinadamu. Ndani mwake mmoja hufundishwa mahusinao na wengine: kwanza kama mtoto ndani ya familia ikimaanisha wapo anaohusiana nao kama wazazi wake. Hawezi kujiona yu asili yake mwenyewe. Wapo waliomzaa na kumleta duniani. Namna ya pili mtoto hujifunza kuwa na ndugu zake wanaozaliwa pamoja naye. Hivyo kuanza kujifunza kutengeneza mahusiano ya kindugu na kushirikiana kindugu. Mwishoni mtoto huyo anajifunza kuanza kuhusiana na jamaa zake wengine, asili ya wazazi wake na hivyo kujikuta anakomaa katika kujitoa, kujifungua nafsi yake na kushirikiana na watu wengine.
Mama Kanisa Mtakatifu sana anatupatia mafundisho mahususi ya tabia muhimu za ndoa ya kikristo. Ni mahusiano ya watu wawili, mwanamke na mwanamme wanaoamua kukaa pamoja na kushirikishana upendo na pia kushiriki katika kazi ya uumbaji (Rejea Sheria za Kanisa, kan. 1052). Sheria hizo zinaendelea kuelezea kuwa ni mahusianao ya mme na mke mmoja na mahusiano yasiyogawanyika. Yaani ni uhusiano wa kudumu. Baba Mtakatifu Fransisko anakaza kufundisha kwamba huku kutokugawanyika kwa ndoa kusichukuliwe kama nira au kifungo cha adhabu “bali ni zawadi wanayopewa wale wanaofunga ndoa… upendo wa Mungu daima huwasindikiza katika safari yao kama wanadamu; kwa njia ya neema, hutuponywa na kuibadili mioyo migumu na kuwarejesha tena mwanzo kwa njia ya msalaba” (Furaha ya Upendo au Amoris Laetitia, n. 62).
Fundisho hili juu ya kutokugawanyika kwa ndoa linapata msingi wake katika Injili ya dominika hii. Kristo anaonesha ni upi uliokuwa mpango wa Mungu tangu mwanzo kama ilivyooneshwa katika kitabu cha Mwanzo. Ilikuwa ni mwanamke na mwanamme kuachana na familia zao na kuungana na kuwa kitu kimoja. Kitendo cha mwenyezi Mungu kuutoa ubavu wa Adamu alisisitiza huo muunganiko wao wa ndani. Na Kristo katika Injili amesakafika kwamba: “Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe” Hivyo ni katazo ambalo linanuia kutuepusha na sababu yoyote ya kibinadamu kwa ajili ya kutenganisha ndoa. Hii inamaanisha kuwa inapofanyika ndoa takatifu anayeunganisha ni Mungu. Ni Yeye ambaye anaturudisha tena pale bustani Eden na kuwaunganisha wawili wanaofunga ndoa.
Tukirudi katika Injili tunaweza kutafakari zaidi swali la Yesu juu ya sheria ya Musa. Kimsingi swali hili lilinuia kuweka wazi tofauti kati ya Sheria ya Mungu na ile ya mwanadamu. Tangu mwanzo wakati wa uumbaji mpango wa Mungu ulikuwa ni udumifu wa agano la ndoa. Ugumu wa mioyo wa wanadamu, matunda ya dhambi umeharibu mpango huu. Hivyo sheria inayowekwa na Musa haijatoka katika mpango wa Mungu wa tangu awali. Ililenga tu katika ugumu wa mioyo. Mpango wa Mungu tangu mwanzo kama ilivyoelezwa katika Somo la Kwanza ni kumhusisha mwanamme na mwanamke. Lilikuwa ni jibu la kuondoa ushabiki wa kifarisayo ambao kwa upande mwingine uliondoa uhuru wa mwanamke na kumgeuza kama chombo tu na siyo mwanadamu anayeshirikishwa katika muungano wa ndoa. Hapa ndipo tunauona msingi wa ndoa takatifu: Ni watu wawili walio sawa wanaoungana na siyo mwanamme anayemchukua mwanamke na akipenda atamuacha. Wote wawili wanatajirishana katika kushirikishana vipawa vyao.
Msingi huo unatusukuma kulitafakari somo la pili la Dominika hii ambalo linatuonesha jinsi binadamu wote tunavyofanyika ndugu katika Kristo. Kwa neema ya Mungu Kristo “ameionja mauti kwa ajili ya kila mtu” Kwa njia ya mauti yake ametukomboa wanadamu wote na kuturudishia uzima wa kimungu. Kwa namna hii ametufanya kuwa wana wa Mungu. Ndiyo “maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa maana hii haoni haya kuwaita ndugu zake”. Huu ndiyo msingi wa uhusiano wetu kama Wakristo, yaani kuwa wana wa Mungu katika Kristo. Katika msingi huu ndipo yanapochipuka mahusiano yote ya kibinadamu. Mahusiano haya kama wana mbele ya Baba yanamfanya Yeye kuwa asili yetu na hivyo kuwa katikati yetu katika mahusiano yetu ya kibinadamu.
Familia ya kikristo inajengwa katika msingi huu. Ndoa takatifu inawaunganisha wawili ambao ni wana wa Mungu na wanachota msingi wa muungano wao katika Mungu. Nje ya mpango huu tunaigeuza ndoa kuwa ni shughuli ya kibinadamu na inakosa misingi ya kimungu. Inakosa msaada wa kimungu, yaani neema zake ambazo kama tulivyonukuu hapo juu kutoka barua ya Amoris Laetitia, neema hiyo huwasindikiza wanandoa, huwaponya na kuibadili mioyo yao migumu. Neema hiyo inawaondoa katika maelekeo na matamanio ya kibinadamu. Mtume Paulo anatufundisha msingi huo wa kikristo akisema: “hali mmenyenyekeana katika kicho cha Kristo. Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu… enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake” (Ef e 5:21,22 na 25).

Masomo ya Misa Oktoba 5

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 05/10/2024

2024 OKTOBA 5: JUMAMOSI-JUMA LA 26 LA MWAKA

Mt. Faustina Kowalska, Bikira
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma II

SOMO 1. Ayu 42: 1-3, 5-6, 12-17

Ayubu alimjibu Bwana na kusema, najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika. Ni nani huyu afichaye mashauri bila maarifa? Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua. Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; bali sasa jicho langu linakuona. Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu katika mavumbi na majivu. “Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng’ombe elfu, na punda wake elfu. Tena alikuwa na wana waume saba, na binti watatu. Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na wa pili akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu. Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wana waume. Kisha baada ya mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia na arobaini, naye akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hata vizazi vinne. Basi Ayubu akafa, mzee sana mwenye kujawa na siku.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 119: 66, 71, 75, 91, 125, 130

1. Unifundishe akili na maarifa,
Maana nimeyaamini maagizo yako.
Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa,
Nipate kujifunza amri zako.

(K) “Umwangazie mtumishi wako uso wako,
Ee Bwana.

2. Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki,
Ee Bwana, na kwa uaminifu umenitesa.
Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo,
Maana vitu vyote ni watumishi wako. (K)

3. Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe,
Nipate kuzijua shuhuda zako.
Kunifafanisha maneno yako kwatia nuru,
Na kumfahamisha mjinga. (K)

INJILI. Lk 10:17-24

Wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, “Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako.” Akawaambia, “Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.” Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza.” Akasema, “Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.” Akawageukia wanafunzi wake, akasema nao kwa faragha, “Heri macho yaonayo mnayoyaona ninyi. Kwa kuwa nawaambia ya kwamba manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi wasiyasikie.”

TAFAKARI

ETI KWA SABABU: Katika yote tunayotenda na tuliyotenda, cha muhimu ni kwamba tumefanya kwa sababu imetupasa kufanya, hatuhitaji zawadi. Wanafunzi wanasoma kwa bidii kusudi wapate matokeo mazuri. Wafanyakazi wanafanya kazi hadi muda wa ziada kusudi wapate mshahara zaidi. Wafuasi wanamtumikia Mungu kusudi wapate kitu gani? Biblia inatuambia kwamba wafuasi wanapaswa kupiga hatua mbele zaidi kwa sababu wanampenda Mungu, na wanadamu, wanatimiza ahadi, wanamwabudu Mungu na kuwahubiria wengine kuhusu Yesu. Katika jitihada zako kwa ajili ya Kristo, mshukuru Mungu kwa sababu unayo ahadi ya maisha ya umilele. Sababu ya msingi iliyopelekea kumjua Mungu ni kwa sababu Mungu amekuchagu upate kumjua. Na kwa nini Mungu amefanya hivyo? Ni kwa sababu ya neema, zawadi ambayo tunaipata bure kwa upendo wake. Unapaswa kufanya nini basi? Mshukuru Mungu katika sala, ishi kwa ajili ya Mungu, zungumza mambo yamuhusuyo Mungu, na waoneshe wengine upendo wa Mungu. Zawadi kubwa anayopokea mtu huendana na kutoa shukrani kubwa.

SALA: Ee Mungu tunakushukuru kwa kutuchagua; utujalie furaha ya kweli.

Masomo ya Misa Oktoba 4

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 04/10/2024

2024 OKTOBA 4: IJUMAA-JUMA LA 26 LA MWAKA

Fransisko wa Asizi
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Juma II

SOMO 1. Ayu 38:1, 12-21, 40:3-5

Ndipo Bwana alimjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake? Yapate kuishika miisho ya nchi, waovu wakung’utwe wakawe mbali nayo? Hubadilika mfano wa udongo chini ya muhuri, vitu vyote vinatokea kama mavazi. Na waovu nuru yao huzuiliwa isiwafikie, na mkono ulioinuka huvunjika. Je! Umeziingia chemchemi za bahari, au umetembea mahali pa siri pa vilindi? Je! Umefunuliwa malango ya mauti, au umeyaona malango ya kuzimu? Umeyafahamu mapana ya dunia? Haya! Sema, ikiwa unayajua hayo yote. “Iko wapi njia ya kuyafikia makao ya nuru? Na giza pia, mahali pake ni wapi? Upate kuipeleka hata mpaka wake, upate kuelewa na mapito ya kuiendea nyumba yake? Hukosi unajua, maana ulizaliwa wakati huo, na hesabu ya siku zako ni kubwa! Ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema, Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu. Nimenena mara moja, nami sitajibu; naam, nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi.”

WIMBO WA KATIKATI. Zab 139:1-3, 7-10, 13-14

1. Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.

(K) Uniongoze Bwana, katika njia ya milele.

2. Niende wapi nijiepushe na roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko;
Ningefanya kuzimu kitanda change, Wewe uko. (K)

3. Ningezitwaa mbawa za asubuhi,
Na kukaa pande za mwisho za bahari;
Huko nako mkono wako utaniongoza,
Na mkono wako wa kuume utanishika. (K)

4. Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
Uliniumba tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. (K)

INJILI. Lk 10: 13-16

Yesu aliwaambia wafuasi wake: “Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu. Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu. Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”

TAFAKARI

WITO WA KUSIKILIZA: Ikiwa heshima huwaendea madaktari na wakufunzi. Ikiwa utajiri, mali na mafanikio huwaendea wakurugenzi na wanasheria, ikiwa umaarufu huwaendea wanamichezo, wanamuziki, waigizaji wanaogonga vichwa vya habari, je! Waandishi wa Injili wanapata kitu gani? Wao wanapata ujumbe ambao unawapatia uzima wa milele. Lakini kama wainjili hao watakataa kuupeleka ujumbe huo wa Habari njema kwa wengine watatengwa milele na Mungu. Ikiwa kuna kazi ya muhimu ambayo inatakikana kufanyika kwa njia au kwa gharama yoyote ile, basi inapaswa ifanywe kwa namna tofauti, kwa weledi na kipekee kabisa. Fursa na wajibu wetu sisi tulio wafuasi wake ni kutangaza Habari njema. “Yesu aliwaambia wafuasi wake: “Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu.” Na kwa maneno ya Paulo mtume; “Ole wangu kama nisipohubiri Injili.”

SALA: Bwana Yesu utujalie fadhila ya kuwasikiliza unaowatuma kwenu.

Masomo ya Misa Oktoba 3

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 03/10/2024

2024 OKTOBA 3: ALHAMISI-JUMA LA 26 LA MWAKA

Wat. Ndugu Ewaldi, Wafiadini
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma II

SOMO 1. Ayu 19:21-27

Ayubu alisema: “Nihurumieni, nihurumieni, enyi rafiki zangu, kwa maana mkono wa Mungu umenigusa. Mbona ninyi mnaniudhi kama Mungu, wala hamkutosheka na nyama yangu? Laiti maneno yangu yangeandikwa sasa! Laiti yangeandikwa kitabuni! Yakachorwa katika mwamba milele, kwa kalamu ya chuma na risasi. “Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; nami nitamwona mimi nafsi yangu, na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine. 

WIMBO WA KATIKATI. Zab 27:7-9, 13-14

1. Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu ninalia,
Unifadhili, unijibu.
Uliposema, nitafuteni uso wangu,
Moyo wangu umekuambia,
Bwana, uso wako nitautafuta.

(K) “Naamini ya kuwa nitauona wema wa
Bwana katika nchi ya walio hai. “

2. Usinifiche uso wako,
Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira.
Umekuwa msaada wangu, usinitupe,
Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. (K)

3. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)

INJILI. Lk 10:1-12

Bwana aliweka wafuasi wengine, sabini na wawili, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni; angalieni, nawatuma kama wanakondoo kati ya mbwamwitu. Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie mtu njiani. Na nyumba yo yote mtakayoingia, semeni kwanza, ‘Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihamehame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii. Na mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapozeni wagonjwa waliomo, waambieni, “Ufalme wa Mungu umewakaribia. Na mji wo wote mtakaouingia, nao hawawakaribishi, tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni, ‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana na miguu yetu tunayakung’uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia.’ Nawaambia ya kwamba siku ile itakuwa rahisi zaidi Sodoma kuistahimili adhabu yake kuliko mji huo.

TAFAKARI

SISI SOTE NI WAMISIONARI: Wakati wengi kati ya wafuasi wakibaki nyuma, wale sabini na wawili walikwenda kumuandalia Yesu mahali atakapotembelea katika miji kadhaa. Ilikuwa ni zamu yao kufanya umisionari na kwa kweli furaha yao ilikuwa kubwa sana. Lakini jambo la muhimu ni kwamba katika kuenenda kwao walikwenda kwa nguvu na ujumbe wa Mungu. Popote tunapokwenda kufanya jambo fulali tuanze na sala, tumtumainie Mungu na uwasaidie watu kumpata mkombozi wao. Yesu anawatia moyo wafuasi kwamba sio tu wakafanye kazi waliyotumwa, bali wasali kuomba wafanyakazi zaidi. Pasipo kujali wajibu wako, sali leo kwa ajili ya watendakazi wengi zaidi. Waamini siku zote hatupaswi kufanya kazi peke peke, Mungu anataka tusali, na tuwafundishe wengine na kuwawezesha kujiunga nao wanapotafuta fursa ya kumtumikia Yesu. Watu wengine mara tu wanapoelewa injili wanataka mara moja kwenda na kuwaongoa watu. Yesu anawapatia namna tofauti kabisa; wanapaswa kuwakusanya watu na kuwafundisha kusali, na kabla ya kusali kuwaombea wale ambao hawajaongoka.

SALA: Mungu mwenyezi tunawaombea wamisionari na wote wanaolitangaza Neno lako wasikate tamaa hata maramoja.