Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 25/04/2024
2024 APRILI 25 : ALHAMISI-JUMA LA NNE LA PASAKA
MT. MARKO, MWINJILI
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Juma 4
Somo 1. 1Pet 5:5-14
Ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu. Uweza una yeye hata milele na milele. Amina. Kwa mkono wa Silwano, ndugu mwaminifu kama nionavyo, nimewaandikia kwa maneno machache, kuonya na kushuhudia ya kuwa hii ndiyo neema ya kweli ya Mungu. Simameni imara katika hiyo. Mwenzenu mteule hapa Babeli awasalimu, na Marko mwanangu. Salimianeni kwa busu la upendo. Amani na iwe kwenu nyote, mlio katika Kristo. Amina.
(K). Fadhili zako nitaziimba milele, Ee Bwana. |
Wimbo wa Katikati. Zab 89:2-3, 6-7, 16 -17
“1. Fadhili za Bwana nitaziimba milele;
Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. (K)
2. Ee Bwana, mbingu zitayasifu maajabu yako,
Uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu.
Maani ni nani katika mbingu awezaye kulinganishwa na Bwana?
Ni nani afananaye na Bwana miongoni mwa alaika? (K)
3. Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe,
Ee Bwana, huenenda katika nuru ya uso wako.
Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa,
Na kwa haki yako hutukuzwa. (K)”
Injili. Mk 16:15-20
Yesu aliwaambia wale Kumi na mmoja, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya. Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.
TAFAKARI
TUMEBATIZWA NA TUMETUMWA: Leo Kanisa linasherehekea sikukuu ya Marko Mwinjili. Tunaelezwa kuwa huyu aliandamana sana na Barnabas, Paulo na Petro na hata Injili aliyoandika imegusia kwa kiasi kikubwa mafundisho ya Petro. Alichangia kwa kiasi kikubwa kukuza imani ya Waamini wa Kanisa la mwanzo hasa barani Afrika. Alivaa moyo wa unyenyekevu kama somo la kwanza lilivyotuambia, ambao ulimfanya kuwa tayari kujisadaka, aliweza kumpinga adui wa imani yetu kwa kuwa imara na thabiti katika imani. Kwa kufanya hivi alitimiza hili analosema Yesu katika Injili, “enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.” Kristo anatualika nasi leo hii tuendeleze utume huu wa kuitangaza Injili yake kwa watu wote. Ziko namna nyingi za kutangaza Injili kama kujitolea kwa ajili ya ujenzi wa makanisa, kusali, kusoma na kutafakari Neno la Mungu, kujiunga katika vyama vya kitume, kuishi maisha maadili, kutoa malezi kwa watoto na vijana, n.k.
SALA: Ee Mungu utupe neema ya kuwa wamisionari wa Neno lako. |