Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 24/04/2024

2024 APRILI 24 : JUMATATU-JUMA LA NNE LA PASAKA

Mt. Fideli wa Stigmaringen, Padre na Shahidi
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 4

Somo 1. Mdo 12:24, 13:5

Siku zile, neno la Bwana likazidi na kuenea. Na Barnaba na Sauli, walipokwisha kutimiza huduma yao, wakarejea kutoka Yerusalemu, wakamchukua pamoja nao Yohane aitwaye Marko. Na huko Antiokia katika Kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao. Basi watu hao, wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu wakatelemkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro. Na walipokuwa katika Salami wakalihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Mayahudi.

Wimbo wa Katikati. Zab 67:2-3, 5-6, 8

“1. Mungu na atufadhili na kutubariki,
Na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulike duniani,
Wokovu wake katikati ya mataifa yote. (K)

2. Mataifa na washangilie,
Naam, waimbe kwa furaha,
Maana kwa haki utawahukumu watu,
Na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K)

3. Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru.
Mungu atatubariki sisi;
Miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K) “

(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu, Watu wote na wakushukuru.  

Injili. Yn 12:44-50

Siku ile Yesu alipaza sauti, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka. Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka. Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani. Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho. Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.

SALA: Tunakuomba ewe Roho Mtakatifu utuwezeshe kuwa wasikivu kwa Kristo.

TAFAKARI

KAZI YA MUNGU LAZIMA ITENDEKE: Yesu anatualika tumsikie yeye na tutekeleze yale anayotuambia vinginevyo hali yetu mbeleni hatutabaki salama. Anataka kila mmoja wetu kazi ambayo kwayo Mungu alimuumba aitekeleze. Anatueleza kuwa maneno aliyotuambia ni kutoka kwa Baba yake na sio yake. Maneno haya ndiyo yaliyowapa nguvu mitume kokote walikotawanyikia, (rej. somo 1), “siku zile Neno la Bwana likazidi na kuenea…na Barnaba na Sauli wakatengwa kwa kazi ile waliyoitiwa.” Hapa tunaona jinsi mitume walivyohangaika kuhakikisha kuwa utume wa Kanisa unaendelea. Mtume Paulo anaeleza tabia za mtu anayeendeleza kazi hii ya kusambaza Neno la Mungu kwamba “awe mtu asiyeshtakiwa kwa neno, asijipendekeze, asitafute maslahi binafsi, asipende mapato ya aibu, awe mkaribishaji, mpenda mema, mwenye kiasi…” (Tit 1:7-9). Hivi ni vielelezo vya kumsaidia mtu katika utume na anajikuta anautekeleza vyema, na hii itamsaidia kuwa msikivu kwa sauti ya Kristo anayetuhabarisha habari toka kwa Baba yake wa mbinguni.