Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 26/04/2024

2024 APRILI 26 : IJUMAA-JUMA LA NNE LA PASAKA

Mt. Kleti, Papa na Mfiadini
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 4

Somo 1. Mdo 13:26-33

Paulo alisimama akawapungia mkono, akasema: ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa. Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu. Na ijapokuwa hawakuona sababu ya kumfisha wakamwomba Pilato auawe. Hata alipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamtelemsha katika ule mti, wakamweka kaburini. Lakini Mungu akamfufua katika wafu; akaonekana siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hata Yerusalemu, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu. Na sisi tunawahubiri Habari Njema ya ahadi ile waliyopewa mababa, ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu kama ilivyoandikwa katika zaburi ya pili, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa.

Wimbo wa Katikati. Zab 2:6-11

“1. Nami nimemweka mfalme wangu
Juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu
Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia
Ndiwe mwanangu, mimi leo nimekuzaa. (K)

K) Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuza

2. Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako,
Na miisho ya dunia kuwa milki yako.
Utawaponda kwa fimbo ya chuma,
Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. (K)

3. Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili,
Enyi waamuzi wa dunia, mwadibiwe.
Mtumikieni Bwana kwa kicho,
Shangilieni kwa kutetemeka. (K)

Injili. Yn 14:1-6

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia, maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi muwepo. Nami niendako mwaijua njia. Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.

TAFAKARI

YESU NI NJIA YETU HALISI: Padre mmoja mgeni alipotea njia. Akawaambia watoto “Nionesheni njia ya kwenda parokiani, nami niwaoneshe njia ya kwenda mbinguni.” Mtoto mmoja akamjibu “Wewe hujui njia ya kwenda parokiani utawezaje kuijua njia ya kwenda mbinguni?” Yesu akiwa njia maana yake ni kwamba ili kufika mbinguni hatuna budi kumfuata Yeye. Amfuataye Yesu hapotei bali hufika anakoelekea, mbinguni. Tukimfuata Yesu hatuhitaji kumuuliza mtu yeyote tunakoelekea. Lengo la kumfuata Yesu aliye njia ni ili atujulishe ukweli kwani Yeye ndiye kweli halisi. Walimu hufundisha ukweli wakati wao sio ukweli. Lakini Yesu si tu kwamba hufundisha ukweli bali Yeye ni kweli yenyewe. Yesu ni njia ielekezayo kwenye uzima. Je, wataka kufika kwa Baba? Usitafute njia kwani Yesu ni njia. Je, wataka kujifunza na kuujua ukweli, Yesu ndiye kweli yenyewe. Je, wataka kuupata uzima? Ukimpata Yesu umeupata uzima. Wakati huu wa Pasaka hatuna budi kusikia sauti ya Yesu asemaye “Mimi ndimi njia, na kweli na uzima. Mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi”(Yoh 14:6).

SALA: Ee Yesu uliye njia yetu halisi, utujalie tukufuate wewe daima.