Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 21/04/2024
2024 APRILI 21 : DOMINIKA YA NNE YA PASAKA
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 4
Somo 1. Mdo 4:8-12
Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, aliwaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.
(K) Jiwe walilokataa waashi, Limekuwa jiwe kuu pembeni. |
Wimbo wa Katikati. Zab 118: 1,8-9, 21-23, 26, 28,29
“1. Aleluya.
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni Mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Ni heri kumkimbilia Bwana
Kuliko kuwatumainia wanadamu
Ni heri kumkimbilia Bwana
Kuliko kuwatumainia wakuu. (K)
2. Nitakushukuru kwa maana umenijibu,
Nawe umekuwa wokovu wangu.
Jiwe walilolikataa waashi
Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu. (K)
3. Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana;
Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana.
Ndiwe Mungu wangu, nami nitakushukuru,
Ndiwe Mungu wangu, nami nitakutukuza.
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele. (K)”
Somo 2. 1 Yoh 3:1-2
Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.
Injili. Yn 10: 11-18
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mimi ndimi mchungaji mwema, Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwamwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwamwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake. Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya Kondoo. Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.
TAFAKARI
“KRISTO MCHUNGAJI MWEMA: KIELELEZO CHA KUITIKIA WITO
Leo ni Dominika ya Kristo Mchungaji Mwema ambapo mama Kanisa anatualika kuiombea miito mitakatifu. Wito wowote ni matokeo ya ndoto anayokuwa nayo mtu katika maisha yake; jambo gani ambalo ana hamu nalo. Katika maisha ya Mtakatifu Yosefu tunaona jinsi ambavyo ndoto zetu zinaundwa katika Mungu na hivyo kumwezesha mmoja kutimiza kile ambacho ni kweli mpango wa Mungu kwake. Hili linahitaji utayari na kuweka maisha ya mmoja rehani. Kuwa tayari kuacha kujisikiliza na kumapatia Mungu nafasi aseme na wewe.
Katika somo la kwanza Mchungaji Mwema aliye msingi na chemchemi ya miito yote amejionesha kama jiwe kuu la pembeni. Hii inamaanisha kwamba ni yeye anayeshikilia uimara wa kundi lake; kwa mafundisho yake, kwa uponyaji wake na kwa kuwamiminia neema kutoka mbinguni. Hivyo daima yupo na kundi lake na kukosekana kwake ni sawa na maangamizi kwa kundi. Ingawa alidharaulika na watu wa ulimwengu, wakiwakilishwa na Wayahudi lakini yeye ambaye ni “Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.” Mchungaji ambaye ni wa kuajiriwa “kondoo si mali yake…huwaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya.” Mchungaji mwema kondoo ni mali yake. Daima anakaa nao kama jiwe kuu la pembeni na ni msingi wake imara.
Huduma na utumishi wetu kwa wenzetu inapata ufanisi pale tunapoona kuwa tukifanyacho ni sehemu muhimu si kwa uwepo wangu au si sehemu muhimu kwa uhai wangu tu bali hata kwa wale ninaowahudumia; pale tutakapoweza kubadili mawazo ya kutumia nafasi mbalimbali tulizonazo kwa ajili ya kujinufaisha binafsi na hivyo kutafuta kujinufaisha wote. Ni hali ya kuwa tayari kujifunua na kuwaangalia wengine walio pembeni yangu; hali ya kuona kuwajibika kwa mwenzangu kwa sababu yu sehemu muhimu na anayeleta maana ya uwepo wangu. Ni hatua muhimu kuelekea undugu wa kikristo ambao Kristo anakuwa kwetu ndugu yetu wa kwanza na katika yeye sote tunafanywa kuwa ndugu.
Mtume Yohane katika somo la pili anatupeleka hatua moja mbele. Kristo Mchungaji Mwema aliutwaa ubinadamu wetu na hivyo kwa fumbo la Umwilisho nasi tunafanyika kuwa wana wa Mungu. Ni tendo la upendo mkubwa wa Mungu kwetu. Hivyo nasi tunafanywa kwa namna fulani kuwa kama Yeye Mchungaji Mwema au Jiwe Kuu la pembeni. Hapo ndipo tunapoona wito wetu ambao unajikita katika fumbo zima la Kristo Mfufuka. Kwa namna nyingine hapa tunaona muunganiko wa Dominika hii na jukumu la kuiombea miito. Zawadi hii ya kufanyika kuwa wana wa Mungu kimantiki inaathiri pia utendaji wetu. Bila shaka utajimithilisha na Yeye, Kristo Mchungaji Mwema ambaye kwa njia yake tunafanyika kuwa wana wa Mungu. Hivyo, ni vema kujitafakari vyema katika sauti ya Mungu inayoita na kuitikia vema kusudi kuleta matunda yanayotarajiwa na Yeye anayetuita.
Kristo Mchungaji Mwema ni kielelezo, chanzo na uhai wa wito huo. Yeye aliye Njia, Ukweli na Uzima (rej. Yoh 14:6) anatuonesha jinsi nasi tunavyopaswa kuwa kama Yeye katika kutekeleza majukumu yetu mbalimbali tuliyoaminishwa kwayo kadiri ya wito wa Mungu. Kwanza kwa kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya unaowahudumia. Ni wito kwa viongozi wa kada zote kuiga mfano wake; zaidi anaonesha kwa kuwajua watu wake, yaani, mahitaji yao, vipaji vyao, udhaifu wao na hivyo kila mmoja atawaongoza kwa namna yake mahsusi. Yeye pia ni chanzo kwani ni ufunuo wa Mungu kwetu; tunapoitikia wito wetu tunapaswa kuchota kutoka kwake yale tunayopaswa kuyatekeleza; tunapaswa kuisikiliza sauti yake. Lakini pia Yeye ni uhai wa kondoo wake. Anakuwa ni nguvu ya kuwaongoza wengine kufikia ukamilifu. Hivyo Yeye aliye Mchungaji mwema anatuita sisi kuitikia miito yetu mbalimbali, kila mmoja kwa kadiri yake na kumwakilisha Yeye kwa kujimithilisha katika haiba yake ya Mchungaji Mwema. Kwa njia hiyo tutashiriki nasi katika kuuokoa ubinadamu.”
SALA: Ee Yesu utujalie wachungaji wema watakaotuongoza kwenye malisho mema na hatimaye tufike kwako mbinguni.