Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 27/04/2024

2024 APRILI 27 : JUMAMOSI-JUMA LA NNE LA PASAKA

Mt. Zita, Bikira
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 4

Somo 1. Mdo 13:44-52

Paulo na wenziwe waliingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi. Watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu. Bali Wayahudi walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana. Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana, Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia. Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini. Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote. Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao. Nao wakawakung’utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio. Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.

Wimbo wa Katikati. Zab 98:1-4

“1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)

2. Machoni pa mataifaameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)

3. Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K) “

(K) Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.

Injili. Yn 14:7-14

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba, tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe. Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.

SALA: Ee Kristo utujalie tutende kadiri ya mapenzi yako.

TAFAKARI

TUKIMWAMINI KRISTO TUTATENDA: Tunamaliza wiki ya nne ya Pasaka kwa ujumbe mzito kwa maneno ya Kristo akitualika kuomba kwa jina lake. Ni ujumbe kutoka injili ya leo (Yoh. 14:7-14). Yesu anamwelekeza Filipo namna ya kumwona Baba. Kwamba aliyemwona Mwana amemwona Baba. Lakini msisitizo mkuu unawekwa ktk kuamini, kwani anayemwamini Kristu anaweza kufanya makuu. Tukiwa na imani tunahakikishiwa kupata lolote tuombalo. Na hasa kama hilo tuombalo tunaliomba kwa jina la Yesu kwa njia ya sala zetu. Yesu ananiambia mimi, anakuambia wewe na anamwambia kila mmoja wetu: “Mkiomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya.” Tuchukue nafasi hii wakati huu wa Pasaka kujifunza kuyaweka maneno ya Kristo katika matendo yetu kwa imani na sala. Aidha tujifunze kutoka mitume ambao waliyaweka matendo na maneno yao yote katika sala wakimtanguliza Mungu awajalie kile walichomwomba kwani Yes anasema “Yeye aniaminiye mimi, kazi nifanyazo mimi, yeye naye atazifanya.”