Select Page

Masomo ya Misa Julai 13

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 13/07/2024

2024 JULAI 13: JUMAMOSI-JUMA  LA 14 LA MWAKA

Mt. Henri
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 2

Somo 1. Isa 6:1-8

Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka. Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.” Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo niliposema, “Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu; nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi.” Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, “Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa.” Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema,” Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?” Ndipo niliposema,” Mimi hapa, nitume mimi!”

Wimbo wa Katikati. Zab 93:1-2, 5

1.Bwana ametamalaki, amejivika adhama,
Bwana amejivika, na kujikaza nguvu.

(K) Bwana ametamalaki, amejivika adhama.

2.Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike; Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani; Wewe ndiwe uliye tangu milele. (K)

3.Shuhuda zako ni amini sana;
Utakatifu ndio uifaao nyumba yako,
Ee Bwana, milele na milele. (K)

Injili. Mt 10:24-33

Yesu aliwafundisha mitume wake: Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake. Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli; je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake? “Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana. Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum. Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora nyinyi kuliko mashomoro wengi. Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”

TAFAKARI.

TUENDELEE KUSHUHUDIA KWA UJASIRI: Siku moja mhubiri mashuhuri aliinuka kuhubiri akagundua kuwa kati ya aliokuwa akiwahubiria kulikuwa na mfalme wa Uajemi aliyekuwa mwovu sana, kuwa mahubiri yake yatamuumiza kwani atakapokuwa anaongea itakuwa kama anamshambulia. Kabla hajaanza kuhubiri alitafakari kidogo, halafu akajisemea kwa sauti kubwa; “Oh mhubiri, uwe makini na utakachokisema, mfalme wa Uajemi leo yupo hapa.” Halafu akatafakari tena halafu akasema, “Wewe mhubiri uwe makini nini ambacho hatokisema leo, Mfalme wa Wafalme yuko hapa leo.” Yesu aliongea dhidi ya uovu bila hofu yeyote. Anawaasa pia wanafunzi wake “Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.” Hakika Mungu pekee ndiye mwenye Mamlaka juu ya mwili na roho ya mwanadamu. Kwa kuelewa hilo nabii Isaya anarudia rudia katika unabii wake kuwa Mungu ni Mtakatifu. Isaya hakuacha kuukiri utakatifu wa Mungu mbele za watu na kwamba Mungu amewaita kuwa watakatifu.

Sala: Ee Bwana utuwezeshe kupokea vema wito wa kuishi Utakatifu na kumsifu Mungu Mtakatifu.

Masomo ya Misa Julai 12

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 12/07/2024

2024 JULAI 12: IJUMAA-JUMA  LA 14 LA MWAKA

Mt. Yohane Gualberti Abate
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 2

Somo 1. Hos 14:2-9

Bwana anasema: Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Bwana; mkamwambie,” Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo tutakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng’ombe. Ashuru hatatuokoa; hatutapanda farasi; wala hatutaiambia tena kazi ya mikono yetu, ninyi ndinyi miungu yetu; maana kwako wewe wasio na baba hupata rehema. Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao; nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo; kwa maana hasira yangu imemwacha. Nitakuwa kama umande kwa Israeli; naye atachanua maua kama nyinyoro, na kuieneza mizizi yake kama Lebanoni. Matawi yake yatatandaa, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake kama Lebanoni. Na wao wakaao chini ya uvuli wake watarejea; watafufuka kama ngano, na kuchanua maua kama mzabibu; harufu yake itakuwa kama harufu ya divai ya Lebanoni.Efraimu atasema,” Mimi nina nini tena na sanamu? Mimi nimeitika, han nitamwangalia. Mimi ni kama mberoshi wenye majani mabichi. Kwangu mimi yamepatikana matunda yako. Ni nani aliye na hekima, naye atayafahamu mambo haya? Ni nani aliye na busara, naye atayajua? Kwa maana njia za Bwana zimenyoka, nao wenye haki watakwenda katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake.

Wimbo wa Katikati. Zab 51: 3-4, 8-9, 12-13, 17

1.   Ee Mungu, unirehemu,
Sawasawa na fadhili zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu.

(K) Ulimi wangu utaiimba haki yako.

2. Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni, Nawe utanijulisha hekima kwa siri, Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe nami nitakuwa mweupe kuliko theluji. (K)

3. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)

4. Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
Na kinywa changu kitazinena sifa zako. (K)

Injili. Mt 10:16-23

Yesu aliwaambia mitume wake: “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwamwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua. Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikirifikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.

TAFAKARI

YESU, MUNGU PAMOJA NASI: Yesu, ni nafsi ya pili ya Mungu iliyoshuka duniani kukutana na mwanadamu ili kumuokoa katika hila zote na vifungo vya shetani. Neno la Mungu akatwaa mwili, akakaa kwetu! Hilo linajidhihirisha wazi katika masomo yetu ya leo. Nabii Hosea anawahubiria watu kuwa, Mungu atakuwa nao nyakati zote mithili ya baba mwenye huruma na upendo tele na tena kama umande wenye kuleta ustawi wa mazao na chanzo cha mafanikio katika jamii yote. Lakini Bwana Yesu anatahadharisha kuwa safari hiyo ya wokovu, inaambatana na msalaba ambao ni chanzo cha wokovu huo tunaouendea. Hivyo, anatuhasa kuwa wavumilivu kwani haitoshi namna ulivyoianza safari yako, namna unavyoienenda safari hiyo, ila zaidi ni namna utakavyoimaliza safari hiyo ndiyo wito tunaouona katika injili kuwa; mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Kwa hali ya kawaida ubinadamu wetu, tunakumbwa na hofu na mashaka ya namna tunaweza kuibuka washindi katika dhiki hizi. Ndiposa tunaalikwa kwa imani kutambua nguvu na uweza wa Mungu ambaye anaambatana nasi siku zote.

Sala: Ee Yesu, utujalie kutambua kuwa wakati tutakapofariki ndiyo mwisho wa mapambano yetu. Amina

Masomo ya Misa Julai 11

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 11/07/2024

2024 JULAI 11: JUMATANO-JUMA  LA 14 LA MWAKA

Mt. Benedikto, Abate
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 2

Somo 1. Hos 11:1, 3-4, 8-9

Bwana anasema: Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri.Lakini nalimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; naliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa naliwaponya. Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayari mwao, nikaandika chakula mbele yao. Niwezeje kukuacha, Efraimu? Niwezeje, kukuponya, Israeli? Niwezeje kukufanya kama Adma? Niwezeje kukuweka kama Seboimu? Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja. Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitarudi kumwangamiza Efraimu; kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya mji.

Wimbo wa Katikati. Zab 80:2-3, 15-16

1.   Wewe uchungaye Israeli, usikie,
Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi;
Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.
Uziamshe nuru zako.
Uje, utuokoe.

(K) Uangazishe uso wako, ee Bwana, nasi tutaokoka.

2.  Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi,
Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.
Na mche ule ulioupanda
Kwa mkono wako wa kuume;
Na tawi lile ulilolifanya
Kuwa imara kwa nafsi yako. (K)

Injili. Mt 10:7-15

Yesu aliwaambia mitume wake: Katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana Mtenda kazi astahili posho lake. Na mji wowote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; han kwake hata mtakapotoka. Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi. Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung’uteni mavumbi ya miguuni mwenu. Amin, nawambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule.

TAFAKIRI

MUNGU AMETUPENDA UPEO: Nabii Hosea anamuonesha Mungu kuwa anawapenda watu. Kwa upendo wake aliwainua na kuwashika mkono Waisraeli. Kama yaya au mlezi amfundishavyo mtoto kutembea ndivyo alivyo wafundisha Waisraeli kutembea. Cha kushangaza zaidi kadiri alivyo wapenda Waisraeli ndivyo walivyo kengeuka, kuwa mbali naye na kumkataa. Ni kwa upendo huo alimpeleka Kristo ili atukomboe. Na Kristo anawaandaa tena mitume na kwawatuma kwa upendo kuwafikishia watu wake upendo wa Mungu. Anawatuma kuutangaza ufalme wa Mungu wakiwaponya wagojwa, wakiwafufua wafu, wakiwatakasa watu na kutoa pepo. Kristo anawaelekeza hawa mitume watambue uhitaji wa watu na kuwahudumia kwa kadri inavyowezekana akiwakumbusha ya kuwa wamepewa bure na watoe bure. Kristo anawaelekeza wawe wakarimu. Inafaa tutafakari kwa moyo wa dhati huu ukarimu na upendo wa Mungu tunaurudishaje? Ni mwaliko kwa kila mmoja kuwa mkarimu kwa wote hasa tuutambue huu ukarimu wa Mungu na kurudisha ukarimu, tumependwa nasi tupendane. 

Sala: Ee Bwana utusaidie kukupenda kwa Moyo wote na kuwapenda wengine kwa pendo lako.

Masomo ya Misa Julai 10

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 10/07/2024

2024 JULAI 10: JUMATANO-JUMA  LA 14 LA MWAKA

Mt. Olaf Alexanda
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 2

Somo 1. Hos 10:1-3, 7-8, 12

Bwana asema hivi: Israeli ni mzabibu, utoao matunda yake; kwa kadiri ya wingi wa matunda yake; kwa kadiri iyo hiyo ameongeza madhabahu zake; kwa kadiri ya wema wa nchi yake, kwa kadiri iyo hiyo wamefanya nguzo nzuri. Moyo wao umegawanyika; sasa wataonekana kuwa na hatia; yeye atazipiga madhabahu zao, ataziharibu nguzo zao. Yakini sasa watasema,”Hatuna mfalme; kwa maana hatumchi Bwana; na mfalme huyo je! Aweza kututendea nini?” Katika habari za Samaria, mfalme wake amekatiliwa mbali, kama povu usoni pa maji. Mahali pa Aveni palipoinuka, yaani, dhambi ya Israeli, pataharibika; mwiba na mbigili itamea juu ya madhabahu zake; nao wataiambia milima,” Tusitirini;” na vilima,”Tuangukeni.”Jipandieni katika haki, vuneni kwa fadhili; uchimbueni udongo wa mashamba yenu; kwa maana wakati umewadia wa kumtafuta Bwana, hata atakapokuja na kuwanyeshea haki.

Wimbo wa Katikati. Zab 105:2-7

1.   Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.

(K) Siku zote mtafuteni uso wake Bwana.

2.   Mtakieni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake sikuzote.
Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya.
Miujiza yake na hukumu na kinywa chake. (K)

3.    Enyi wazao wa Ibrahim, mtumishi wake;
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
Duniani mwote mna hukumu zake. (K)

Injili. Mt 10:1-7

Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye; Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti. Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema.”Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.”

TAFAKARI

KRISTO ANATUITA, ANATUWEZESHA NA KUTUTUMA: Katika kuteua Kristo ameteua watu wa kawaida kabisa wa kufanya utume mgumu sana katika historia. Hawakuwa watu maalumu au wataalamu, ila kwa kuwaita anaanza kuwaandaa. Katika hali yao hiyo Kristo anawawezesha na kuwapa mamlaka juu ya pepo wachafu wawatoe, kuponya magonjwa na udhaifu wa kila aina. Kisha kuwawezesha anawatuma kwa maelekezo kwenda kutafuta kilichopotea katika nyumba ya Israeli na kuutangaza Ufalme wa Mungu. Kristo anamwita kila mmoja wetu, anatuwezesha kuutenda utume wake kwa sakramenti tunazozipokea, kwa ubatizo tunashirikishwa ukuhani, unabii, na ufalme wa Kristo. Kama makuhani tuwe watu wa sala na kutolea sadaka kwa Mungu wetu, kama wafalme kujitawala na kutawala malimwengu tukiyaelekeza kwa Mungu na kama manabii kutangaza Neno la Mungu na kuwaalika watu kwenye ufalme wa Mungu kwa kufanya toba. Nabii Hosea anautimiza vema utume wake katika Israeli akiwaonya na kuwaalika kufanya toba ya kweli.

Sala: Ee Bwana Neema yako ituwezeshe kuitikia vema wito uliotuitia na kuutimiza kwa sifa na utukufu wa Mungu.

Masomo ya Misa Julai 9

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 09/07/2024

2024 JULAI 9: JUMANNE-JUMA  LA 14 LA MWAKA

Mt. Veronika Giuliani, Bikira.
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 2

Somo 1. Hos 8:4-7, 11-13

Bwana asema hivi: Wamesimamisha wafalme, lakini si kwa shauri langu; wamejifanyia wakuu, lakini nalikuwa sina habari; kwa fedha yao na dhahabu yao wamejifanyizia sanamu, kusudi wakatiliwe mbali. Amemtupa ndama yako, Ee Samaria; hasira yangu imewaka juu yao; siku ngapi zitapita kabla ya hao kupata hali isiyo na hatia? Maana katika Israeli kimetokea hata na kitu hiki; fundi ndiye aliyekifanya, nacho si Mungu kamwe; naam, ndama ya Samaria itavunjika vipande vipande. Kwa maana wao hupanda upepo, nao watavuna tufani; nafaka haina bua; machipuko yake hayatoi masuke; hata ikiwa yatoa, wageni watayameza. Kwa kuwa Efraimu ameongeza madhabahu kwa dhambi, madhabahu zimekuwa dhambi kwake. Nijapomwandikia sheria yangu katika amri elfu kumi, zimehesabiwa kuwa ni kitu kigeni. Kwa habari za dhabihu za matoleo yangu, hutoa dhabihu ya nyama na kuila; lakini Bwana hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, na kuwapatiliza dhambi zao; watarudi kwenda Misri.

Wimbo wa Katikati. Zab 115:3-10

1.  Mungu wetu yuko mbinguni,
Alitakalo lote amelitenda.
Sanamu zao ni fedha na dhahabu,
Kazi ya mikono ya wanadamu.

(K) Enyi Israeli, mtumainini Bwana.

2.  Zina vinywa lakini hazisemi,
Zina macho lakini hazisomi,
Zina maskio lakini hazisikii,
Zina pua lakini haziskii harufu. (K)

3.   Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi,
Wala hazitoi sauti kwa koo zake
Wazifanyao watafanana nao,
Kila mmoja anayezitumainia. (K)

 4.   Enyi Israeli, mtumainini Bwana;
Yeye ni msaada wao na ngao yao;
Enyi mlango wa Haruni, mtumainini Bwana;
Yeye ni msaada wao na ngao yao. (K)

Injili. Mt 9:32-39

Walimletea Yesu mtu bubu mwenye pepo. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastaajabu, wakasema,” Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wo wote.”Lakini Mafarisayo wakasema,”Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo.”Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”

TAFAKARI

TUMEITWA KUENDELEZA UTUME WA KRISTO: Yesu alifukuza mapepo, aliponya wagonjwa, alifufua wafu, alisamehe dhambi na alitangaza Ufalme wa Mungu.Kristo alielewa hali mbaya waliyokuwa nayo watu wa kawaida kabisa. Hawakuwa na mtu wa kuwapa matumaini na kuwaelezea juu ya fadhila za Kimungu.Ni wajibu wa kila mkristo kutangaza Habari Njema ya wokovu wetu kwa namna ya maisha yake. Alihimiza utume waliopaswa kuuishi wanafunzi wake, uliohitaji kujitoa sadaka, kujikatalia na kufuata mfano wa Kristo. Mark Link anasema Yesu angali andika nukuu katika hili ingekuwa “Sina miguu ila miguu yako kunipeleka ulimwenguni. Sina Mikono ila mikono yako kuwafikia wahitaji. Sina ulimi bali ulimi wako kuwaambia watu ni kwa nini niliteseka na kufa kwa ajili yao.” Somo la kwanza latupa mfano mzuri wa mtu anayeitenda kazi ya Mungu, ni nabii Hosea anaendelea kuitenda kazi ya Mungu akiwaonya Waisraeli juu ya mwenendo wao wa kumwasi Mungu. Anawaalika kufanya toba na wampendeze Mungu. Ndio wito tunaoupokea kila siku ya maisha yetu. 

Sala: Ee Bwana neema yako ituwezeshe kuwafikishia watu wako habari njema ya wokovo.

Masomo ya Misa Julai 8

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 08/07/2024

2024 JULAI 8: JUMATATU-JUMA  LA 14 LA MWAKA

Wat.Hesperius na Zoa, Wafiadini
Rangi: Kijani

Zaburi:

Somo 1. Hos 2: 14-16, 19-20

Bwana asema hivi:”Angalia, mimi nitamshawishi, na kumleta nyikani, na kusema naye maneno ya kumtuliza moyo. Naye ataniitikia huko, kama siku zile za ujana wake, na kama siku ile alipopanda kutoka nchi ya Misri.Tena siku hiyo itakuwa, asema Bwana, utaniita ‘Ishi’, wala hutaniita tena ‘Baali.’Nami nitakuposa uwe wangu kwa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema. Nami nitakuposa kwa uaminifu; nawe utamjua Bwana.

Wimbo wa Katikati. Zab 145:2-9

1. Ee Bwana wangu, Mfalme,nitakutukuza,
Nitalihimidi jina lako milele na milele.
Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele.

(K) Nitalihimidi jina lako milele na milele.

2. Bwana  ana fadhili,ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira,ni mwingi wa rehema.
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.

3. Ee Bwana,kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu  wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako. (K)

4. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinamia chini. (K)

Injili. Mt 9:18-26

Yesu alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema,”Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi.”Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake.  Kwa maana alisema moyoni mwake,”Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.” Yesu akageuka, akamwona, akamwambia,”Jipe moyo mkuu, binti yangu, imani yako imekuponya.”Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Yesu alipofika nyumbani kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia,”Ondokeni, kwa maana kijana hakufa, amelala tu.”Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule kijana akasimama. Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote.

TAFAKARI

IMANI INAPONYA: Jumbe anayewakilisha ombi lake kwa Kristo, amedhihirisha imani yake kwa kumwendea na kumwambia “Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi.” Mwanamke aliyekuwa mgonjwa kwa miaka kumi na mbili alijitafakari akatambua kwa imani kuwa akigusa vazi la Kristo atapona. Watu hawa wawili wanadhihirisha kuwa wana Imani kubwa. Mimi msomaji wa sasa je nadhihirisha Imani yangu kwa Kristo.Nadhiriki kulinganisha vazi la Kristo na Sakaramenti za Kanisa. Kama huyu mama kwenye Injili ya leo alivyoamua na kugusa vazi la Kristo kwa Imani nasi wakristo tunaweza kumfikia na kumgusa Kristo kwa Imani katika Sakaramenti tunazopokea. Tukifanya hivyo nguvu ya uponyaji kutoka kwenye Sakramenti za Kristo utatufikia kama ilivyomfikia huyu mama. Ulinganisho huu unaweza usiwe makini ila unatuwezesha kutambua zawadi ya neema inayopatikana kwa Sakramenti hizo, ukweli ni kuwa Kristo anapenda kumponya kila mmoja kama alivyomponya yule Mwanamke. Tuidhihirishe imani yetu.  

Sala: Ee Bwana utuwezeshe kutambua kuwa tunapata nguvu ya uponyaji wako katika Sakramenti.