Select Page

Masomo ya Misa Mei 8

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 08/05/2024

2024 MEI 8 : JUMATANO-JUMA LA SITA LA PASAKA

Mt. Viktori wa Mauritania, Mfiadini
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Mdo 17:15, 22-18:1

Siku zile, wale waliomsindikiza Paulo wakampeleka mpaka Athene; nao wakiisha kupokea maagizo kuwapelekea Sila na Timotheo, ya kwamba wasikawie kumfuata, wakaenda zao. Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema, Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, kwa Mungu asiyejulikana. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua. Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wetu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake. Basi, kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu. Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu. Basi waliposikia habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine wakasema, Tutakusikiliza tena katika habari hiyo. Basi hivi Paulo akaondoka akawaacha. Baadhi ya watu wakashikamana naye, wakaamini; katika hao alikuwamo Dionisio, Mwareopago, na mwanamke mmoja jina lake Damari, na watu wengine pamoja na hao. Baada ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho.

Wimbo wa Katikati. Zab 148:1-2, 11-14

1. Aleluya.
Msifuni Bwana kutoka mbinguni;
Msifuni katika mahali palipo juu.
Msifuni enyi malaika zake wote;
Msifuni, majeshi yake yote.

(K)Utukufu wako unajaza mbingu na ulimwengu.

2. Wafalme wa dunia, na watu wote,
Wakuu, na makadhi wote wa dunia.
Vijana waume na wanawali,
Wazee, na watoto. (K)

3. Na walisifu jina la Bwana,
Maana jina lake peke yake limetukuka;
Adhama yake i juu ya nchi na mbingu. (K)

4. Naye amewainulia watu wake pembe,
Sifa za watauwa wake wote;
Wana wa Israeli, watu walio karibu naye. (K)

Injili. Yn 16:12-15

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake:  Bado ningali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa.  Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.  Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasha habari.

TAFAKARI

ROHO MTATAKATIFU NI KIONGOZI WETU: Injili ya leo ni mwendelezo wa Injili ya jana. Yesu anaendelea kuagana na wafuasi wake na anajua kuwa kazi aliyokuwa ameanza haikuwa imekamilika. Wafuasi ndiyo walikuwa katika hatua za awali za kuendeleza kazi aliyoanza Yesu. Yesu aliwafahamu wafuasi wake kuwa hata baada ya kuwafundisha hawakuwa na uwezo wa kuelewa yote na kuwa wasingejua matokeo ya kazi ya mafundisho yake kwao kwa wakati ule. Ili wapate kuelewa zaidi bado alikuwa na mengi ya kuwafundisha ila Roho Mtakatifu atakuja kuwasaidia waelewe. Amewapa maelekezo kuwa Roho Mtakatifu atawaimarisha na kuwafundisha ukweli wote. Sisi tulipobatizwa tulipewa Roho Mtakatifu na katika Kipaimara tukampokea tena na ukamilifu wa mapaji yake saba. Tumpe Roho Mtakatifu nafasi afanye kazi ndani mwetu kwa kuwa tayari kutumia vema karama mbalimbali anazotujalia. Kama Injini ya gari ilivyo na umuhimu kwenye gari ndivyo Roho Mtakatifu alivyo wa Muhimu katika Kanisa la Mungu.

Masomo ya Misa Mei 7

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 07/05/2024

2024 MEI 7 : JUMANNE-JUMA LA TANO LA PASAKA

Mt. Rose Venerini
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Mdo 16:22-34

Siku ile pale Filipi, wenyeji waliwakamata Paulo na Sila, wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora. Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako. Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake.  Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati huo huo. Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu.

Wimbo wa Katikati. Zab 138:1-3, 7-8

1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu. 

(K) Utanyosha mkono, Ee Bwana, utaniokoa.

2. Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
Kwa maana umeikuza ahadi yako,
Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)

3. Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu,
Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
Usiziache kazi za mikono yako. (K)

Injili. Yn 16:5-11

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake:  Sasa mimi naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwendapi?  Ila kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu. Lakini mimi  nawambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi; kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena; kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.

TAFAKARI

ROHO MTAKATIFU NI MSAIDIZI WETU: Katika Injili ya leo tumemsikia Yesu akiwaaga wanafunzi wake kuwa anarudi kwa yule aliyemtuma. Kama ilivyo kawaida kwa watu waliozoeana kwa muda mrefu kuagana, ndivyo ilivyokuwa kwa wafuasi wa Kristo. Wamehuzunika kwasababu wanalazimika kuagana na Kristo japo hawapendi. Huzuni yao ilisukumwa na ukweli kwamba watakosa uwepo wa Yesu kati yao kwa muda. Yesu anatuliza huzuni yao kwa kuwahakikishia kuwa atampeleka Roho Mtakatifu. Yesu anawaeleza kuwa Roho Mtakatifu atakapokuja atawafumbulia mambo mengi ikiwemo kuudhihirishia ulimwengu kuwa ulianguka katika dhambi ya kutomwamini Mwana wa Mungu. Tunaalikwa tutambue nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu. Katika kupokea Sakramenti ya upatanisho Roho Mtakatifu ni muhimu kwani anatukumbusha ni wapi tumekosea na hivyo tufanye toba ya kweli na kujirudi. Tumruhusu Roho Mtakatifu atuangaze katika maisha yetu.
SALA: Ewe Roho Mtakatifu uje ukawe Msaidizi wetu katika utume wetu.

Masomo ya Misa Mei 6

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 06/05/2024

2024 MEI 6 : JUMAMOSI-JUMA LA TANO LA PASAKA

Mt. Evodi, Askofu
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 2

Mtakatifu Evodi wa Antiokia

by Claretian Publications

Somo 1. Mdo 16:11-15

Tuling’oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake kwa tanga moja, na siku ya pili tukafika Neapoli; na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha. Hata siku ya Sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale. Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo. Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha. 
(K) Bwana awaridhia watu wake.

Wimbo wa Katikati. Zab 149:16, 9

1. Aleluya.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao. (K)

2. Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)

3. Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wote. (K)

Injili. Yn 15:26-16:4

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia. Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami. Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa.  Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi.  Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia.

TAFAKARI

MAISHA YETU YAMSHUHUDIE KRISTO: Leo katika Injili Yesu anatuahidia Roho Mtakatifu ambaye atamshuhudia. Anatoa mwaliko kwetu sisi tuliobatizwa na kukaa pamoja na Kristo kwa muda mrefu tumshuhudie pia. Maisha ya ushuhuda ni maisha yanayodai sadaka kubwa hata ikibidi kumwaga damu. Yesu anatupa moyo kuwa tusiogope kuishi maisha ya ushuhuda. Kwa kuwa mwaminifu kwa Yesu tunaweza kutengwa na jamii hata kuuawa kama ilivyokuwa kwa Kristo mwenyewe. Tukumbuke kuwa kwa Sakramenti ya Kipaimara tunafanywa kuwa askari hodari wa Yesu Kristo. Tusiache ujumbe wa Kristo upotoshwe kwa sababu ya hofu. Yesu ametuandaa vizuri hivyo tuwe tayari kushuhudia Habari Njema hata kama itatugarimu damu na jasho letu. Tupo katika ulimwengu ambao hauna taswira sahihi ya Mungu, ndiyo maana mambo yanayomhusu Mungu hayapewi kipaumbele. Sisi tuliofunuliwa hayo yote hatuna budi kushuhudia taswira sahihi ya Mungu hata kama ulimwengu utatuchukia.

SALA: Ee Yesu naomba unijalie ujasiri wa kushuhudia imani yangu wakati wote.

Masomo ya Misa Mei 5

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 05/05/2024

2024 MEI 5 : DOMINIKA YA 6 YA PASAKA

Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 

Somo 1. Mdo 10: 25-26, 34 -35, 44-48

Petro alipokuwa akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguu, akamsujudia. Lakini Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu. Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye. Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno. Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu, Ni nani awezaye kukataza maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi? Akaamuru wabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha.

Wimbo wa Katikati. Zab 98: 1 – 4

“1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)

2. Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)

3. Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)”

(K) Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.

Somo 2. 1 Yoh 4: 7 -10

Wapenzi, na tupendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.

Injili. Yn 15: 9-17

Yesu aliwaambia wafuasi wake: Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe. Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana.

TAFAKARI

“FURAHA YA KWELI INAPATIKANA KATIKA KRISTO
Hati ya kichungaji ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vaticano juu ya Kanisa katika ulimwengu mamboleo «Furaha na Matumaini (Gaudium et Spes) »inasema hivi: “Ukweli ni kwamba katika fumbo la Neno la Mungu kufanyika mwili ndipo fumbo la mwanadamu linafumbuliwa. Hii ni kwa sababu Adam, mwanadamu wa mwanzo kabisa alikuwa taswira ya yeye Kristo Yesu ambaye alipaswa kutujia. Kristo ambaye ni Adam wa mwisho amemfunulia mwanadamu ukweli kuhusu asili yake na ukweli juu ya wito wake mkuu kwa kuufunua upendo wa Baba na upendo wake” (Namba 22). Sehemu hii ya waraka wa Mtaguso inanuia kutuonesha tija ya fumbo la umwilisho ambalo kwalo majawabu mengi kuhusiana na changamoto zinazomkabili mwanadamu hupata majawabu yake. Moja ya changamoto hizo ni furaha. Ni ipi iliyo furaha ya kweli?
Kiuhalisia mwanadamu anatamani kuwa katika hali ya furaha daima lakini je, ni ipi iliyo kwake furaha ya kweli na ya kudumu? Furaha ya kweli inapatikana katika Kristo. Mtakatifu Bernadetha Subiru aliambiwa na Mama Bikira Maria kwamba anamuahidi furaha lakini si katika maisha ya ulimwengu huu bali maisha ya baadaye. Kristo anatuambia katika Injili ya leo: “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.” Hivyo mambo mawili yanawekwa wazi kama nyenzo ya kuifikia furaha kamilifu, yaani kuzishika amri za Mungu na kukaa katika pendo la Mungu.
Utimilifu wetu wanadamu unapatikana katika kuungana na Kristo. Dhana hii imetafakariwa kwa kirefu katika Dominika mbili zilizopita ambapo Kristo alijitanabaisha kama Mchungaji wa Kondoo na mzabibu wa kweli. Fumbo la umwilisho kama nilivyodokeza hapo mwanzoni limeweka wazi ukweli kuhusu mwanadamu na ukweli huo unajionesha katika muunganiko kamilifu na Kristo na kwa njia yake na Mungu Baba. Muunganiko huo hutekelezwa kwa njia ya kuzishika amri za Mungu ambazo ndizo miongozo na kanuni za kuipata furaha ya kweli na inayodumu. Hakuna kitu chochote kinachoweza kuwa katika ukamilifu bila kufuata kanuni za kuundwa kwake. Gari likiacha kufuata kanuni za kuundwa kwake matairi yakagoma kwenda au breki zikaacha kukamata sawasawa au taa ya kuashiria kulia au kushoto ikaacha kuwaka matokeo yake ni majanga na uharibifu. Hivi ndivyo kwetu sisi wanadamu. Hatukujiumba au kujileta duniani kwa utashi wetu wenyewe. Tunapoacha kuunganika na Yeye aliyetufanya kwa kuendana na kanuni anazotuwekea tunaingia katika ukengeufu na mwisho ni majanga.
Changamoto tuipatayo katika ulimwengu mamboleo ni kuenea kwa uhuru wa mwanadamu katika kutafuta auheni ya maisha na furaha. Namna hii imetuondoa katika kulitazama neno la Mungu na matokeo yake tunajitafutia namna zetu kadiri ya vionjo vyetu na misukumo ya kibinadamu. Matokeo yake ni dhahiri: ni anguko kwa mwanadamu na udhalilishaji wa utu wa mtu. Uhuru tunaojivika unamithilika na uhuru bandia kwani wengi hujikuta tumeingia katika misukosuko na matatizo mengi badala ya kupata uhuru wa kweli. Kristo ambaye ni ufunuo wa uhuru wa kweli katika kutafuta furaha ya kudumu ametufundisha bustanini Getsemani namna ya kuonesha uhuru wako hali umeunganika na mapenzi ya Mungu, yaani amri zake. Akiwa katika hali ya huzuni kubwa kiasi cha kutokwa na jasho la damu alisali akisema: “Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke” (Lk 22:42). Kama binadamu anatamani kupata faraja na furaha ya kudumu lakini akiwa ameunganika na Baba yake anataka kuipata furaha hiyo kadiri ya mapenzi yake.
Tunapoitafuta furaha bila kuunganika na Mungu tunaishia katika furaha za muda mfupi. Hili kwa namna ya pekee huonekana katika furaha tuitafutayo kwa kuwatumia wenzetu kama vyombo. Ni namna ambavyo mwanadamu anafumba macho na kutoona muunganiko wa asilia uliopo kati yake na ndugu yake pembeni yake na hivyo kumweka mbele yake kama chombo cha kujinufaisha na kuifurahisha nafsi yake. Namna hii kamwe haitupatii furaha ya kweli. Hata tukijidanganya kwa kusema kila mmoja ahangaike na hali yake lakini bado damu yake itakuita tu. Unyonyaji, manyanyaso, mateso na uhasi mwingine dhidi ya mwanadamu mwenzako hukurudia mwenyewe tu. Nahau ya kiingereza isemayo what goes around comes around itugutushe katika hilo.
Ndiyo maana Kristo anaipanua namna ya kuufanya upendo wetu utupatie furaha ya kudumu: “Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” Furaha yetu ya kweli inaonekana kwanza katika mwelekeo wa upendo kwa Mungu na pili katika mwelekeo wa upendo wetu kwa jirani. Kristo anaendelea kuwa kielelezo kwetu kwa namna hiyo kama anavyofafanua Mtume Yohane katika somo la pili la Dominika hii. Hii namna ya kujitoa nafsi yako, kujisadaka kwa ajili ya wenzako. Sehemu hiyo ya Maandiko matakatifu inapigia mstari dhana ya Mungu kuwa asili au sababu ya yote ayatendayo mwanadamu. Upendo wetu kwa wenzetu asili yake si sisi; asili yake tunapaswa kuiona katika Mungu: “Wapenzi na tupendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mngu.” Hivyo namna yoyote ya upendo kati yetu sisi kwa sisi inapaswa kuchipuka katika Yeye kupitia Kristo Bwana wetu.
Upendo huo ambao unapata asili yake katika Mungu unatutajirisha zaidi kwa kuunganika na watu wote na pia kuona utendaji wa Mungu katika kila kazi njema ya mwanadamu. Petro anapoingia nyumbani kwa Kornelio anatamka kwa ujasiri akisema: “hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.” Petro amefanya tamko hilo baada ya maono aliyoyapata katika aya zilizotangulia somo la leo, aya ambazo zilimfunulia namna utendaji Mungu unavyotenda kazi kwa wanadamu wote. Kristo anayeufunua ubinadamu wetu katika hali yake stahiki anaugusa ubinadamu wote na yeyote anayeifuata njia yake kwa njia ya neema ya Mungu ataweza kumtukuza Mungu na hivyo kuingia katika kundi la wale wanaozishika amri zake na hivyo sote tutaipata furaha ya kweli.
Hivyo tuitikie wito wa Kristo katika hitimisho la Injili ya leo. Yeye anatutaka tuendelee kubaki katika urafiki na Yeye kwa kusikiliza na kuliishi lile analotufundisha. Hali hiyo itatufanya kuwa wana huru na si watumwa. Hii ni kwa sababu kwa kulisikiliza Neno lake tutayafahamu yale anayotuamuru kufanya na yale anayoyatenda lakini “mtumwa hajui atendalo bwana wake.” Ni wito wa kujitajirisha na habari za ufalme wa Mungu kwa kuisikiliza sauti ya Kristo ambaye anatuambia yote anayoyasikia kwa Mungu Baba aliye chanzo na maana ya ubinadamu wetu na pia chimbuko la furaha yetu ya kweli.”

SALA: Ee Kristo Mfufuka utujaze furaha katika upendo wako.

Masomo ya Misa Mei 4

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 04/05/2024

2024 MEI 4 : JUMAMOSI-JUMA LA TANO LA PASAKA

Mt. Godehardi, Askofu”
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 1

Somo 1. Mdo 16:1-10

Siku zile, Paulo alifika Derbe na Listra na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani. Mtu huyo alishuhudiwa vyema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio. Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtairi kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani. Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike. Makanisa yakatiwa nguvu katika ile imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku. Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia, wakajaribu kwenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemka Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, vuka, uje Makedonia utusaidie. Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.

Wimbo wa Katikati. Zab 100:1-3, 5

“1. Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote
Mtumikieni Bwana kwa furaha.
Njoni mbele zake kwa kuimba; (K)

K) Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote.

2. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)

3. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)”

Injili. Yn 15:18-21

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka.

TAFAKARI

ULIMCHUKIA KRISTO, UTATUCHUKIA NA SISI PIA: Tupo ulimwenguni lakini hatupaswi kuwa wa ulimwengu. Kwa ubatizo wetu tumechaguliwa na Yesu tusiwe tena wa ulimwengu. Matendo yetu, maneno yetu, na namna yetu ya kuishi, havipaswi kufuata mawimbi ya ulimwengu huu. Tunapaswa kuwa mwanga pale ulimwengu unapokuwa giza, tunapaswa kuleta ladha ulimwenguni pale ulimwengu unapopoteza ladha. Haya yote ni kwenda kinyume na mkondo wa walimwengu wa sasa, na hivyo tukiendelea hivyo tuwe tayari kuchukiwa kwa matendo yetu yasiyoendana na ya walimwengu kwani matendo yetu yanapaswa kuwashitaki walimwengu. Tusife moyo kwani tunachota nguvu kutoka kwa Yesu kwani kama ulimwengu ulivyomchukia Kristo, utatuchukia sisi wafuasi wake pia. Watakatifu wengi walikubali kwenda kinyume na ulimwengu na malimwengu hata wakamwaga damu yao kwa ajili ya Kristo. Mtakatifu Karoli Lwanga na wenzake ni kielelezo hapa kwetu Afrika Mashariki jinsi walivyokubali kufa wakiishuhudia imani.

SALA: Ee Yesu nijalie uvumilivu katika magumu yaletwayo na Maisha ya ufuasi.

Masomo ya Misa Mei 3

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 03/05/2024

2024 MEI 3 : IJUMAA-JUMA LA TANO LA PASAKA

WAT. FILIPO NA YAKOBO, MITUME
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Juma 1

Somo 1. 1 Kor 15:1-8

Ndugu zangu, nawaarifu ile Injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri; isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake.

Wimbo wa Katikati. Zab 19:2-5

“1. Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa. (K)

K) Sauti yao imeenea duniani mwote.

2. Hakuna lugha wala maneno,
Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
Katika hizo ameliwekea jua hema. (K)”

Injili. Yn 14:6-14

Yesu alimwambia Tomaso: Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba, tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuoneshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuoneshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe. Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.

SALA: Ee Yesu naomba unifungue macho yangu ya imani nimwone Baba kupitia wewe.

TAFAKARI

YESU NI NJIA YETU: Leo tunaadhimisha sikukuu ya watakatifu Filipo na Yakobo mitume. Hawa walitambua umuhimu wa maisha ya sadaka ili waweze kufika kwa Baba. Katika Injili tunaona kuwa Yesu ni Sakramenti ya Baba, yaani tunamwona Baba kupitia Yesu. Yesu anaposema yeye ni njia ya kwenda kwa Baba, hamaanishi kuwa yeye ni barabara tu bali anayetaka kwenda kwa Baba ni lazima aishi na kutenda kama Yesu. Yeye ni njia kwa kuwa yeye ndiye mlango wa kuingia na kutoka (Yn 10:9). Yeye ndiye ukweli kwani kwa kumtazama yeye tunamwona Baba. Yeye ni uzima kwani kwa kuishi kama yeye tunaungana na Baba anayetupa uzima. Swali la Philipo la kutamani kumwona Baba liwe tamanio letu sote ila tusimtafute Baba nje ya Yesu. Tumwone Baba katika Neno lake, katika Sakramenti zake, katika mamlaka funzi ya kanisa na katika nafsi ya kuhani mwadhimishaji wa mafumbo matakatifu ya imani yetu. Pia tumwone Baba katika mapokeo matakatifu yanayofunuliwa kwetu na Yesu Kristo.