Select Page

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa 11/02/2024

2024 FEBRUARI 11. DOMINIKA YA 6 YA MWAKA.
Nyeupe
Zaburi: Juma 2

SOMO 1:  Law 13: 1- 2, 44-46

Bwana alinena na Musa na Haruni, na kuwaambia, mtu atakapokuwa na kivimbe katika ngozi ya mwili wake, au kikoko, au kipaku king’aacho, nalo likawa pigo la ukoma katika ngozi ya mwili wake, ndipo atakapoletwa kwa Haruni kuhani, au kwa wanawe, makuhani mmojawapo; yeye ni mtu mwenye ukoma, yu najisi; na kuhani hana budi atasema kuwa yu najisi; pigo lake li katika kichwa chake. Kisha mwenye ukoma aliye na pigo ndani yake, nguo zake zitararuliwa, na nywele za kichwa chake zitaachwa wazi, naye atafunika mdomo wake wa juu, naye atapiga kelele, Ni najisi, ni najisi. Sikuzote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi; yeye yu najisi; atakaa peke yake; makazi yake yatakuwa nje ya marago.

Wimbo wa Katikati.  Zab 32: 1-2, 5, 11

1. Heri aliyesamehewa dhambi,
Na kusitiriwa makosa yake.
Heri Bwana asiyemhesabia upotovu,
Ambaye rohoni mwake hamna hila.  (K)

(K) Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso,
       Utanizungusha nyimbo za wokovu. 
   
2. Nalikujulisha dhambi yangu,
Wala sikuuficha upotovu wangu.
Nalisema, nitayakiri maasi yangu kwa Bwana,
Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu. (K)

3. Mfurahieni Bwana;
Shangilieni enyi wenye haki, pigeni vigelegele vya furaha;
Ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo. (K)

Somo 2. 1 Kor 10:31, 11:1

Ndugu, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lolote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu. Msiwakoseshe Wayahudi wala Wayunani wala Kanisa la Mungu; vile vile kama mimi niwapendezavyo watu wote katika mambo yote, nisitake faida yangu mwenyewe, ila faida yao walio wengi, wapate kuokolewa. Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo. 

Injili. Mk 1:40-45

Siku ile, mtu mwenye ukoma alimsihi Yesu na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajioneshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao. Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali. 

TAFAKARI.

NENDA MBELE YA YESU, JIONESHE UKOMA WAKO NAYE ATAKUTAKASA
Ukoma ni aina ya ugonjwa ambao hujionesha katika ngozi ya mwanadamu. Ugonjwa huu huathiri mishipa ya fahamu kiasi cha mgonjwa kushindwa kuhisi chochote anapoguswa sehemu ya ngozi iliyoathiriwa. Wengine hupata uvimbe unaopasuka baadaye na hata kuwa sababishia vidonda vikubwa. Ugonjwa huu usipotibiwa mapema hupelekea ulemavu au upotevu wa viungo mbalimbali. Jamii ya kale iliwatenga watu wenye ukoma kwani waliogopa kuambukizwa. Hii ni kwa sababu kwa wakati huo tiba yake ilikuwa bado haijapatikana. Katika mazingira hayo ziliwekwa hata sheria kali za kidini za kuwatenga, suala ambalo tunalisikia katika somo la kwanza la Dominika hii. Mtu huyo alihesabika kuwa ni “najisi na pigo lake li katika kichwa chake”. Huyu atatamkwa kuwa yu najisi na kuhani na hivyo kutengwa kadiri ya sheria ya Musa.
Hivyo tunaona moja kwa moja kuwa yeye ambaye anapatwa na ukoma anakuwa ni yeye aliyepatwa na balaa na anapaswa kutengwa na jamii. Ujio wa Kristo unaleta Mapinduzi makubwa kwa mtazamo huo. Zamani za Wayahudi waliwatenga bila kuwapatia nafasi ya uponyaji na kurejea tena katika jamii yao. Lakini lipo la msingi ambalo pengine lilirukwa au kutotiliwa maanani, yaani nafasi ya uponyaji. Katika somo la kwanza tumeelezwa wazi kwamba “atapiga kelele, ni najisi, ni najisi. Siku zote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi”. Lakini tujiulize kilio chake cha kujitangaza yu najisi kilimsadia nini? Je! Kilinuia tu kumtambulisha na hivyo watu kumkwepa? La hasha. Hicho kilikuwa kilio cha ndani cha kuwaomba wenzake huruma yake ili kufikia uponyaji na kurejea tena. Ni njia ya kuwafanya wengine watambue ugonjwa wake wamsaidie na wao pia kuwa katika tahadhari kusudi wasipatwe na ugonjwa huo; kilio chake kinadai huruma yake na kuonesha hamu ya uponyaji. Ila kinyume chake walizidi kutengwa na kudharaulika.
Katika jamii magonjwa hatari ya kuambukiza hulazimisha mtu kutengwa kwenye kambi maalum. Hali hii haimuondolei mtu huyu haki yake ya kuhudumiwa na kuthaminiwa kama mwanadamu. Utu wake na thamani yake haibadilishwi na ugonjwa au kasoro anayokuwa nayo. Kwa muono huo huo kwa mtu aliye dhaifu kiroho; yeye anayeonekana kuzama katika maisha ya dhambi, huyu pia anahitaji kuthaminiwa katika utu wake. Ni wajibu wetu kuwa karibu nao na kuwasaidia kupona na kuepukana na madhila wanayokabiliana nayo. (Angalia mfano wa sasa katika corona na pia namna watu wanavyowatendea wenye dhambi zinazoonekana za aibu).
Ndani ya watu hawa ni kilio cha kutaka uponyaji. Tukiwatenga na kuwaona hawafai kuwa karibu yetu watagangwa vipi? Kilio na hamu yao hii inapata mwarobaini katika Kristo ambaye anaonesha utayari wa kumakaribia na kumsikiliza. Hapa ndipo mkoma anafunguka na kuweza kutamka kiu yake: “ukitaka waweza kunitakasa”. Anatamka katika namna ya unyenyekevu huku akiwa amepiga magoti na pia kuomba ridhaa ya Kristo na si kumlazimisha. Katika hali hiyo huruma ya Mungu inamfungukia na ukoma wake unatakaswa. “Ukitaka”: ni utayari wa kuyapokea mapenzi na mpango wa Mungu kwako. Si kudai uponyaji, si kulazimisha bali ni kuomba atakavyo Mungu kifanyike. “Waweza”: ni jicho la kiimani linalotambua na kukiri uwezo wa Mungu. Yeye anaweza yote kwa kuwa ni Mwenyezi (omnipotent). Inadhihirisha imani yake kubwa katika wema wa Mungu na utendaji wake.
Ni fundisho kwetu kuangalia namna ambavyo tunawatendea wenye shida wote ambao kupitia kwetu wanaitamani huruma ya Mungu. Mwanadamu anayeteseka katika namna mbalimbali anategemea huruma ya Mungu impatie uponyaji na mwenyezi Mungu anatenda kupitia mimi na wewe katika matendo yetu ya ukarimu. Daima anaimba na Mzaburi akisema: “Ndiwe sitara yangu, utanihifahi na mateso, utanizungusha nyimbo za wokovu”. Je! Upi ni mwitikio wetu? Je, tunafuata upande wa Kristo kwa kuwakaribia na kuwaganga au tunawaona kuwa ni waliopoteza na hivyo kuwaacha huku tukisema: “pambana na hali yako?”
Dhambi inastahili kabisa kurandanishwa na ukoma wa kiroho. Mwenye ukoma anapoteza kabisa hisia. Hivyo ndivyo kwa mdhambi. Anakosa hisia kabisa ya wema wa Mungu kwa sababu amejitenga naye na amejiwekea ulimwengu wake. Hii ni kwa sababu tunapotenda dhambi tunajitenga na upendo wa Mungu na pia wanadamu wenzetu. Kwa uhalisia dhambi ni tukio la kibinafsi na bila mmoja kuitaja waziwazi au kushuhudiwa, atabakia katika hali hiyo na pengine kuifurahia au kuiona kama jambo la kawaida. Kwa maneno mengine dhambi ni jambo ambalo linamtaka mwanadamu kuwa mkweli ndani ya dhamiri yake na kujitangaza kwa matendo ya toba kuwa ni mdhambi huku akiichuchumilia huruma ya Mungu. Katika muktadha wa jamii yetu leo hii, jamii ambayo imeathiriwa vibaya na ulegevu wa kiimani tunaona changamoto kubwa sana ya watu kuuona huu ukoma ndani mwao na kutafuta tiba kwa Kristo. Hii ni changamoto nyingine, yaani, pamoja na kufunuliwa njia za uponyaji zinazoidhihirisha huruma ya Mungu wengi wanakimbia na kuloea katika ukoma wao wa kiroho.
Pengine watu wanaona fahari kutembea na ukoma huu na wanafikia hatua mbaya zaidi ya kuuona kuwa si ugonjwa bali ni jambo la kawaida. Tuchukulie mathalani suala la rushwa ambalo Baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Nyerere aliifananisha na ukoma. Matendo ya rushwa katika ujumla wake yanauondoa utu wa mtu. Hii inawaathiri pande zote mbili. Yule anayeyafurahia anapoteza hadhi ya utu kwa kukosa upendo kwa jirani na kwa upande mwingine yeye anyonywaye anageuzwa kuwa kama bidhaa au mahali pa kujichotea utajiri kwa mwingine. Lakini katika uhalisia wa mazingira yetu ambayo yanapoteza kwa kasi chachu ya uwepo wa Mungu kati yao hakuna anayegutuka wala kuguswa na ukoma wa namna hii. Mbaya zaidi tunaendelea kuwakumbatia na kuwatukuza wapokea rushwa bila hata kushituka au kuona uchungu.
Hali hii inahitaji hatua za ziada. Jamii ya waamini inapaswa kufanya bidii katika kuamsha dhamiri za watu na kuimarisha imani yao. Kipindi cha Kwaresima ambacho karibu tunakianza ni majira ya neema ambayo kwayo tunapaswa kuionja neema ya Mungu. Hivyo tujiandae vyema kwa kutafakari mioyoni mwetu kile ambacho ni ukoma kwako: pengine ni uzinzi au uvivu, au unyonyaji au ukatili au mauaji ya nafsi za watu kiroho na kimwili au namna yoyote ambayo inauondoa urafiki wako na Mungu na pia urafiki wako na wenzako.
Mtume Paulo anatupatia njia ya kufuata akisema: “mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo”. Ni mwaliko wa kutenda yote kwa kadiri ya mapenzi ya Mungu. Anatukumbusha kuepuka kufanya mambo ili kuwafurahisha wanadamu na tamaa zetu za kimwili kwani hayo ndiyo hututenga na Mungu na kutufumba macho yetu tusiuone wema wake. Mwanadamu hutumbukia katika dhambi si kwa kuisikiliza sauti ya Mungu na maongozi yake bali ni pale anapojitenga naye au kutompatia nafasi yake stahiki. Mla Rushwa kamwe hanuii kumtukuza Mungu bali kuhifadhi utukufu wake; mzinzi kamwe hayuko katika kutimiza mapenzi ya Mungu bali hamu na mihemuko ya mwili wake; mmbea na mchonganishi atarajii kumsifu Mungu bali ni katika kujisafisha mbele za watu. Wadhambi wote wanafanya mambo yao kwa ajili ya utukufu na ufahari wao. Tupokee kwa unyenyekevu mahusia haya ya kitume: “Fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu”, na hapo ndipo tutapata fursa ya kujitakasa ukoma wetu na kuungana wa wote. Ninawatakieni maandalizi mema ya kipindi cha Kwaresima.

SALA: Ee Yesu utukinge na ukoma wa kiroho.