Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 19/05/2024

2024 MEI 19 : SHEREHE YA PENTEKOSTE

Rangi: Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku

Somo 1. Mdo 2:1-11

Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.  Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya?  Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelami, nao Wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.

Wimbo wa Katikati. Zab 104:1, 24, 29-31, 34

1. Ee nafsi yangu umhimidi Bwana,
     Wewe, Bwana, Mungu wangu,
     Umejifanya mkuu sana;
      Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
      Dunia imejaa mali zako.

(K)Waipeleka roho yako, Ee Bwana, Nawe waufanya upya uso wa nchi.

2. Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
      Na kuyarudia mavumbi yao,
      Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
      Nawe waufanya upya uso wa nchi. (K)

3. Utukufu wa Bwana na udumu milele;
      Bwana na uyafurahie matendo yake.
      Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake;
      Mimi nitamfurahia Bwana. (K)

Somo 2. 1 Kor 12:3b-7, 12-13

Hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.

Injili. Yn 20:19-23

Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye  akiisha kusema hayo, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu  akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.

TAFAKARI

ROHO MTAKATIFU NI MTENDAJI NDANI YETU
Siku hamsini baada ya Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo na siku kumi baada ya kupaa kwake Mama Kanisa anatualika kusherehekea sherehe ya Pentekoste. Neno Pentekoste lina asili yake katika lugha ya kiyunani πεντηκοστή (likitamkwa “pentekostee”) ambalo linamaanisha siku ya hamsini. Sherehe ya Pentekoste ina asili yake katika dini ya kiyahudi ambapo walifanya shukrani ya mazao kwa Mungu siku hamsini baada ya pasaka ya kiyahudi (rej. Kut 23:16; Law 23:24, 42- 43). Sherehe hii iliyojulikana kwa jina la “Shavout” au sherehe ya majuma au vibanda ilikuwa pia ni kumbukumbu ya tukio la kupewa Amri Kumi (10) za Mungu mlimani Sinai. Hii ilikuwa ni sherehe wakati wa kipindi cha kuchepuka, sherehe ambayo iliashiria mwanzo mpya wa maisha. Majira ya baridi yanayotangulia kipindi hiki yana tabia ya kuonesha ufu. Mimea mingi hupoteza majani yake mithili ya mmea unaokauka. Lakini majira ya mchepuke huleta matumaini mapya na mwanzo mpya.
Kwetu sisi Wakristo sherehe hii ya siku hamsini baada ya ufufuko wa Kristo ni adhimisho la tukio la Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume. Kabla ya kupaa mbinguni, Bwana wetu Yesu Kristo aliwapatia ahadi mitume ya kumpokea Roho Mtakatifu na ndipo watoke na kwenda kumshuhudia. Ujio huu wa Roho Mtakatifu unafanya kuzaliwa kwa Kanisa jamii mpya ya wanadamu inayoongozwa katika Sheria ya Kristo. Sheria hiyo inawezeshwa katika Roho Mtakatifu. Mtakatifu Ireneo wa Lyon alisema: “kama vile isivyowezekana kwa unga kufinyangwa na kufanya mkate bila tone la maji ndivyo isivyowezekana kwetu sisi kufanyika upya katika Kristo bila uwepo wa Roho Mtakatifu.” Jumuiya mpya ya mwanadamu inayoundwa na Kristo inawezeshwa na Roho Mtakatifu: “Waipeleka Roho yako, Ee Bwana, nawe waufanya upya uso wa nchi.” Hivyo adhimisho hili kila mwaka kama ilivyo kwa Wayahudi linapaswa kuwa chemchemi mpya na chimbuko la maisha mapya ya kikristo.
Leo hii tunauona ujio huu wa Roho Mtakatifu katika Kanisa ambalo limejengwa kwa msingi wa mitume. Msingi huo ni Kristo mwenyewe ambaye ni Jiwe kuu la pembeni. Matendo makuu ya Mungu yamefunuliwa kwetu katika nafsi ya Kristo. Ni Yeye ambaye ametuondoa utumwani na kutupatia mfano wa maisha mapya. Baada ya kupaa kwake mbinguni alituagiza kuyashuhudia matendo hayo. “Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakisema matendo makuu ya Mungu, Aleluya!” Matendo haya yalikuwa yananenwa kwa namna ya maisha. Maisha ya aliyejazwa Roho Mtakatifu yanafunua matendo makuu ya Mungu. Hapa tunauona wito wa utakatifu ambao Kristo anatupatia, wito ambao tunautimiza vema tunapounganika na Roho Mtakatifu. Yeye anatuelekeza mpango wa Mungu uliofunuliwa kwetu katika Kristo na kutupatia ujasiri wa utekelezaji wake. Muunganiko huu thabiti na Mungu ndiyo utakatifu wa maisha ya kikristo. Watakatifu ni rafiki za Mungu; wale ambao wameunganika naye kuyatenda mambo yake makuu.
Roho Mtakatifu anapotupatia utakatifu huo ambao unatokana na upya wa maisha tuupatao katika Kristo anatusaidia pia kujua maana ya kila sauti: “Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inaviunganisha viumbe vyote, hujua maana ya kila sauti, Aleluya!” Katika somo la kwanza muujiza huo na utendaji huo wa Roho Mtakatifu unaonekana kwani watu walielewa kila kitu katika lugha yao. Watu katika Yerusalemu walistaajabishwa kwa kusema: “Inakuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?” Maana yake nini maneno haya? Tunaweza kuyaelewa kwa tafakari mbalimbali kama ile hali ya kupata utambuzi wa kimungu na kuelewa maana na faida ya karama mbalimbali katikati ya jamii ya mwanadamu. Utambuzi huu unaeleweka kwa kila mmoja katika muktadha wake kwa ajili ya kukidhi haja yake. Inaelezea utajiri wa karama tofauti tunazojaliwa na mwenyezi Mungu katika kutajirishana. Pato hili ni muhimu kwetu kwanza kwa kujali na kuheshimu kila mmoja kwa nafasi yake kwa ajili ya faida ya wote na pili kwa kutupatia hamasa ya kuitendea haki na kuigawa karama tuliyopewa kwa ajili ya faida wa wengine. Hii ni kwa sababu “pana tofauti ya karama; bali Roho ni yeye yule.”
Jumuisho ya hayo yote tunayoyapata hapo juu kutoka kwa Roho Mtakatifu huonekana katika kutufanya kuwa wamoja. Tunda la Roho Mtakatifu ni kutufanya kuwa ndugu. Sakramenti ya Ubatizo ambayo inatuingiza katika kundi la wana warithi wa Mungu huwezeshwa na Roho Mtakatifu. “Hawezi mtu kusema Yesu ni Bwana isipokuwa katika Roho Mtakatifu… kukiri huko kwa imani kwawezekana tu katika Roho Mtakatifu… kwa nguvu ya ubatizo wetu, Sakramenti ya kwanza ya imani, uzima ambao una chemchemi yake katika Baba, na ambao umetolewa kwetu katika Mwana; unashirikishwa kwa ndani kabisa katika nafsi ya mtu na Roho Mtakatifu katika Kanisa” (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, namba 683). Roho Mtakatifu anapotuunganisha na Mungu na hivyo kutufanya kuwa wana warithi wa Mungu anatuunganisha sisi kwa nini. Undugu wetu uliopo katika Kristo unapata msingi wake katika Roho Mtakatifu.
Hivyo leo pia hatuna budi kusherehekea umoja wetu ambao kwa njia yake tutaendelea kuheshimiana, kujaliana, kusaidiana na kuimarisha mahusiano ya kiutu kati yetu. Tunapoishi katikati ya jamii ambayo inabariki na kushabikia utengano baina ya mtu na mtu na uharibifu mkubwa wa haiba na utu wa mwanadamu, changamoto inawekwa kwetu sisi Wakristo; sisi ambao kwa ubatizo wetu tumempokea Roho Mtakatifu na kwa namna ya pekee tukaimarishwa kwa mapaji yake saba wakati wa Sakramenti ya Kipaimara. Changamoto hiyo ni kudhihirisha upya wa maisha tulioupata, upya ambao umetufanya kuwa rafiki wa Mungu kwa kutenda matendo yake na hivyo kuwa wamoja katika Kristo. Itakuwa ni sikitiko kwa jamii ya mwanadamu na ubinadamu kwa ujumla tutakapoififisha sauti ya Roho Mtakatifu.
Mara nyingi tunaelemewa sana na maelekeo ya Dunia mambo leo na kumuweka Roho Mtakatifu chemba. Mara ngapi tunashindwa kuonesha upendo, huruma, kusaidiana na kusameheana ndani ya familia zetu? Je, matendo hayo hurandana na matendo makuu ya Mungu? Mara ngapi tunafurahia au kuhusika katika dhuluma kati ya jamii moja au nyingine? Familia moja na nyingine? Imani moja na nyingine? Kwa hakika haya si matendo makuu ya Mungu. Kama tunafanyika kuwa watoto wa Mungu vinasaba vyetu vinapaswa kububujika yale yatokayo kwake, ambayo tunayapata kwa njia ya Kristo tukiwezeshwa na Roho Mtakatifu. Kristo katika Hekima yake ya kimungu alituahidia Roho Mtakatifu aliye nguvu, mwangaza, mtakasaji na anayetukumbusha kila mara. Tuifungue mioyo yetu ili kuisikiliza sauti yake na hivyo kuwa kweli mashuhuda wa Habari njema ya Wokovu kwa mwanadamu.

SALA: Njoo Roho Mtakatifu utupatie mapaji yako saba yafanye kazi ndani yetu.