Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 17/05/2024

2024 MEI 17 : IJUMAA-JUMA LA 7 LA PASAKA

Mt. Paskali Bayloni, Mtawa Mfransisko
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Mdo 25:13-21

Siku zile, Agripa mfalme wa Bernike walifika Kaisaria, wakimwamkia Festo. Na walipokuwa wakikaa huko siku nyingi, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni; ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake. Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika mashitaka yake. Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumunikaamuru mtu huyo aletwe. Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama nilivyodhani, bali walikuwa na maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika habari ya mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema kwamba yu hai. Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya. Lakini Paulo alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru alindwe hata nitakapompeleka kwa Kaisari.

Wimbo wa Katikati. Zab 103:1-2, 11-12, 19-20

1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.

(K)Bwana ameweka kiti chake cha enzi Mbinguni.

2. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. (K)

3. Bwana ameweka kiti chake cha enzi Mbinguni,
Na ufalme wake unavitawala vitu vyote.
Mhimidini Bwana, enyi malaika zake,
Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake,
Mkiisikiliza sauti ya neno lake. (K)

Injili. Yn 21:15-19

Walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohane, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda.  Akamwambia, Lisha wanakondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohane wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda.  Akamwambia, Chunga kondoo zangu.  Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohane, wanipenda?  Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu. Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka.  Akasema neno hilo kwa kuonesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu.  Naye akiisha kusema hayo, akamwambia, Nifuate.

TAFAKARI

UPENDO NDIYO KIINI CHA HUDUMA: Katika Injili ya leo Yesu anakutana na wanafunzi wake; na anafanya mazungumzo na Petro akimuuliza mara tatu kama anampenda. Baada ya kujibu mara ya tatu kuwa anampenda anampa kazi ya kulisha kondoo. Hii inamaanisha kuwa ili kuweza kuwatumikia watu nyenzo muhimu inayotakiwa ni upendo. Tuwaombee Mapadre wetu ambao wamekabidhiwa jukumu la kuwalisha na kuwachunga kundi la Bwana watimize wajibu huo kwa upendo. Tuwaombee wawe wachungaji kweli kama Yesu wawatafute wale waliopotea na kuwarudisha zizini. Petro alijifahamu na alifahamu mapungufu yake lakini alisisitiza upendo wake kwa Yesu. Yesu hakutazama yale mapungufu bali alitazama ule uwezo wake wa kupenda na akaamuru Petro awashirikishe watu wake upendo huo. Katika huduma zetu mbalimbali tuwe na mtazamo chanya zaidi badala ya mtazamo hasi unaotazama mapungufu tu. Pamoja na kwamba Petro alimkana Yesu mara tatu sasa anaungama kosa hilo mara tatu na hivyo anachaguliwa kutoa huduma zile alizokuwa anatoa Yesu.
Sala: Ee Yesu utujalie tukupende kwa dhati licha ya madhaifu yetu.