Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 16/05/2024
2024 MEI 16 : ALHAMISI-JUMA LA 7 LA PASAKA
Mt. Simoni Stock
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 3
Somo 1. Mdo 22:30; 23:6-11
Wakati ule Jemadari alitaka kujua hakika, ni kwa sababu gani Paulo ameshitakiwa na Wayahudi, akamfungua, akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza yote wakutane. Akamleta Paulo chini, akamweka mbele yao. Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu. Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindano baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana. Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; Bali Mafarisayo hukiri yote. Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, wakisema, hatuoni uovu wowote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema naye, ni nini? Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao, akaamuru askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome. Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako. |
Wimbo wa Katikati. Zab 16:1-2a, 5, 7, 11
1. Mungu unihifadhi mimi, (K)”Mungu unihifadhi mimi, 2. Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri, 3. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, 4. Utanijulisha njia ya uzima; |
Injili. Yn 17:20-26
Siku ile, Yesu alisali akisema: Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi. Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu. Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma. Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao. |
TAFAKARI
UMOJA WETU NA KRISTO: Injili ya leo inatupa sehemu ya mwisho ya sala ya Yesu kwa wafuasi wake akiwaombea umoja. Umoja anaotuombea Yesu ni umoja katika upendo. Utengano mkubwa uliopo duniani kati ya taifa na taifa, au dini moja na dini nyingine ni matokeo ya kukosekana kwa umoja kati yao. Tunapotafakari umoja aliotuombea Kristo, tujitazame ni kwa namna gani sisi Wakristo tunakumbatia umoja au utengano. Ni ajabu sana kwa watu wanaokiri kuwa Yesu ni Mwokozi na wakati huohuo hawana umoja kati yao. Wabatizwa wote tuwe mabalozi wa kutetea na kulinda umoja wetu pasipo kujali madhehebu yetu. Tuungane kama wanakanisa kila tarehe 18-25 Januari kila mwaka kuomba umoja wa Wakristo, ili kuenzi kile alichotuombea Yesu. Tukumbuke Wahenga walisema “umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.” Tuweke nguvu zetu pamoja katika kumtangaza Kristo ili Habari Njema iweze kuwafikia watu wote. SALA: Ee Yesu utujalie wafuasi wako umoja ili tuwe na nguvu ya pamoja katika kukushuhudia. |