Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 05/05/2024

2024 MEI 5 : DOMINIKA YA 6 YA PASAKA

Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 

Somo 1. Mdo 10: 25-26, 34 -35, 44-48

Petro alipokuwa akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguu, akamsujudia. Lakini Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu. Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye. Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno. Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu, Ni nani awezaye kukataza maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi? Akaamuru wabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha.

Wimbo wa Katikati. Zab 98: 1 – 4

“1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)

2. Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)

3. Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)”

(K) Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.

Somo 2. 1 Yoh 4: 7 -10

Wapenzi, na tupendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.

Injili. Yn 15: 9-17

Yesu aliwaambia wafuasi wake: Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe. Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana.

TAFAKARI

“FURAHA YA KWELI INAPATIKANA KATIKA KRISTO
Hati ya kichungaji ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vaticano juu ya Kanisa katika ulimwengu mamboleo «Furaha na Matumaini (Gaudium et Spes) »inasema hivi: “Ukweli ni kwamba katika fumbo la Neno la Mungu kufanyika mwili ndipo fumbo la mwanadamu linafumbuliwa. Hii ni kwa sababu Adam, mwanadamu wa mwanzo kabisa alikuwa taswira ya yeye Kristo Yesu ambaye alipaswa kutujia. Kristo ambaye ni Adam wa mwisho amemfunulia mwanadamu ukweli kuhusu asili yake na ukweli juu ya wito wake mkuu kwa kuufunua upendo wa Baba na upendo wake” (Namba 22). Sehemu hii ya waraka wa Mtaguso inanuia kutuonesha tija ya fumbo la umwilisho ambalo kwalo majawabu mengi kuhusiana na changamoto zinazomkabili mwanadamu hupata majawabu yake. Moja ya changamoto hizo ni furaha. Ni ipi iliyo furaha ya kweli?
Kiuhalisia mwanadamu anatamani kuwa katika hali ya furaha daima lakini je, ni ipi iliyo kwake furaha ya kweli na ya kudumu? Furaha ya kweli inapatikana katika Kristo. Mtakatifu Bernadetha Subiru aliambiwa na Mama Bikira Maria kwamba anamuahidi furaha lakini si katika maisha ya ulimwengu huu bali maisha ya baadaye. Kristo anatuambia katika Injili ya leo: “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.” Hivyo mambo mawili yanawekwa wazi kama nyenzo ya kuifikia furaha kamilifu, yaani kuzishika amri za Mungu na kukaa katika pendo la Mungu.
Utimilifu wetu wanadamu unapatikana katika kuungana na Kristo. Dhana hii imetafakariwa kwa kirefu katika Dominika mbili zilizopita ambapo Kristo alijitanabaisha kama Mchungaji wa Kondoo na mzabibu wa kweli. Fumbo la umwilisho kama nilivyodokeza hapo mwanzoni limeweka wazi ukweli kuhusu mwanadamu na ukweli huo unajionesha katika muunganiko kamilifu na Kristo na kwa njia yake na Mungu Baba. Muunganiko huo hutekelezwa kwa njia ya kuzishika amri za Mungu ambazo ndizo miongozo na kanuni za kuipata furaha ya kweli na inayodumu. Hakuna kitu chochote kinachoweza kuwa katika ukamilifu bila kufuata kanuni za kuundwa kwake. Gari likiacha kufuata kanuni za kuundwa kwake matairi yakagoma kwenda au breki zikaacha kukamata sawasawa au taa ya kuashiria kulia au kushoto ikaacha kuwaka matokeo yake ni majanga na uharibifu. Hivi ndivyo kwetu sisi wanadamu. Hatukujiumba au kujileta duniani kwa utashi wetu wenyewe. Tunapoacha kuunganika na Yeye aliyetufanya kwa kuendana na kanuni anazotuwekea tunaingia katika ukengeufu na mwisho ni majanga.
Changamoto tuipatayo katika ulimwengu mamboleo ni kuenea kwa uhuru wa mwanadamu katika kutafuta auheni ya maisha na furaha. Namna hii imetuondoa katika kulitazama neno la Mungu na matokeo yake tunajitafutia namna zetu kadiri ya vionjo vyetu na misukumo ya kibinadamu. Matokeo yake ni dhahiri: ni anguko kwa mwanadamu na udhalilishaji wa utu wa mtu. Uhuru tunaojivika unamithilika na uhuru bandia kwani wengi hujikuta tumeingia katika misukosuko na matatizo mengi badala ya kupata uhuru wa kweli. Kristo ambaye ni ufunuo wa uhuru wa kweli katika kutafuta furaha ya kudumu ametufundisha bustanini Getsemani namna ya kuonesha uhuru wako hali umeunganika na mapenzi ya Mungu, yaani amri zake. Akiwa katika hali ya huzuni kubwa kiasi cha kutokwa na jasho la damu alisali akisema: “Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke” (Lk 22:42). Kama binadamu anatamani kupata faraja na furaha ya kudumu lakini akiwa ameunganika na Baba yake anataka kuipata furaha hiyo kadiri ya mapenzi yake.
Tunapoitafuta furaha bila kuunganika na Mungu tunaishia katika furaha za muda mfupi. Hili kwa namna ya pekee huonekana katika furaha tuitafutayo kwa kuwatumia wenzetu kama vyombo. Ni namna ambavyo mwanadamu anafumba macho na kutoona muunganiko wa asilia uliopo kati yake na ndugu yake pembeni yake na hivyo kumweka mbele yake kama chombo cha kujinufaisha na kuifurahisha nafsi yake. Namna hii kamwe haitupatii furaha ya kweli. Hata tukijidanganya kwa kusema kila mmoja ahangaike na hali yake lakini bado damu yake itakuita tu. Unyonyaji, manyanyaso, mateso na uhasi mwingine dhidi ya mwanadamu mwenzako hukurudia mwenyewe tu. Nahau ya kiingereza isemayo what goes around comes around itugutushe katika hilo.
Ndiyo maana Kristo anaipanua namna ya kuufanya upendo wetu utupatie furaha ya kudumu: “Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” Furaha yetu ya kweli inaonekana kwanza katika mwelekeo wa upendo kwa Mungu na pili katika mwelekeo wa upendo wetu kwa jirani. Kristo anaendelea kuwa kielelezo kwetu kwa namna hiyo kama anavyofafanua Mtume Yohane katika somo la pili la Dominika hii. Hii namna ya kujitoa nafsi yako, kujisadaka kwa ajili ya wenzako. Sehemu hiyo ya Maandiko matakatifu inapigia mstari dhana ya Mungu kuwa asili au sababu ya yote ayatendayo mwanadamu. Upendo wetu kwa wenzetu asili yake si sisi; asili yake tunapaswa kuiona katika Mungu: “Wapenzi na tupendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mngu.” Hivyo namna yoyote ya upendo kati yetu sisi kwa sisi inapaswa kuchipuka katika Yeye kupitia Kristo Bwana wetu.
Upendo huo ambao unapata asili yake katika Mungu unatutajirisha zaidi kwa kuunganika na watu wote na pia kuona utendaji wa Mungu katika kila kazi njema ya mwanadamu. Petro anapoingia nyumbani kwa Kornelio anatamka kwa ujasiri akisema: “hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.” Petro amefanya tamko hilo baada ya maono aliyoyapata katika aya zilizotangulia somo la leo, aya ambazo zilimfunulia namna utendaji Mungu unavyotenda kazi kwa wanadamu wote. Kristo anayeufunua ubinadamu wetu katika hali yake stahiki anaugusa ubinadamu wote na yeyote anayeifuata njia yake kwa njia ya neema ya Mungu ataweza kumtukuza Mungu na hivyo kuingia katika kundi la wale wanaozishika amri zake na hivyo sote tutaipata furaha ya kweli.
Hivyo tuitikie wito wa Kristo katika hitimisho la Injili ya leo. Yeye anatutaka tuendelee kubaki katika urafiki na Yeye kwa kusikiliza na kuliishi lile analotufundisha. Hali hiyo itatufanya kuwa wana huru na si watumwa. Hii ni kwa sababu kwa kulisikiliza Neno lake tutayafahamu yale anayotuamuru kufanya na yale anayoyatenda lakini “mtumwa hajui atendalo bwana wake.” Ni wito wa kujitajirisha na habari za ufalme wa Mungu kwa kuisikiliza sauti ya Kristo ambaye anatuambia yote anayoyasikia kwa Mungu Baba aliye chanzo na maana ya ubinadamu wetu na pia chimbuko la furaha yetu ya kweli.”

SALA: Ee Kristo Mfufuka utujaze furaha katika upendo wako.