Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 13/05/2024
2024 MEI 13 : JUMATATU-JUMA LA 7 LA PASAKA
Bikira Maria wa Fatima
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 3
Somo 1. Mdo 19:1-8
Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohane. Paulo akasema, Yohane alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye anayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri. Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili. Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akahojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu. |
Wimbo wa Katikati. Zab 68: 2-7
1. Mungu huondoka, adui zake wakatawanyika, (K) Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu. 2. Bali wenye haki hufurahi, 3. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, |
Injili. Yn 16:29-33
Wanafunzi walimwambia Yesu: Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yo yote. Sasa tumejua ya kuwa wewe wafahamu mambo yote wala huna haja ya mtu akuulize; kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu. Yesu akawajibu, Je! Mnasadiki sasa? Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami. Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu. |
SALA: Ee Yesu naomba unilinde dhidi ya mwovu shetani. |
TAFAKARI
PAMOJA NA KRISTO TUTASHINDA YOTE: Katika Injili ya leo wanafunzi wa Yesu wanakiri kwa vinywa vyao kwamba wamemwelewa Yesu na kuwa ametoka kwa Mungu. Kwa upande mwingine Yesu anaweka wazi kuwa kwa sababu ya ufuasi, watapata mahangaiko mengi duniani, ila wasife moyo kwani yeye ameshaushinda ulimwengu. Kwa sadaka aliyotoa kwa upendo mkubwa ameushinda ulimwengu wa Ibilisi. Hivyo anatoa mwaliko kwetu pia kushiriki katika mapambano na hivyo kuleta ushindi dhidi ya Ibilisi. Wapendwa familia ya Mungu, tupo katika mapambano ya maisha ya kiroho. Vita yetu ni dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho, dhidi ya watawala wanaomiliki ulimwengu wa giza. Jemedari wetu ni Yesu na ametuambia wazi kuwa ameushinda ulimwengu. Tuendeleze mapambano haya kwa njia ya sala na matendo mema ili msingi mzuri alioweka Jemedari wetu utufae katika vita hii. Tuvae ujasiri na matumaini katika mapambano haya tukitambua kuwa Yesu yupo nasi daima. |