Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 14/05/2024

2024 MEI 14 : JUMANNE-JUMA LA 7 LA PASAKA

MT. MATHIA MTUME
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Mdo 1:15-17, 20-26

Siku zile Petro alisimama kati ya ndugu zake (jumla ya majina ilipata mia na ishirini), akasema, Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi, katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu, kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii. Kwa maana imeandikwa katika chuo cha Zaburi,  Kikao chake na kiwe ukiwa, Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo; tena usimamizi wake autwae mwingine. Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, kuanza tangu ubatizo wa Yohane, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi. Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya. Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuoneshe ni nani uliyemchagua katika  hawa wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe. Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.

Wimbo wa Katikati. Zab 113:1-8

1. Aleluya.
    Enyi watumishi wa Bwana, sifuni,
    Lisifuni jina la Bwana.
    Jina la Bwana lihimidiwe
    Tangu leo na hata milele.

(K)”Amketishe pamoja na wakuu,
pamoja na wakuu wa watu wake. “

2.  Toka mawio ya jua hata machweo yake
      Jina la Bwana husifiwa.
      Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote,
      Na utukufu wake ni juu ya mbingu. (K)

3.    Ni nani aliye mfano wa Bwana,
      Mungu wetu aketiye juu;
     Anyenyekeaye kutazama,
     Mbinguni na duniani? (K)

4.   Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
      Na kumpandisha maskini kutoka jaani.
      Amketishe pamoja na wakuu,
      Pamoja na wakuu wa watu wake. (K)

Injili. Yn 15:9-17

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe. Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi mpate kupendana.
SALA: Ee Yesu naomba uniongezee fadhila ya mapendo.

TAFAKARI

KIPIMO CHA UPENDO WA KWELI NI YESU: Leo tunaadhimisha sikukuu ya Mtakatifu Matia mtume. Kama ilivyo kawaida kwa mitume na mashahidi wengine, damu yake imekuwa mbegu ya imani yetu, kwani kwa kumwaga damu yake kwa ajili ya kushuhudia imani, imani yetu imeimarika zaidi. Huyu alibaki katika muungano na Yesu na kushika amri ya upendo kwa Mungu kama Yesu alivyofundisha. Katika Injili ya leo Yesu anatufundisha kuwa kipimo cha upendo wa kweli ni yeye. Katika Agano la Kale imeandikwa umpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe (rej. Law 19:18). Yesu anakamilisha amri hii kwa kutuonesha kuwa kipimo cha upendo ni yeye. Alitupenda upeo mpaka akakubali kufa msalabani kwa ajili yetu. Ili kuwa na muungano wa upendo wa kweli ni lazima kutenda yale anayotuelekeza Yeye. Kupitia Kristo tumefunuliwa siri za ufalme wa Mbinguni na hakuna kilichofichika kwetu, hivyo tutumie ufunuo huo wa Kristo ili tuweze kufika kwa Baba. Yesu ametupenda na akatupa utume wa kuzaa matunda yadumuyo.