Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 15/05/2024

2024 MEI 15 : JUMATANO-JUMA LA 7 LA PASAKA

Mt. Isidori Mkulima
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Mdo 20:28-38

Paulo aliwaambia wakuu wa Kanisa la Efeso: Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha Kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwamwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao. Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi. Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa. Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea. Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote. Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusu-busu, wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.

Wimbo wa Katikati. Zab 68:29-30, 33-36

1. Ee Mungu, uziamuru nguvu zako;
Ee Mungu, uwe hodari uliyetufanyia makuu.
Kwa ajili ya hekalu lako Yerusalemu
Wafalme watakuletea hedaya.

(K)Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu.

2. Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu,
Msifuni Bwana kwa nyimbo.
Apandaye mbingu za mbingu za tangu milele;
Aitoa sauti yake, sauti ya nguvu.
Mhesabieni Mungu nguvu. (K)

3. Enzi yake i juu ya Israeli
Na nguvu zake zi mawinguni.
Mungu ni mwenye kutisha
Kutoka patakatifu pako.
Ndiye Mungu wa Israeli;
Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo.
Na ahimidiwe Mungu. (K)

Injili. Yn 17:11-19

Siku ile, Yesu alisali akisema:  Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.  Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.  Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu.  Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.  Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni.  Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli.

TAFAKARI

MUNGU NI CHANZO YA UMOJA WETU: Leo katika Injili Yesu anawaombea wafuasi wake, kwani anawaaga na baada ya muda mfupi hatakuwa nao tena. Wafuasi wataendelea kuwepo na watakumbana na mateso na mahangaiko mengi. Kutokana na hili Yesu anawaombea ili furaha yao katika kuungana na Kristo ikamilike. Wanapaswa kuishi ulimwenguni bila kuwa wa ulimwengu yaani bila kufuata mkondo wa walimwengu. Kwa ubatizo wetu sisi tunaomwuungama Kristo, kama yeye na pamoja naye tunapaswa kuishi na kuwa na mwelekeo tofauti na walimwengu. Tunapaswa kuvaa ujasiri wa kuishi maisha ya ushuhuda kwa kuushuhudia ukweli. Kwa mfano kama ulimwengu au Taifa linasema kutoa mimba ni sahihi, tuwe nuru na kuonesha kuwa siyo sawa. Kama mkondo wa ulimwengu ni kukubali mahusiano ya jinsia moja tuvae ujasiri wa kusema hapana kwani ni kinyume na mpango wa Mwenyezi Mungu. Kwa kufanya hivyo tutatoa sauti ya kitume na kinabii na kuonesha kuwa tupo ulimwenguni ila sisi siyo wa ulimwengu.