Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 17/04/2024

2024 APRILI 17 : JUMATANO-JUMA LA TATU LA PASAKA

Mt. Mt. Stefano Harding, Abate
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Mdo 8:1-8

Siku ile kulitukia adha kuu ya Kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu Kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule.

Wimbo wa Katikati. Zab 66:1-7

“1. Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
Imbeni utukufu wa jina lake,
Tukuzeni sifa zake.
Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini! (K)

2. Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,
Naam, italiimbia jina lako.
Njoni yatazameni matendo ya Mungu;
Hutisha kwa mambo awatendeayo wnadamu. (K)

3. Aligeuza bahari kuwa nchi kavu;
Katika mto walivuka kwa migoo;
Huko ndiko tulikomfurahia.
Atawala kwa uweza wake milele;
Macho yake yawaangalia mataifa;
Waasio wasijitukuze nafsi zao. (K)”

(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.

Injili. Yn 6:35-40

Yesu aliwaambia: Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe. Lakini naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini. Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho. Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.

TAFAKARI

KAZI YA MUNGU HAIZUILIKI: Katika Injili Yesu anasema, alikuja ili ayafanye mapenzi ya Baba yake wa Mbinguni ambayo ni kumkomboa mwanadamu na kumfufua kwa uzima wa milele siku ya mwisho. Kazi hii ya ukombozi ndio hiyo tuliyoishuhudia mitume wakiitekeleza kwenye somo la kwanza, japo Stefano aliuawa, lakini hili halikuweza kuzuia mpango wa Mungu, bado tunaelezwa kuwa mitume walikuwa na ujasiri wa kumtangaza Kristo ijapokuwa Sauli alikuwa tishio. Kanisa Katoliki halipaswi kuogopa vitisho vya siasa na wavamizi mbalimbali. Tangu wakati huo hadi sasa Wakristo sehemu mbalimbali za dunia wamekuwa wakidhulumiwa na kuuawa. Lakini jambo la uhakika ni kwamba “wala milango ya kuzimu haitalishinda”(Mt 16:18). Hivyo tusikate tamaa tunapokutana na magumu ya kimisionari, Kristo Mfufuka ametuahidia ushindi.

SALA: Ee Mungu utujaze Roho Mtakatifu ili tusikate tamaa hata katika misukosuko ya kiimani.