Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 14/04/2024

2024 APRILI 14 : DOMINIKA YA 3 YA PASAKA

Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Mdo 3: 13-15, 17-19a

Petro aliwaambia watu wote: Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu; ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule mtakatifu, yule mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake. Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda. Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe.

(K) Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.

Wimbo wa Katikati. Zab 4: 2, 7 – 9

“1. Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo;
Umenifanyizia nafasi wakati wa shida;
Unifadhili na kuisikia sala yangu. (K)

2. Bali jueni ya kuwa Bwana amejiteulia mtauwa;
Bwana atasikia nimwitapo. (K)

3. Wengi husema, Nani atakayetuonesha mema?
Bwana, utuinulie nuru ya uso wako. (K)

4. Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara,
Maana wewe, peke yako Bwana, peke yeko,
Ndiwe unijaliaye kukaa salama. (K)”

Somo 2. 1 Yoh 2: 1- 5a

Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote. Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu amekamilika kweli kweli.

Injili. Lk 24: 35- 48

Wafuasi waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate. Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu. Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho. Akawaambia, mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikeni shikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo. Na baada ya kusema hayo aliwaonesha mikono yake na miguu yake. Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, mna chakula chochote? Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akala mbele yao. Kisha akawaambia, hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa ningali pamoja nanyi. Ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii, na Zaburi. Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo hayo.

TAFAKARI

“HAKUNA TENA HOFU, KWELI AMEFUFUKA! TUKAMSHUHUDIE
Mwinjili Luka anaendelea kutusimulia jinsi Kristo Mfufuka anavyowatokea wafuasi wake. Na leo anawatokea wakiwa Yerusalemu wamejifungua kwa woga, hofu na wasiwasi. Na katika hali hiyo Yesu anawaambia “”Amani iwe kwenu.”” Najaribu kufikiria kwamba Kristo Mfufuka angekuwa ametokea katika kundi la watu wasio na imani ambao wako ndani wamejifungia wakiendelea na shughuli zao. Au tuseme mtu maarufu amefariki na baada ya siku tatu akawatokea kundi la watu, mfano familia yake, je, hali yao ingekuwaje? Kwanza wangesema wameona mzimu. Pili wangehama mahali hapo kwa muda. Tatu wangeenda kwa mganga wa kienyeji ili afanye kitu fulani kutakasa mahali hapo. Na huenda wangefanya tambiko ili kutuliza huyo mzimu asitokee tena. Haya yote ni kwa sababu ya woga na hofu ya kumwona mfu. Hali hiyo iliwatokea wafuasi wa Yesu. Hawakwenda kwa mganga wa kienyeji. Ila walishangaa kuona mtu ameingia ndani ilhali milango imefungwa. Huenda walijaribu kukimbia lakini hawakuweza kwa vile milango ilikuwa imefungwa. Lakini katika wasiwasi huo walihitaji Yesu mwenyewe awaondolee mashaka. Akawaambia “Amani iwe kwenu.” Maana yake msiogope. Na akawaambia zaidi “”Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikeni-shikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo””(Lk 24:39). Maneno hayo yaliwapa wafuasi mwanga wa furaha. Yaliwarudishia imani na hasa pale Kristo Mfufuka alipowaomba chakula na wao “”Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akala mbele yao””(Lk 24:42-43). Katika hali ya hofu na mashaka tunahitaji kusikia neno “Amani.” Amani ni ishara ya upendo, na matokeo ya upendo ni msamaha. Wafuasi wa Yesu walihitaji amani ya Kristo Mfufuka na hasa baada ya kumkimbia na kumwacha siku ile ya Ijumaa Kuu. Hivyo kwa kuwaambia “amani kwenu” ni kuwaambia “msiogope.” Amani hiyo ya Kristo Mfufuka iliwapa fursa wafuasi kukumbushwa tena yanavyosema Maandiko juu ya Kristo kwamba “”atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi…””(Lk 24:46-47). Amani ya Kristo Mfufuka inawapa wafuasi wa Yesu jukumu la wao kuwa sasa ni watangazaji wa Habari Njema ya ufufuko wa Bwana, kuanzia Yerusalemu. Wafuasi wanaalikwa na kutumwa kuwa mashahidi wa habari hii ya ufufuko. Ndicho anachofanya mtume Petro katika somo la kwanza (Mdo 3:13-15, 17-19a), akiongea na Wayahudi namna walivyomfanyia Kristo, Mtakatifu, Mwenye haki walivyomtoa auawe. Hata hivyo mtume Petro anawaalika wasikilizaji wake kwamba pamoja na hayo “”Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe””(Mdo 3:19a). Kristu Mfufuka ameleta amani; ameleta msamaha hata kwa waliomtesa na kumwua. Amani ya Kristo Mfufuka, ni amani ya msamaha wa dhambi kwa kila mmoja wetu. Ndicho anachosema Mt. Yohane anapotuandikia akisema “”Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote””(1Yoh.2:1-2). Amani iwe kwenu, Amani iwe kwetu sote. Ni amani ya Kristo Mfufuka; Ni amani, ishara ya upendo, ishara ya msamaha, ishara ya umoja kati yetu na Kristo Mfufuka. Ni amani, ishara ya mwanzo wa uinjilishaji kwa mataifa yote, ishara ya toba na ondoleo la dhambi. Tunapoendelea na maadhimisho ya Pasaka, tuombe neema ya kupokea amani ya Kristo Mfufuka, na kisha hapo nasi tuwe wajumbe wa hiyo amani kwa watu wote. “

SALA: Ee Yesu utufanye vyombo vya amani yako.