Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 30/03/2024

2024 MACHI 30 : JUMAMOSI KUU
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

“SOMO 1: Mwa 1: 1 — 2: 2 au 1: 1. 26-31a
(K) Nchi imejaa fadhili za Bwana. Zab 33: 4-7. 12-13. 20-22

SOMO 2: Mwa 22: 1-18 au 22: 1-2. 9a. 10-13. 15-18
(K) Mungu unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia Wewe. Zab 16:5, 8-11

SOMO 3: Kut 14: 15 — 15: 1-6, 17-18 (lazima lisomwe)
(K) Nitamwimbia Bwana kwa maana ametukuka sana. Kut 15:1-6, 17-18

SOMO 4: Isa 54: 5-14
(K) Ee Bwana nitakutukuza kwa maana umeniiua. Zab 30:1,3-5, 10-12

SOMO 5: Isa 55:1-11
(K) Kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu. Isa 12:2-6

SOMO 6: Bar 3: 9-15, 32 — 4: 4
(K) Wewe unayo maneno ya uzima wa milele, Ee Bwana. Zab 19:7-10 (K) Yh. 6:69

SOMO 7: Eze 36: 16-28
(K) Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji. Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, ee Mungu. Zab 42:2, 4; 43:3-4

Agano Jipya
SOMO 1: Rum 6: 3-11
Zab 118:1-2, 16-17, 22-23
(K) Aleluya, Aleluya, Aleluya. “

Injili. Mk 16:1-7

Hata Sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu, mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka. Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza. Wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayevingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi? Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; Nalo lilikuwa kubwa mno. Wakaingia kaburini wakaona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe; Wakastaajabu. Naye akawaambia, msistaajabu; Mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulubiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka. Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia. Wakatoka nje, wakakimbia kutoka kaburini; kwa maana wameingia tetemeko na ushangao; wala hawakumwambia mtu neno, maana waliogopa.

TAFAKARI

UKIMYA UNA NGUVU: Mama Kanisa tangu Ijumaa Kuu alasiri, amekumbwa na ukimya na simanzi nzito kutokana na Mkuu wake, yaani Kristo kulazwa kaburini. Ni katika ukimya huu tunaona jinsi Mungu akiamua kutenda anatenda. Mungu anakamilisha pendo lake kwa mwanadamu kwa kushinda mauti na kufufuka. Masomo ya usiku huu yanaturudisha nyuma tangu uumbaji ili kutupa picha halisi ya mpango wa Mungu tangu mwanzo na jinsi mwanadamu alivyoanguka hadi kuinuliwa tena na kurudishiwa ile hadhi/heshima ya kuwa mwana wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni habari yenye mshangao mkuu kwani kwa yenyewe ni tukufu, haielezeki kiurahisi. Hata hawa wamama wa kwenye Injili pamoja na kuambiwa na Malaika, walistaaajabu, Malaika akawaambia “msistaajabu, mnamtafuta Yesu Mnazareti aliyesulubiwa, amefufuka…enendeni mkawaambie wanafunzi wake.” Kila mmoja wetu ni mjumbe wa habari njema ya Ufufuko.

SALA: Ee Yesu utujalie tushiriki furaha ya ufufuko wako.