Select Page

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 15/03/2024

2024 MACHI 15 IJUMAA: JUMA 4 LA KWARESIMA
Mt. Klementi Hofbauer, Padre
Urujuani
Zaburi: Juma 4

Somo 1. Hek 2: 1, 12-22

Wasiomsadikia Mungu walisema hivi, huku wakifikiri yasiyo kweli, Zaidi ya hayo na tumwotee mtu wa haki, maana hatuna haja naye, naye yu kinyume cha matendo yetu; atukaripia  ya kama tumeiasi torati, na kutushitaki ya kama tumekosa adabu. Asema ya kwamba anamjua Mungu, na kujiita mtumishi wa Bwana. Ametuwia magombezi ya fikra zetu. Hata kumtazama twaona ni kugumu; maana maisha yake si sawasawa na maisha ya wengine, na mwenendo wake ni wa kigeni. Tunahesabiwa naye kuwa kama madini hafifu; anajitenga na njia zetu kama na uchafu. Wenye haki wasema kuwa mwisho wao ni heri; hujivuna ya kwamba Mungu ndiye baba yake. Haya na tuone kama maneno yake ni kweli; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake; mradi mwenye haki akiwa ni mwana wa Mungu, Yeye atamtegemeza na kumwokoa mikononi mwa adui zake. Na tumhakikishe kwa jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake akidhulumiwa. Hata tumhukumu auawe mauti ya aibu, maana ataangaliwa sawasawa na maneno yake. Ndivyo walivyosemezana, wakakosea kabisa. Kwa maana uovu wao uliwapofusha; hawakuzijua siri za Mungu; wala hawakuutarajia mshahara wa utakatifu, wala kudhani ya kwamba iko thawabu kwao wenye roho zisizo na hatia.

Wimbo wa Katikati. Zab 34:17-23

1. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote. (K)

(K) Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo.

2. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
Mateso ya mwenye haki ni mengi,
Lakini Bwana humponya nayo yote. (K)

3. Huihifadhi mifupa yake yote,
Haukuvunjika hata mmoja.
Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake,
Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao. (K)

Injili. Yn 7: 1-2, 10, 25-30

Wakati ule, Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Uyahudi, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitafuta kumwua. Na sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya vibanda, ilikuwa karibu. Hata ndugu zake walipokwisha kukwea kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye alipokwea, si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri. Basi baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, ”Je, Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue? Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Yamkini hao wakuu wanajua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo? Lakini huyu twamjua atokako; bali Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako.” Basi Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, ”Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenipeleka ni wa kweli, msiyemjua ninyi. Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.” Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.

TAFAKARI

UKWELI UNAUMA: Ni tabia ya wengi kupendelea kusikia/kuambiwa maneno matamu yenye kutusifia na kutuvimbisha vichwa; hatupendi kukaripiwa na kurekebishwa pale tunapofanya sivyo. Katika somo la kwanza tumeona wahusika wanasema “atukaripia ya kama tumeasi torati na kutushitaki ya kama tumekosa adabu.” Katika Injili Wayahudi walikuwa wanamtafuta Yesu ili wamuue. Daima anayesema ukweli na kutetea haki huwa hapendwi na jamii, atachukiwa na hata wakati mwingine atazushiwa jambo la uongo ili tu kumchafulia. Jamii ya leo inapendelea zaidi mambo yanayofuatana na vionjo vyao tu na kuleta furaha ya muda angali roho inaangamia. Mtu yuko radhi adhulumu mali za wengine ili mradi mtaani aonekane ni tajiri, hata kama ni kupoteza uhai wa mtu. Wanasahau kuwa kuna maisha baada ya kifo.  Ndio maana Yesu anasema, ‘yeye aliyempeleka ni wa kweli na ametoka kwake.’ Kila mara Yesu alisimamia ukweli, nasi tunaalikwa tusimamie ukweli hata kama tutachukiwa na wengine.

SALA: Ee Mungu utujalie kusimamia ukweli siku zote.