Select Page

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 14/03/2024

2024 MACHI 14 ALHAMISI: JUMA 4 LA KWARESIMA
Mt. Matilda wa Ringelheim, Malkia 
Urujuani
Zaburi: Juma 4

Somo 1. Kut 32:7-14

Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha, wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Tena Bwana akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu; basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize; nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu. Musa akamsihi sana Bwana, Mungu wake, na kusema, Bwana, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu,  ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako. Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu, nao watairithi milele. Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake.

Wimbo wa Katikati. Zab 106:19-23

1. Walifanya ndama huko Horebu,
Wakaisujudia sanamu ya kuyeyusha
Wakaubadili utukufu wao
Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani. (K)


 (K)  Ee Bwana unikumbuke mimi,
         Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako. 


2. Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,
Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu.
Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,
Aliyetenda makuu katika Misri. (K)

3. Akasema ya kuwa atawaangamiza,
Kama Musa, mteule wake, asingalisimama,
Mbele zake kama mahali palipobomoka,
Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu. (K)

Injili. Yn 5:31-47

Yesu aliwaambia Wayahudi: Mimi nikijishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Yuko mwingine anayeshuhudia; nami najua ya kuwa ushuhuda wake anaonishuhudia ni kweli. Ninyi mlituma watu kwa Yohane, naye akaishuhudia kweli. Lakini mimi siupokei ushuhuda kwa wanadamu; walakini ninasema haya ili ninyi mpate kuokoka. Yeye alikuwa taa iwakayo na kung’aa, nanyi mlipenda kuishangilia nuru yake kwa muda.
Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohane; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma. Naye Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wo wote, wala sura yake hamkuiona. Wala neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa na yeye.
Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu. Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu. Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo.
Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti? Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika habari zangu. Lakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaamini wapi maneno yangu?

TAFAKARI

MAFANIKIO DAIMA YANAHITAJI MSIMAMO: Mwanadamu mara nyingi hupenda kujaribu na kubahatisha mambo na hii wakati mwingine hupelekea yeye kujikuta amepoteza vyote. Somo la kwanza tumeona Waisrael wanapotoka na kumwacha Mungu na kugeukia miungu mingine. Katika Injili Yesu anaweka bayana na kusema, “mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu wala hamnipokei, mwingine akija kwa jina lake mwenyewe mtampokea.” Wahenga wanasema, “miluzi mingi humpotezea mbwa mwelekeo” au “mshika mawili kwa pupa yote humponyoka.” Tunashuhudia siku hizi kila uchwao makanisa yanaibuka kila kona na kila mmoja anatumia Biblia lakini katika uhalisia ni miradi kwa manufaa binafsi ya kujitafutia hela. Mwanadamu amekosa mwelekeo na hata mafanikio ya kubaki imara kwa imani kwa Mungu hamna, amekosa msimamo, leo yupo Katoliki, kesho yuko kwingineko. Kutangatanga kumekuwa kwingi.

SALA: Yesu Mwema, utuwezeshe tudumu imara kwa imani Katoliki.