Masomo ya Misa Machi 13

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 13/03/2024

2024 MACHI 13 JUMANNE: JUMA 4 LA KWARESIMA
Mt. Eufrasia
Urujuani
Zaburi: Juma 4

Somo 1. Isa 49: 8-15

Bwana asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwaridhisha urithi uliokuwa ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza. Nami nitafanya milima yangu yote kuwa njia, na njia kuu zangu zitatukuzwa zote. Tazama, hawa watakuja kutoka mbali; na tazama, hawa kutoka kaskazini, na kutoka magharibi, na hawa kutoka nchi ya Sinimu. Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi; pazeni sauti ya kuimba, enyi milima; kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, naye atawahurumia watu wake walioteswa. Bali Sayuni alisema, Yehova ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake amnyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.

Wimbo wa Katikati. Zab 145:8-9, 13-14, 17-18

1. Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako. (K)

(K) Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma.

2. Huipeleka amri yake juu ya nchi,
Neno lake lapiga mbio sana.
Ndiye atoaye theluji kama sufu,
Huimwaga barafu yake kama majivu. (K)

3. Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua. (K)     

Injili. Yn 5: 17-30

Yesu aliwajibu Wayahudi: Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi. Basi kwa sababu hiyo Wayahudi walizidi kutaka kumwua, kwa kuwa hakuivunja sabato tu, bali pamoja na hayo alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu. Basi Yesu akajibu, akawaambia, Amin, amin, nawaambia, mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vilevile. Kwa kuwa Baba ampenda Mwana, naye humwonyesha yote ayatendayo mwenyewe; hata na kazi kubwa zaidi kuliko hizi atamwonyesha, ili ninyi mpate kustajaabu. Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana awahuisha wale awatakao. Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote, ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka. Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai.
Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake. Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu. Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu. Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.

TAFAKARI

TUSIFANYE MAAMUZI KWA HARAKA: Kuna watu wakisikia jambo hupenda kuchukua maamuzi ya haraka bila hata kufanya uchunguzi wa kutosha. Wayahudi walipanga kumuua Yesu japo alikuwa amefanya mambo machache tu pale kwao. Hapa ni kuchukua maamuzi ya haraka. Katika matukio mengine, wapo waliochomwa moto kwa tuhuma za wizi tena wa vitu vidogo tu-simu/kuku, huku ni kujichukulia sheria mkononi na kuchukua maamuzi ya haraka yasiyo na busara, hata kama mtu katenda kosa, kuna sheria na taratibu za kumwajibisha/kumwadhibu na sio kuua. Kuna usemi wa Wahenga usemao “jambo usilolijua ni kama usiku wa kiza.” Hapa tujifunze kutopenda kuchukua maamuzi ya haraka na hasa yale yahusuyo kuondoa uhai, yapo yanayotakiwa kutatuliwa kwa haraka japo busara lazima iwepo, mfano katika janga la moto ili kuokoa uhai na vitu, lazima uharaka uwepo. Je, mara ngapi tumejikuta hata tunawakwamisha wenzetu kiimani kutokana na uharaka tunaokuwa nao hata katika kutatua changamoto za kiimani.

SALA: Yesu Mwema, tuwezeshe kuwa na busara katika maamuzi yetu.

About the Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You may also like these