Select Page

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa 12/03/2024

2024 MACHI 11 JUMANNE: JUMA 4 LA KWARESIMA
Mt. Bernad wa Karinola 
Urujuani
Zaburi: Juma 4

Somo 1. Eze 47: 1– 9, 12

Malaika alinileta mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kuume wa nyumba, upande wa kusini wa madhabahu. Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji yalitoka upande wa kuume. Na alipotoka mtu yule, mwenye uzi wa kupimia mkononi mwake, kwenda masharikini, akapima dhiraha elfu, akanivusha maji yale; maji yakafika mpaka viweko vya miguu. Kisha akapima dhiraha elfu, akanivusha maji yale, maji yakafika mpaka magoti. Kisha akapima dhiraha elfu, akanivusha, maji yakafika mpaka viuno. Kisha akapima dhiraha elfu, yakawa mto nisioweza kuuvuka; maana maji yamezidi, maji ya kuogelea, mto usiovukika. Akaniambia, ”Mwanadamu, je, Umeona haya?” Kisha akanichukua, akanirudisha mpaka ukingo wa mto. Basi nikiisha kurudi, tazama, kando ya ukingo wa mto ilikuwapo miti mingi sana, upande huu na upande huu. Ndipo akaniambia, ”Maji haya yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki, nayo yanashuka mpaka Araba, na kuingia katika bahari; maji yatokezwayo yataingia baharini, na maji yake yataponyeka. Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko; maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po pote utakapofikilia mto huo. Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa.

Wimbo wa Katikati. Zab 46:2-6, 8-9

1. Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,
Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
Kwa hiyo hayutaogopa ijapobadilika nchi,
Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. (K)

(K) Bwana wa majeshi yu pamoja nasi,
       Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.


2. Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu,
Patakatifu pa maskani zake Aliye juu.
Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa;
Mungu atausaidia asubuhi na mapema. (K)

3. Bwana wa majeshi yu pamoja nasi,
Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
Njoni myatazame matendo ya Bwana,
Jinsi alivyofanya ukiwa katika mchi. (K)

Injili. Yn 5: 1-16

Baada ya hayo palikuwa na sikukuu ya Wayahudi; naye Yesu akakwea kwenda Yerusalemu. Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha, nayo ina matao matano. Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza. Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, ”Wataka kuwa mzima?” Yule mgonjwa akamjibu, ”Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.” Yesu akamwambia, ”Simama, jitwike godoro lako, uende.” Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni Sabato siku hiyo. Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwambia yule aliyeponywa, ”Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro.” Akawajibu, ”Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, ‘Jitwike godoro lako, uende.”’ Basi wakamwuliza, ‘Yule aliyekuambia, ‘Jitwike, uende, ni nani? ”’Lakini yule mtu aliyeponywa hakumjua ni nani; maana Yesu alikuwa amejitenga, kwa sababu palikuwa na watu wengi mahali pale. Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, ”Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi.” Yule mtu akaenda zake, akawapasha habari Wayahudi ya kwamba ni Yesu aliyemfanya kuwa mzima. Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwudhi Yesu, kwa kuwa alitenda hayo siku ya Sabato.

TAFAKARI

TUFURAHIE BARAKA NA MAFANIKIO YA WENGINE: Mungu hujifunua kwetu hatua kwa hatua, wakati mwingine hutumia njia ngumu kufanya hivyo na twaweza tusitambue, tunachoalikwa kufanya ni sisi kutoa ushiriki wetu kama Mt. Augustino alivyosema, “Yeye aliyekuumba wewe, bila ya wewe, hatakukomboa wewe bila ya wewe.” Huyu mgonjwa aliyeponywa alitoa ushiriki wake, Yesu alipomuuliza alijibu “sina mtu wa kunitia birikani” na alipoambiwa “simama jitwike godoro lako uende” hakubisha, alitekeleza mara moja na kizuri kingine alichofanya baada ya kupona, alirudi hekaluni kushukuru na hii ilimfanya akakamilisha uponyaji wake. Wayahudi hawakufurahishwa na kuponywa kwake, ndio maana wanamhoji juu ya kubeba godoro siku iliyokatazwa. Tupo ambao hata tukitendewa wema haturudi kushukuru, ndo imetoka hivyo. Kwenye maparokia mengi, watoto wakishapata Kipaimara, Kanisani hawakanyagi tena, labda utamuona siku ya kufunga ndoa. Tujifunze kuwa na maisha endelevu ya kiroho, tujue hamna likizo, mwisho wa hatua moja ni mwanzo wa hatua nyingine.

SALA: Ee Mungu utujkalie neema ya kufurahia mafanikio ya wengine.