Select Page

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 26/02/2024

2024 FEBRUARI 26 JUMATATU: JUMA 2 LA KWARESIMA
Mt. Alexander wa Alexandria 
Urujuani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Dan 9: 4-10

Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki ina wewe lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii.

Wimbo wa Katikati. Zab 79:8, 9-11

1. Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije kutulaki hima,
Kwa maana tumeadhilika sana. (K)

(K) Usitutende sawasawa na hatia zetu, Ee Bwana.
 
2. Ee Mungu wokovu wetu utusaidie.
Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utughofiri dhambi zetu,
Kwa ajili ya jina lako. (K)  

3. Kuugua kwake aliyefungwa na kuingie mbele zako.
Kwa kadiri ya ya uweza wa mkono wako
Uwahifadhi wana wa mauti.
Na sisi tulio watu wako, na kondoo za malisho yako,
Tutakushukuru milele;
Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi. (K)

Injili. Lk 6:36-38

Yesu aliwaambia wafuasi wake: ”Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa”.

TAFAKARI

MWENYE KUTUSTAHILISHA NI MUNGU: Ni yapi mastahili yetu mbele ya Mungu? Swali hili ni la msingi katika maisha yetu. Katika kutafuta majibu ya swali hili tutajikuta kuwa hatuna mastahili kwani sisi tu wadhambi. Pamoja na dhana hii wanadamu tumeendelea kushutumiana, kuuana, kulaumiana na hata kukosa huruma kwa wenzetu. Namna hii ya kutostahili mbele ya Mungu inaleta msukumo kwa Yesu kutukumbusha kuwa na huruma. Yesu alieleza kuwa kipimo tukitumiacho ndicho kitakachotumika kwetu pia. Nabii Danieli anaeleza wazi kuwa tumemwasi Mungu kwa kuwa hatukuitii sauti yake aliyotupatia kwa njia ya watu wake. Nabii Danieli anakiri kuwa tumetenda dhambi. Kukosa huruma kwa wenzetu, kuwahukumu wenzetu pasi mastahili ni dhambi. Wapendwa, ili tuweze kuoneana huruma ni lazima tujifunze kuonja maumivu ya watu wale tunaowatendea vibaya. Tunapokosa huruma tunazalisha chuki, ugomvi, mauaji n.k. Tufuate mfano wa nabii Danieli, tutambue makosa yetu, tujiulize kwanini hatujawahurumia wenzetu na tuwe tayari kujirekebisha.

SALA: Ee Bwana, utujalie mapendo na huruma kwa wote. amina.